TFF YAITAKA STAND UNITED KULIPA MIL 71.7/-

TFF YAITAKA STAND UNITED KULIPA MIL 71.7/-

1859
0
KUSHIRIKI

NA ZAINAB IDDY

KLABU ya Stand United ya mjini Shinyanga, imetakiwa kulipa kiasi cha Sh milioni 71.7 kabla ya Oktaba mwaka huu, zikiwa ni fedha za usajili na mishahara ya wachezaji wake.

Agizo hilo limetolewa na Kamati ya Sheria, Katiba na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) chini ya Mwenyekiti wake, Elias Mwanjala.

Mwanjala alisema kuwa baada ya kamati yao kukutana na kuangalia mashauri yaliopelekwa mezani kwao, wamebaini uhalali wa Stand United kulipa kiasi hicho cha fedha.

“Tumeangalia vielelezo mbalimbali vilivyoletwa na wanaodai pamoja na kuwasiliana na uongozi wa Stand wenyewe na kuona ni kweli wachezaji wanadai na wana haki ya kulipwa tena kwa wakati tofauti na hapo, itabidi tuwasiliane na bodi ya ligi ikiwezekana zikatwe katika fedha za milangoni au zile zinazotolewa na wadahamini,” alisema.

Alisema fedha hizo zimetokana na madai ya wachezaji, Adam Kingwande anayedai kiasi cha Sh milioni nane za usajili pamoja na Sh milioni 56 za mshahara wa miezi nane, yupo pia Sospeter Kasola anayetakiwa kulipwa Sh milioni tatu za usajili pamoja na Sh milioni 2.1 za mshahara wa miezi sita.

Wengine ni Jacob Massawe anayedai fedha za usajili kiasi cha Sh milioni 13 na mshahara wa miezi minne sawa na Sh milioni nne, wakati Adeyum Ahmed anaedai  kiasi cha milioni 24 za mshara na usajili, huku Seleman Selembe akidai fedha za usajili Sh milioni nane pamoja na milioni nne za mshahara.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU