GYAN TUMSUBIRI, SIMBA WATACHEKA SANA TU

GYAN TUMSUBIRI, SIMBA WATACHEKA SANA TU

1956
0
KUSHIRIKI

NA ZAINAB IDDY

UWEZO wa hali juu ulioonyeshwa na kiungo mshambuliaji mpya wa Simba, raia wa Ghana, Nicholas Gyan, katika mchezo wake wa kwanza wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Azam, umewapa jeuri mashabiki wa timu hiyo wakitamba iwapo nyota wao huyo atapewa muda, atakuwa moto wa kuotea mbali.

Gyan amejiunga na kikosi cha Simba katika kipindi cha usajili msimu huu, ambapo juzi ndio alianza kukinukisha katika ligi hiyo baada ya kuukosa mchezo wa kwanza dhidi ya Ruvu Shooting uliopigwa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam na timu yake kushinda mabao 7-0.

Katika mchezo huo wa juzi uliochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam, Gyan aliyecheza nafasi ya winga alionekana kuwa moto wa kuotea mbali kwa mabeki wa Azam, akishambulia na kutengeneza nafasi nyingi za kufunga mabao ambazo zilishindwa kutumiwa vyema.

Ilikuwa ni dakika ya nne tu ya mchezo huo, pale Gyan ‘alipowa-beep’ mashabiki wa Simba kwa kuunganishwa kiufundi kwa kichwa krosi ya John Bocco, lakini mpira ulipanguliwa na kipa wa Azam, Mghana mwenzake Razack Abalora na kuwa kona tasa.

Kwa muda wote wa mchezo huo, mashabiki wa Simba walionekana kumkubali Gyan baada ya kuonyesha kiwango cha hali ya juu, ambapo ndani ya dakika 79 alizokuwapo uwanjani, alipiga pasi 20 zilizofika kwa walenga, huku tano pekee zikipotea.

Kutokana na uwezo aliouonyesha Mghana huyo, mashabiki wa Simba wameonekana kumkubali, wakisikika kutaka aendelee kupewa nafasi ili aweze kuzoeana na wenzake.

“Gyan ni mchezaji mzuri sana, mchezo wake wa kwanza ameonyesha kitu cha ziada, naamini kama akiendelea kuaminiwa zaidi, atakuwa na msaada sana katika kikosi chetu msimu huu,” alisema mmoja wa mashabiki waliokuwa uwajani hapo huku akiungwa mkono na wenzake lukuki.

 

 

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU