CIOABA AKIIMARISHA HIKI, MTAJUTA KUMFAHAMU

CIOABA AKIIMARISHA HIKI, MTAJUTA KUMFAHAMU

397
0
KUSHIRIKI

MPAKA sasa kocha wa Azam, Aristica Cioaba, amefanikiwa kufanya vitu viwili vya msingi sana katika kikosi chake, kuwapa morali wachezaji wake na kujenga ukuta imara. Kama Azam wakiufumbia macho uswahili, wana nafasi ya kufanya vizuri msimu huu kulingana na ‘fact’ hizo mbili nilizozitaja.

Mwezi uliopita kabla Ligi Kuu Tanzania Bara haijaanza, Cioaba alinukuliwa na chombo kimoja cha habari na kusema wapo tayari kwa mbio za ligi, alimaanisha walijipanga na walishajua ugonjwa wao ni upi na wautibu vipi na nguvu yao iko wapi waitumie kwa wakati gani.

Inakumbukwa kuwa Azam ilienda kuweka kambi ya ‘pre-season’ nchini Uganda na kucheza mechi tano, wakishinda tatu na kutoa sare mbili, huku mshambuliaji wao, Yahaya Mohamed, akifanya vizuri zaidi huko kwenye mechi za kujipima ubavu kwa kutupia mabao ya kutosha.

Mechi hizo zilimridhisha Cioaba, kwa mujibu wake mwenyewe na alisema kwamba alipata nafasi ya kutengeneza kikosi chake cha kwanza kwa ajili ya msimu huu, jambo jema ni kwamba alifanikiwa.

Ligi ndio kwanza iliingia wiki yake ya pili juzi kwa kila timu kucheza mechi mbili, ambapo kabla ya Yanga kuwavaa Njombe Mji jana, Simba na Azam zilichuana vikali pale Chamazi. Moja kati ya mechi zenye kukera kwa wale wasiopenda kuangalia mechi isiyo na mabao!

Sare tasa iliufanya mchezo uonekane mbovu kwa pande zote mbili. Huku lawama nyingi zikielekezwa hasa kwa benchi la ufundi la Simba kwa kuonekana kama halina mipango mbadala kutokana na kushikwa vibaya mno na vijana wa Azam waliocheza soka la nidhamu ya hali ya juu hasa eneo la ulinzi.

Cioaba juzi muda mwingi alitumia mfumo wa mabeki watatu, mara kwa mara muundo wake ukawa unabadilika kutoka 4-1-3-2 kwenda 3-4-3 hadi 3-3-3-1.

Walianza kawaida kwa mfumo wa mabeki wanne, Amoah, Kangwa, Morris na Yakubu, kabla ya mchezo kushika kasi na kuanza kutumia watu watatu mbele, Mbaraka kushoto kulia Enock na Yahaya katikati. Kiungo cha kati wakawa wanasimama watu wawili, Kingue na Sure Boy, Himid Mao akisogea pembeni kulia na Kangwa akicheza kama wing back ya kushoto. Wakati huo, huku nyuma waliwaacha mabeki watatu, Amoah, Morris na Yakubu.

Mara chache sana walitumia huo mfumo kwani Simba walionekana kushindwa kufurukuta kadiri mchezo ulivyoendelea. Cioaba alipoona hakuna madhara makubwa kutoka kwa Simba, aliamua kuifanya timu yake ijaribu kumiliki sana mpira kwenye eneo la kiungo kwa kutumia watu wa ziada.

Ndipo mfumo wa 3-3-3-1 ulipoanza kutumika kwa muda mwingi wa mchezo. Ingawa alishindwa kutimiza lengo kuu la kuizuia Simba isimiliki sana mpira, angalau anaweza kukaa leo na kujipongeza kwa kuwaacha wajisifu kwamba ‘tulimiliki sana mpira, ila bahati yao wamepona tungewafunga nyingi wale!’

Umiliki wa mpira haukupi ubingwa, bali kama unamiliki mchezo na kutengeneza nafasi na ukazitumia hizo nafasi kwa kufunga mabao, hatutakuwa na shida na wewe. Tutazitazama alama za nyakati na kutafakari jinsi gani timu yako itakavyofanya vizuri.

Azam ilifanikiwa kutoka kwenye mchezo huo bila kuruhusu bao kwa mara ya pili msimu huu. Hilo ndilo lengo lao kubwa, kutoruhusu mabao mara kwa mara. Dhidi ya Simba, alipoutumia mfumo wa 3-3-3-1, alikuwa na walinzi takribani sita!

Ukiwatoa wale mabeki watatu waliokuwa nyuma, Himid na Kingue kiasili ni viungo wakabaji na wana uzoefu mkubwa tu. Kangwa ambaye ni beki wa kushoto alikuwa akifanya majukumu ya ulinzi zaidi licha ya kwamba alichezeshwa kama wing back. Kitu ambacho kilimhakikishia Cioaba kuwa ana ulinzi imara sana.

Wengi walisema kwamba kama angekuwepo Emmanuel Okwi, Simba isingepata shida jana ya kutofunga mabao. Wako sahihi sana, kwani Okwi kazi yake ni kufunga na kuisaidia timu yake ipate ushindi. Lakini, waliitazama vizuri Azam ilivyocheza juzi? Waligundua kitu gani ambacho Cioaba alikifanya kwenye ule mchezo? Kama walikuwepo Kichuya, Gyan na Bocco na mipira ikashindwa kutinga nyavuni, ni uhakika wa asilimia ngapi kwamba angekuwepo yeye mabao yangefungwa ya kutosha?

Nashawishika kulisema hili mapema kuwa Azam ipo vizuri kiulinzi. Ila kama kuna kitu mbadala kitakachowapa jeuri zaidi ni washambuliaji kuamka kutoka usingizini. Hilo ni jukumu la kocha Cioaba, kuamsha makali ya Yahaya, Enock na akina Mbaraka, kwani hiki ndicho kipindi kizuri cha kushinda michezo ya awali wa ligi ili kujiweka kwenye mazingira ya kujiamini kabla msimu haujashika kasi. Na iwapo atafanikiwa kurudisha makali hayo jumlisha na uimara wa ulinzi na viungo dhabiti, Azam itawafurahisha na kukera wengi msimu huu.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU