TUKIANZIA ZILIPOISHIA SIMBA, AZAM TUTAFIKA

TUKIANZIA ZILIPOISHIA SIMBA, AZAM TUTAFIKA

367
0
KUSHIRIKI

 

SIMBA na Azam juzi zilivaana katika mchezo wa raundi ya pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Azam Complex, uliopo Chamazi, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

Mchezo huo ulioishia kwa suluhu, ulikuwa na ushindani wa hali ya juu hivyo mwisho wa siku kutoa bonge la burudani kwa mashabiki waliofika kwenye uwanja huo, lakini pia wale waliokuwa wakiufuatilia kupitia runinga.

Japo timu hizo hazikufungana, lakini kutokana na kandanda lililoonyeshwa na kila upande, kila mdau wa soka alijikuta akiwa roho kwatu kwani wachezaji walionyesha kila walichojaliwa na Mwenyezi Mungu kwa muda wote waliokuwapo uwanjani.

BINGWA ambao tulikuwapo uwanjani hapo tangu asubuhi, tuchukue nafasi hii kuzipongeza timu hizo, lakini pia wachezaji na mashabiki wa pande zote mbili kwa uanamichezo waliouonyesha.

Kwa upande wetu tunaamini iwapo wachezaji wa timu zote zinazoshiriki Ligi Kuu Bara msimu huu zitaanzia pale zilipoishia Simba na Azam pale Chamazi juzi, ni wazi soka letu linaweza kupiga hatua na kufikia kule ambako kila mmoja wetu anatarajia.

Ikumbukwe kuwa kwa muda mrefu Tanzania imekuwa ikizorota kisoka kwenye anga ya kimataifa kutokana na sababu mbalimbali, ikiwamo utovu wa nidhamu wa wachezaji, viongozi na hata mashabiki wa mchezo huo.

Lakini pia, suala zima la wachezaji kutojituma kadiri ya uwezo wao, imekuwa ni sababu mojawapo inayoifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zilizopo chini mno katika viwango vya soka vya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa).

Hivyo basi, tunapoelekea raundi ya tatu ya Ligi Kuu Bara wiki hii, ni vema wachezaji wa timu zote 16 kujipanga vilivyo kuona ni vipi wanawatendea haki mashabiki wao kama ilivyokuwa kwa wenzao wa Simba na Azam juzi.

Tunaamini kama wachezaji na timu zetu wakiamua kucheza soka, basi ligi yetu inaweza kufika mbali zaidi ya mahali ilipo kwa sasa.

Kwa kuwa ligi yetu inaonekana katika mataifa mbalimbali barani Afrika kutokana na kuonyeshwa ‘live’ na runinga, hali hiyo itasaidia kuwavutia mashabiki wengi watakaokuwa wakitamani kuifuatilia kwa karibu ili kujionea burudani na vipaji vilivyosheheni kwa baadhi ya wachezaji wetu badala ya kushuhudia mieleka, kareti na vitendo vya utovu wa nidhamu.

Kwa kuonesha kandanda safi, pia inaweza kuwa njia mbadala kwa wachezaji wetu kuwavutia mawakala wanaosaka vipaji ili kuvinadi katika mataifa mbalimbali, zaidi ikiwa ni barani Ulaya.

 

 

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU