NAY: KUNIFANANISHA NA MADEE NI SAWA NA KUMFANANISHA MAYWEATHER NA CHEKA

NAY: KUNIFANANISHA NA MADEE NI SAWA NA KUMFANANISHA MAYWEATHER NA CHEKA

469
0
KUSHIRIKI

NA GLORY MLAY

WASANII wengi nchini wanafanya kila njia ili kufanya soko la muziki lisipotee, kama ilivyo kwa tasnia ya filamu, ambayo inaelezwa kupoteza mwelekeo.

Juhudi, kujiamini na kutokukata tamaaa ni moja ya sifa za msanii ambaye anapambana kuhakikisha anafanya vizuri kitaifa na pia kazi zake kujulikana hata nje ya nchi.

Wasanii wengi wamekuwa wakishindwa kuzungumza ukweli kuhusu maisha yao ya sasa, lakini baadhi yao, hasa wa ‘hip hop’, wamekuwa wakiweka wazi kuhusu changamoto mbalimbali zinazowakumba.

Emmanuel Elibariki ‘Ney wa Mitego’, ni miongoni mwa wasanii wa hip hop wanaofanya vizuri hapa nchini kutokana na mtindo wake wa uimbaji.

Msanii huyo wiki iliyopita alitembelea ofisi za New Habari (2006) Limited, wazalishaji wa magazeti ya BINGWA, DIMBA, MTANZANIA, RAI na THE AFRICAN, zilizopo Sinza Kijiweni, jijini Dar es Salaam, ambapo alifanya mahojiano na waandishi wa magazeti hayo na kufunguka mengi, huku kitamba kuwa hakuna msanii anayeweza kumfunika.

BINGWA: Tumeona umetoa nyimbo tatu kwa wakati mmoja, kwanini imekuwa hivyo?

Nay: Muziki unahitaji chuma cha moto, hiki ni kipindi cha baridi, kwahiyo unatakiwa utoe vitu vya moto, ukitoa leo, unatoa na kesho, ili soko lisipoe na mashabiki wasichoke kusubiri. Kutokana na ubaridi huo, hapa ndipo hujulikana msanii wa kweli ni yupi na mbabaishaji ni yupi.

BINGWA: Kumekuwa na ubishi mitaani kwamba kati yako na Madee ni nani hasa ni Rais wa Manzese?

Nay: Kunifananisha na Madee ni sawa na kumfananisha Mayweather (Lloyd-bondia asiyepigika wa Marekani) na Francis Cheka (bondia wa Tanzania), hicho kitu hakiwezekani wala kutokea, maana itakuwa kituko.

BINGWA: Katika nyimbo zako ulishawahi kuandikiwa mistari na wasanii wengine?

Nay: Nimeshaandikiwa na vijana wangu ambao wapo studio, siwezi kuandika, mara nyingi wazo langu natoa kichwani namwelezea mtayarishaji anatengeneza ‘beat’ na pale ninaposhindwa, wananiongezea maneno; mfano wimbo wa Cheza, mistari mingi kaandika Rich Mavoko.

BINGWA: Kwanini nyimbo zako nyingi huwa unamshirikisha Rich Mavoko, ukizingatia yupo lebo ya WCB inayomilikiwa na Diamond na siyo wasanii wengine waliopo pale?
Nay: Mavoko anajitambua na anatambua nini anataka, watu kama hao ndio napenda kufanya nao kazi, yeye ana kiu ya kutafuta na kufika mbali, sina budi kumpa sapoti, hata wengine wakijitokeza wenye njaa ya mafanikio lazima nitawasapoti.

BINGWA: Kwanini unapenda sana kutumia wasichana wengi kwenye video zako.

Nay: Wasichana ni kivutio kikubwa katika muziki, ukifanya video bila wasichana wengi jua kuwa hiyo haitafanya vizuri sokoni, lakini ukiwashirikisha kwenye video hupendwa na hufanya vizuri pia.

BINGWA: Kitu gani kwenye maisha yako kiliwahi kukuumiza na hutoweza kukisahau na kipi kilichokupa furaha?
Nay: Sitaweza kuisahau siku naambiwa yule mtoto wangu wa kike siyo wangu, nilichanganyikiwa, nilikaa siku nne bila kula, niliamua kwenda kupima DNA na hapa nikaambiwa mpaka wiki nne, yaani mwezi mzima… nilizidi kuchanganyikiwa kabisa, nikaamua kumchukua nikakimbilia hotelini, nikalala naye mpaka siku iliyofuata, wakati huo akiwa na miezi mitatu tu.

Pia, nakumbuka nilikaa miaka mitano bila kuongea na mama yangu wala kuwasiliana naye, baada ya kuingia kwenye muziki na kujifanya ninajua, nikaanza kujitegemea kila kitu bila msaada wa mtu, lakini maisha hayakwenda sawa, nikaamua kurudi kwa mama, nikaomba msamaha na kunibarika kwa kazi niliyokuwa nafanya na nikaanza kufanikiwa mpaka leo.

BINGWA: Mbali ya muziki, unafanya biashara gani inayokuingizia kipato?

Nay: Binafsi nina magari ya shule na ya mikoani, pia nimejikita katika kilimo cha mazao mbalimbali.

BINGWA: Kama msanii mkubwa, je, katika mafanikio yako ulishawahi kuishirikisha jamii?

Nay: Mafanikio yangu yanakuja kutokana na baraka za watu katika jamii, nina vituo vitatu vya watoto yatima, haipiti mwezi au miezi miwili bila kupeleka vyakula, pia hata mtaani tunasaidiana na majirani na ndugu, ndiyo maana ninazidi kubarikiwa.

BINGWA: Tulisikia unajenga kanisa, vipi hiyo ishu imeishia wapi?

Nay: Kanisa ninajenga na linakaribia kumalizika, nimepata michango kutoka kwa watu mbalimbali, pia mchungaji Gwajima alisema atatoa mchango, imani yangu ndio iliyonituma kumjengea Mungu kanisa ili watu wapate kumwabudu.

BINGWA: Ndani na nje ya nchi wewe ni shabiki wa timu zipi?

Nay: Hapa nyumbani ni shabiki wa Yanga damu tokea utotoni, naipenda sana timu hiyo, huniambii kitu na nje ni Arsenal, yaani japo kwa sasa haifanyi vizuri kwenye Ligi Kuu England, lakini siwezi kuiacha.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU