GOODLUCK GOZBERT MAISHA YAKE YA NDOA, KIDUNIA, MUZIKI WA INJILI

GOODLUCK GOZBERT MAISHA YAKE YA NDOA, KIDUNIA, MUZIKI WA INJILI

780
0
KUSHIRIKI

NA JESSCA NANGAWE

JINA la Goodluck Gozbert si geni miongoni mwa wapenzi wa burudani hasa wale wa nyimbo za Injili (Gospel), kutokana na umahiri wake wa kulitumia vyema jukwaa pale anapohitajika kufanya kazi ya Mungu.

Mtumishi huyu wa Mungu ameendelea kusikika zaidi kwenye midomo ya watu kutokana na nyimbo zake kufanya vizuri kama ‘Ipo Siku’, Acha Waambiane, Shukrani na nyingine nyingi ambazo zimeonekana kupokelewa kwa kasi zaidi katika maeneo mbalimbali.

Gozbert mbali na kuimba nyimbo za kumtukuza Mungu pia ni mtunzi mzuri wa nyimbo za Bongo Fleva, ambapo nyimbo kama Moyo Mashine ya Ben Pol na ile ya Baraka alizozitunga, nazo zimepokelewa vyema na mashabiki wa muziki.

Uwezo wa Gozbert umeweza kumkutanisha na watu mbalimbali ambao wametamani kufanya naye kazi, huku akipata nafasi ya kushiriki kwenye matamasha mbalimbali ambayo yamezidi kuimarisha jina lake ndani na nje ya Tanzania.

BINGWA lilipata nafasi ya kufanya naye mahojiano ambapo alizungumzia mambo mbalimbali ya maisha yake, ndoa, familia na mikakati yake ya baadaye katika kuiendeleza kazi ya Mungu.

HISTORIA YAKE

Gozbert ni mtoto wa mwisho kwa familia yake ya watoto wanne akiwa ndiye mtoto pekee wa kiume, huku akitanguliwa na wadada watatu, Jessica, Yasintah na Godliver ambapo hakuweza kulelewa na baba yake mzazi ambaye alifariki yeye akiwa na mwaka mmoja tu.

Gozbert alianza shughuli za uimbaji mwaka 2005 akiwa na Tumaini Choir (K.K.K.T-Imani) ya mkoani Mwanza na kuanza kuimba pekee yake mwaka 2008. Alitoa album yake ya kwanza Agosti 19, mwaka 2008 aliyoifanya chini ya studio za Ujumbe Records.

Mwaka 2012 alirekodi album yake ya pili aliyoipa jina la ‘Nimeuona’, moja ya nyimbo zilizomtambulisha vyema. Ukiachana na kuimba Gozbert ana uwezo wa kupiga vyombo mbalimbali vya muziki kama kinanda, guitar, drums na tarumbeta.

Kushiriki nyimbo za Bongo Fleva

Gozbert anasema yupo kwa ajili ya kumtumikia Mungu na kuinua mioyo iliovunjika, hivyo ajawahi kupendezwa kuitwa mwandishi wa Bongo Fleva, yeye huandika mashairi ya kuelimisha tu na kitendo cha kuwaandikia kina Ben Pol mashairi ni sehemu ya majukumu yake ya kuelimisha.

“Kuna mashairi mengi huimbwa na wanamuziki wa ‘gospel’ yangeimbwa na mtu wa Bongo Fleva tungesema ni nyimbo za Bongo Fleva na kinyume yake ni hivyo hivyo, sioni kama ni kosa mimi kufanya hivyo ikiwa kipaji changu kinaruhusu,” anasisitiza Gozbert.

Gozbert anasema hafanyi biashara ya kuandikia watu ngoma za Bongo Fleva na nyimbo alizoziandika kwa Mo-Music, Baraka Da Prince na Ben Pol ni mazingira ya wao tu kama marafiki yaliteleza kuzalisha yeye kufanya hivyo, kwa hiyo yeye hawa watu kwake si kama wasanii wa Bongo Fleva bali ni marafiki wa karibu.

MAISHA YA NDOA

Gozbert anasema anaamini mke mwema hupangwa na Mungu, hivyo akiwa kama mtumishi wa Mungu anategemea kupata mke aliye bora ambaye atakua amepangiwa kuishi naye.

“Kwa sasa sifikirii kuwa na familia kwa kuwa naamini wakati wa Bwana haujafika na mke wangu yupo anaandaliwa na Mungu wakati wake ukifika nitamfahamu ni yupi.”

NJE YA MUZIKI

Mwimbaji huyo anafafanua kuwa ukiachilia kazi yake hiyo anaamini Mungu anamtengeneza kuja kufanya kazi nyingine, mbali na uimbaji ambayo itakuwa ni sehemu ya kueneza neno lake.

“Naamini nina karama nyingine mbali ya hii niliyonayo, kwanza sikuwahi kufikiria kama nitakuja kuwa mwimbaji, najua kuna kingine Mungu amenipangia zaidi ya hiki ninachokifanya kwa sasa…pia napenda sana mambo ya kuhubiri neno la Mungu,” anasema.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU