WASTARA AGEUKIA MUZIKI, ATOKA NA KITU MAMA AFRIKA

WASTARA AGEUKIA MUZIKI, ATOKA NA KITU MAMA AFRIKA

289
0
KUSHIRIKI

NA KYALAA SEHEYE

BAADA ya kufanya vyema kwenye tasnia ya filamu na kampuni yake ya Wajey, msanii Wastara Juma, sasa ameamua kuwaonyesha mashabiki wake kuwa anaweza pia kuimba, baada ya hivi karibuni kuachia wimbo wake wa Mama Afrika, ambao unazungumzia thamani ya mwanamke wa Kiafrika na shida anazopitia.

Wastara, ambaye ni mlemavu wa mguu na mke wa marehemu Juma Kilowoko ‘Sajuki’, amefafanua kuwa, mwanamke wa Kiafrika anapitia katika shida nyingi mno, hasa akiwa mjane.

“Lazima tufahamu thamani ya mwanamke wa Kiafrika, tuondoe mila potofu kwa akina mama, kwani wanaweza kusimama na kufanya mambo makubwa, wanachotakiwa kupewa ni nafasi ambayo wanaikosa na kukandamizwa, kitu ambacho huwa kinamuumiza sana moyo wake,” anasema Wastara.

Udhalilishaji anaofanyiwa mwanamke mjane, hasa wa Afrika ni kitu cha kulaaniwa na kutokomezwa, kwani mwanamke anaweza kusimama kama ataamua, hata kama hana mume na hii inatokana na kujipanga namna atakavyolea watoto wake, hayo yote ameyaelezea katika wimbo wake huo ambao tayari umeshaanza kusikika katika vyombo mbalimbali na mitandaoni pia.

“Wimbo wangu nimefanya kwa usimamizi wa Wajey, hii ndio mara yangu ya kwanza, ila nimefanya kazi ya uhakika na nzuri ambayo imebeba ujumbe mzito unaogusa dunia kwa ujumla, ikumbukwe kwamba, mleta amani ni mwanamke na mvunja amani pia ni mwanamke,” anasema Wastara.

Aidha, Wastara anasema mashairi mengi ya wimbo huo ni matukio yaliyowahi kumtokea yeye mwenyewe na mengine ameyaona kwa baadhi ya watu wake wa karibu na baadhi ya nchi alizozunguka ikamsukuma kutunga wimbo ambao unabeba ujumbe.

“Mimi naamini mwanamke ndiyo ngao ya dunia, akitetereka basi dunia yote itayumba, nikaona hamna budi kuielimisha jamii kwa wimbo ambao utatoa funzo na sio hadi uimbe mapenzi na nyimbo zisizoeleweka ndiyo uonekane umeimba,” anasema Wastara.

Akizungumza na BINGWA, jijini Dar es Salaam juzi, Wastara anasema kuwa, alipokuwa nchini Sweden ameweza kujifunza vitu vingi mno kwa wanawake wa nchi hiyo na ndipo alipojiunga katika chama cha wanawake wa Tanzania waishio huko, kutokana na changamoto alizopitia na kufanikiwa kuzivuka salama wameamua kumteua kuwa Mwenyekiti wa chama hicho.

Aliongeza: “Nilifurahi mno nilipochaguliwa na hasa vigezo walivyovitumia, ni kweli nimepitia changamoto nyingi tangu kufiwa na mume wangu, ningekuwa mwanamke legelege basi hadi leo hii ningekuwa nimesahaulika au pengine ningekuwa ombaomba wa hali ya juu, ila namshukuru Mungu na huu siyo kwangu tu, kuna wanawake wengi mno wanaopigania haki.

“Ninachokiomba ni kupendana, huku tukijali kwa njia ya kweli shida zetu, nina uhakika hakutakuwa na vilio kwa wanawake wajane au waliotelekezwa, mwanamke ni nguzo ya Taifa na dunia kwa ujumla.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU