HAPONI MTU

HAPONI MTU

755
0
KUSHIRIKI

 

NA EZEKIEL TENDWA

HAPA Okwi, Niyonzima na Bocco, unaponaje kwa mfano? Lakini vipi kwa upande wa Azam, kule wakiwa na Mbaraka Yusuph, huku Himid Mao na pale Yahaya Mohamed, inakuwaje hapo? Ni wazi haponi mtu kwenye Uwanja wa Azam Complex, jijini Dar es Salaam leo.

Hivyo ndivyo hali itakavyokuwa kwenye uwanja huo, unaomilikiwa na Azam FC, pale wenyeji watakapowakabili Wekundu wa Msimbazi, Simba, katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ambao kila upande umetamba kuwa lazima uibuke na pointi zote tatu.

Simba wao wana hasira kuhakikisha wanashinda mchezo huo, kwani msimu uliopita Azam FC walikuwa wababe wao, wakiwafunga bao 1-0, katika mchezo wa mzunguko wa pili, huku pia wakipokea kipigo kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi, iliyofanyika Zanzibar.

Faida kubwa waliyonayo Simba msimu huu ni kwamba, wanacho kikosi kipana, huku safu yao ya ushambuliaji ikiwa moto wa kuotea mbali kiasi kwamba, timu pinzani zikisikia zinakutana na Wekundu wa Msimbazi hao, matumbo yanawauma.

Tayari safu hiyo ya ushambuliaji ilishaonyesha umahiri wake baada ya kuibuka na ushindi mnono wa mabao 7-0 dhidi ya Ruvu Shooting, katika mchezo wao wa ufunguzi wa Ligi Kuu Bara na sasa wenyewe wanadai ni zamu ya Azam FC ‘kulala na viatu’.

Kocha Mkuu wa Simba, Joseph Omog, wala hana wasiwasi, kwani anajua kuwa Emmanuel Okwi asipowaumiza Azam, John Bocco hatawaacha salama; ikishindikana kwa hao, Mghana Nicholas Gyan atamaliza mchezo.

Pia, wapo wakali kama Juma Luizio na Laudit Mavugo ambao kwa ushirikiano na viungo mahiri kama Haruna Niyonzima, Muzamiru Yassin, James Kotei, Said Ndemla na wengineo, wanaweza kuiliza Azam kama wasipokuwa makini.

Kwa jinsi Omog alivyokuwa akiwafua vijana wake kwa wiki nzima, mchezo wa leo anaweza akaanza na kikosi hiki: Aishi Manula, Erasto Nyoni, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Method Mwanjali, Jjuuko Murushid, James Kotei, Shiza Kichuya, Mzamiru Yassin, John Bocco, Haruna Niyonzima, pamoja na Emmanuel Okwi.

Kocha msaidizi wa kikosi hicho, Jackson Mayanja, ameweka wazi kwamba, Azam FC hawana pa kutokea, ikizingatiwa kuwa wachezaji wao muhimu wamekimbilia Simba, akiwamo Bocco, ambaye msimu uliopita ndiye aliyewafungia Azam bao la ushindi timu hizo zilipokutana.

Mbali na Bocco, pia Aishi Manula pamoja na Erasto Nyoni wanatarajiwa kung’ara kwenye mchezo huo kutokana na kuwa na uzoefu na Uwanja wa Azam Complex, ambapo Mayanja anadhani kwamba, wachezaji hao ndio watakaoimaliza timu yao ya zamani.

Wakati Simba wakijinasibu hivyo, kwa upande wao, Azam FC, wamekuwa wakifanya mambo yao kimyakimya na wameahidi kwamba hawatakubali kudhalilishwa uwanja wao wa nyumbani, huku wakiringia safu yao ya ushambuliaji, inayoongozwa na Mbaraka Yusuph pamoja na Yahaya Mohamed.

Pia, safu yao ya ulinzi inaweza kuongozwa na mkongwe Aggrey Morris, huku kiungo wakiwa na injini yao, Himid Mao, atakayesaidiana na akina Frank Domayo, Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na wengine, kitu ambacho nao wanadhani kitawapa ushindi na kuondoka na pointi zote tatu.

Kulingana na mazoezi ya juzi na jana, kikosi cha Azam leo kinaweza kuwa hivi: Razack Abalora, Daniel Amoah, Bruce Kangwa, Aggrey Morris, Yakubu Mohammed, Himid Mao, Salum Abubakar ‘Sure Boy Jr’, Frank Domayo, Yahaya Mohammed, Mbaraka Yusuph pamoja na Enock Agyei.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU