ARUSHA WALIVYOTHIBITISHA SEDUCE ME SI YA KITOTO

ARUSHA WALIVYOTHIBITISHA SEDUCE ME SI YA KITOTO

512
0
KUSHIRIKI

NA ZAINAB IDDY

USIKU wa Jumamosi ya wiki iliyopita, Jiji la Arusha lililipuka kutokana na burudani ‘bab kubwa’ iliyotolewa na wasanii wa hapa nchini katika tamasha kubwa la muziki la Fiesta, lililozinduliwa rasmi mkoani humo.

Tamasha hilo mwaka huu limepewa jina la Tigo Fiesta-Tumekusoma ambapo wasanii mbalimbali wamepata nafasi ya kutumbuiza katika majukwaa mbalimbali ambako tukio hilo litafanyika.

Katika uzinduzi huo jijini Arusha, wasanii waliopata nafasi ya kupanda jukwaani na kutoa burudani ni pamoja na kundi la Weusi, Vanessa Mdee, aliyewapagawisha wakazi wa Arusha kwa kibao chake cha Don’t Bother pamoja na Ali Kiba aliyeimba wimbo wa ‘Seduce Me’ zaidi ya mara tatu.

Japo wote waliopanda jukwaani walipagawisha, lakini Kiba na wimbo wake wa Seduce Me, ndiye aliyetia fora kiasi cha mashabiki kumtaka kupanda jukwaani zaidi ya mara moja ambapo walikuwa wakiuimba wimbo wake huo na kuucheza kwa umahiri.

Ama kwa hakika, wakazi wa Arusha wamethibitisha kuwa watu wanaoufagilia wimbo huo, wakiwamo wanasiasa maarufu hapa nchini, viongozi, wasanii na mastaa mbalimbali, hawajakosea kummwagia sifa mkali huyo wa Bongo Fleva kwa ‘ngoma’ yake hiyo matata.

Mbali ya Kiba, wasanii wengine waliopanda jukwaani siku hiyo walikuwa ni Weusi, Roma, Rostam, Darassa, Stamina, Chegge, Bilnas, Ben Pol, Dogo Janja, Rich Mavoko, Country Boy, Lulu Diva, Vanessa, Maya, Feza Kessy, Jux, Msaga Sumu na Bright.

Wengine ni Ray Vanny, Shilole, For Q ‘Ngosha the Don’, Madee, Saida Karoli, Ditto, Christian Bella, Harmonize, Foby, Mr. Blue na Nandy.

Ikiwa ni mwaka wa 18 tangu kuanzishwa kwa tamasha hilo, limeweza kuibua wasanii wengi ambao kwa sasa wanaonekana kuleta changamoto katika soko la muziki wa kizazi kipya.

Ingawa Fiesta inachukuliwa kama sehemu ya burudani kwa watu wengi, lakini ina maana kubwa kwa wasanii wachanga ambao wana nia ya dhati kutoka kimaisha kupitia muziki.

Inakumbukwa miaka iliyopita wapo wasanii wachanga waliopata nafasi ya kupanda jukwaani na kuonyesha uwezo wao hivi sasa ni wanamuziki wakubwa wanaotoa ushindani kwenye soko la muziki wa Bongo Fleva.

Miongoni mwao wapo Fiesta ni pamoja na Erick Msodoki ‘Young Killar’, Faustina Charles ‘Nandy’, Billnas, Lulu Abbas ‘Lulu Diva’, Elias Barnaba ‘Barnaba’ kabla hajajiunga na Nyumba ya Vipaji Tanzania (THT), Abduazizi Chende ‘Dogo janja’, Amin Mwinyimkuu na wengineo.

Kutokana na ukweli huo ni wakati wa wasanii wachanga wanaopata nafasi ya kuonyesha uwezo wao kufanya kile wanachostahili ili waweze kuyafikia malengo ya kuwa wanamuziki wakubwa ndani na nje ya Tanzania kama ilivyokuwa kwa wenzao.

Kwa wasanii wachanga ni jambo jema kuitumia fursa hii kuhakikisha wanatengeneza nafasi ya ajira kwao kwani kupitia tamasha hilo upo uwezekano wa kupata kampuni au vikundi vya muziki vitakavyohitaji kuwaendeleza mfano mzuri kile cha THT.

Wapo watakaodharau tamasha la Fiesta, lakini ni lazima wafahamu kuwa kuna watu wengi wanahitaji nafasi hata ya kupanda tu jukwaani kuonekana na watu lakini hawakuweza kuipata kutokana na sababu mbalimbali zilizo nje ya uwezo wa waandaaji au wahusika wenyewe.

Si jambo jema kuona wasanii wageni kwenye muziki wanaopata nafasi ya kuonyesha uwezo wao wakitoka patupu wakati kila dhana ya kuwafikisha sehemu walizokuwepo akina Dogo Janja, Barnaba na wengi wanazo.

Juu ya shoo iliyofanyika Arusha mwishoni mwa wiki iliyopita lililofanyika kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Kaimu Meneja wa Tigo Kanda ya Kaskazini, Henry Kinabo, anasema msimu wa Fiesta ndio umeanza mkoani humo na hii ni kutokana na kuitikia wito wa watu baada ya miaka mingi kutofanyika.

“Msimu huu Tigo Fiesta itazunguka mikoa 15 nchi mzima na kama tunavyojua jinsi tunavyojali na kuwapenda wateja wake na wale wenye kadi zao ambazo  hawazitumii huu ndio muda wa kuzitumia kwani tuna vifurushi ambavyo mteja akinunua tiketi yake atanufaika hivyo tunawasihi wote wajitokeze na kufurahia huduma zetu,” anasema Kinabo.

Anasema baada ya Arusha, tamasha hilo litaelekea Kahama, Mwanza, Dodoma, Mbeya, Singida, Kilimanjaro na mikoa mingine ambapo itahitimishwa jijini Dar es Salaam.

 

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU