NI WAKATI WA KUWEKEZA KWENYE NDONDI

NI WAKATI WA KUWEKEZA KWENYE NDONDI

351
0
KUSHIRIKI

PAMOJA na ukweli kuwa soka ndio mchezo unaopendwa zaidi duniani, kwa hapa nchini umeshindwa kuwatendea haki Watanzania kutokana na timu zetu kuboronga katika mashindano ya kimataifa.

Tangu timu yetu ya Taifa ‘Taifa Stars’ ilipofuzu fainali za Afrika mwaka 1980, timu hiyo haijawahi kufika mbali kwenye anga ya kimataifa zaidi ya kuishia hatua za awali.

Hali imekuwa hivyo miaka nenda miaka rudi pamoja na soka kupewa kipaumbele na Serikali takribani zote nne zilizopita tofauti na ilivyo kwa michezo mingine.

Ni kutokana na hali hiyo, Watanzania wapenda michezo wamekuwa wakisononeka na kufikia kukata tamaa ya kushabikia timu zao, kuanzia zile za klabu hadi za Taifa na kuamua kuhamishia mapenzi yao kwa timu za Ulaya.

BINGWA tukiwa kama wadau wa soka, tumekuwa tukigushwa na kuendelea kudorora kwa soka letu, pamoja na mchezo huo kupewa sapoti ya hali ya juu kutoka kwa mtu mmoja mmoja, taasisi, mashirika, kampuni na hata Serikali.

Lakini pia, kwa kuwa tu-wadau wa michezo mingine, tunadhani kuna umuhimu wa Watanzania kuhamishia hisia zetu katika michezo mingine kama ndondi, riadha, mpira wa kikapu, netiboli, voliboli, kuogelea na hata mieleka.

Tunadhani iwapo michezo hiyo, hasa ndondi na riadha itapewa sapoti kama ilivyo katika soka, inaweza kutuletea heshima kubwa kama ilivyokuwa zamani enzi za wanariadha Filbert Bayi na wenzake pamoja na mabondia Emmanuel Mlundwa, Michael Yombayomba, Habibu Kinyogoli ‘Masta’, Stanley Mabesi ‘Ninja’, Rashid Matumla ‘Snake Boy’ na wengineo.

Kwa bahati nzuri, angalau riadha wana sehemu ya kujinoa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ambako iwapo watapewa sapoti, wanaweza kujipanga upya na kuitangaza vema Tanzania katika anga la kimataifa.

Lakini kwa ndondi ni ‘shida’, hakuna ukumbi wowote rasmi wa kisasa unaoweza kutumika kuwaandaa vilivyo vijana chipukizi wenye ndoto za kufuata nyayo za akina Mlundwa.

Wenye mapenzi na mchezo huo wamekuwa wakijifunza katika mazingira na vifaa duni, huku wakikosa msaada wa kitaalamu. Pamoja na hilo, tumeshuhudia kama si kusikia bondia wetu chipukizi, Ibrahim Class, akifanya kweli kwenye anga ya kimataifa hivi karibuni.

Ni kutokana na hali hiyo, tunadhani kuna umuhimu wa kuanza kwa kujenga ukumbi wa kisasa wa ndondi ili kutoa fursa kwa vijana wenye vipaji kujiendeleza, lakini pia wakipatiwa msaada wa wataalamu na vifaa vya kisasa pia.

Tumalizie kwa kuwasisitiza Watanzania, kuanzia Serikali, mashirika, kampuni na wadau mmoja mmoja kuona umuhimu wa kuisaidia michezo mingine nje ya soka, zaidi ikiwa ni ndondi ambao angalau ulishaitangaza nchi yetu kimataifa miaka iliyopita kama ilivyokuwa kwa riadha.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU