TSHISHIMBI AWA MTAJI YANGA

TSHISHIMBI AWA MTAJI YANGA

2522
0
KUSHIRIKI

NA EZEKIEL TENDWA

KILA mtu ana nyota yake hapa duniani, kama ilivyo kwa kiungo wa Yanga, Papy Kabamba Tshishimbi, ambaye amegeuka kuwa mtaji kwa mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, kutokana na kandanda lake alilolionyesha tangu alipotua Jangwani.

Unajiuliza kivipi? Iko hivi! Tangu aliposajiliwa na Yanga, kiungo huyo raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), amekuwa dili kubwa, kwani kila anapokuwa uwanjani, lazima kuna faida Wanajangwani hao wataipata, kama inavyotarajiwa kutokea kesho watakapowakabili Njombe Mji mkoani Njombe.

Yanga, ambao wanataka kuweka historia mpya ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara nne mfululizo, watakuwa wageni wa Njombe Mji, mchezo utakaochezwa Uwanja wa Sabasaba, mkoani humo.

Kabla hata ya Yanga kuwasili mkoani Njombe, tayari jina la Tshishimbi lilikuwa likitajwa kila kona ya mji huo, ikiashiria kwamba hata wachezaji wa Njombe Mji watakuwa wamepewa kazi maalumu ya kuhakikisha wanadili naye ipasavyo.

Kama itakuwa hivyo, mashabiki wa Yanga hawatakiwi kuwa na wasiwasi wowote, kwani kuna kitu kizuri wanaweza wakakifaidi kupitia kukamiwa kwa Tshishimbi na wachezaji hao wa Njombe Mji.

Tshishimbi ni mmoja wa wachezaji wenye akili nyingi sana, hivyo kama Njombe Mji watamkamia, hiyo inamaanisha watamchezea faulo nyingi ambazo zinaweza kuwaathiri wapinzani wao hao kwa kupata kadi za njano na hata nyekundu.

Pia, kitendo hicho kinaweza kuwa mtaji kwa Yanga kupata mipira mingi ya adhabu karibu na lango la wapinzani wao hao na hata penalti zitakazowasaidia kuvuna mabao.

Hata katika mchezo wao wa ufunguzi dhidi ya Lipuli, Yanga walipata mipira mingi ya faulo iliyotokana na Tshishimbi kufanyiwa madhambi na wapinzani wao, lakini washambuliaji wa Wanajangwani hao hawakuwa makini kutumia nafasi hizo za mabao na kujikuta wakiambulia sare ya bao 1-1.

Faida nyingine wanayoweza kuipata Yanga kama Njombe Mji watamkamia zaidi Tshishimbi, ni kwamba wachezaji wengine, akiwamo Thaban Kamusoko, wanaweza wakamaliza mchezo mapema na mashabiki wa Wanajangwani hao, kuondoka uwanjani wakiwa wamejawa na furaha.

Uzuri wa Yanga ni kwamba, wanao wachezaji wajanja sana kiasi kwamba ukimdhibiti mmoja, wengine wanakumaliza, kitu ambacho kinaweza kikawafanya Njombe Mji kuondoka na kapu la mabao, ikizingatiwa kuwa, hawana uzoefu na michuano hii ya Ligi Kuu Bara.

Kutokana na mazoezi waliyoyafanya, wenyewe wanadai kwamba, Njombe Mji hawana pa kutokea, kwani wakimzuia Tshishimbi, Kamusoko na wengine wanamaliza kazi na kwamba wakimpa uhuru, ndiyo kwanza watakuwa wamejitafutia kiama.

Bahati mbaya waliyonayo Njombe Mji ni kwamba, Yanga walitoka sare ya kufungana bao 1-1 na Lipuli FC, kitu ambacho wanakiona kama udhalilishaji na sasa wanaingia katika mchezo huo wakiwa na hasira kubwa.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU