YALIYOMKUTA HERITIER WATANABE JIJINI PARIS (2) (NA NOAH YONGOLO

YALIYOMKUTA HERITIER WATANABE JIJINI PARIS (2) (NA NOAH YONGOLO

402
0
KUSHIRIKI

(NA NOAH YONGOLO

KONA ya Bolingo (KB) ikiwa ndani ya viunga vya Jiji la Kinshasa ndani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), inakuletea mwendelezo wa stori ya mwanamuziki Heritier Bondongo Kabeya ‘Wata Plus’.

Wiki iliyopita tuliona jinsi dogo huyo alivyopata ‘kashkash’ kutoka kwa Wakongomani wenye msimamo mkali waishio barani Ulaya Combattants, walipozuia shoo yake iliyokuwa ifanyike ndani ya Ukumbi wa Olympia, jijini Paris, Ufaransa.

Wakati mashabiki wake wakisherehekea kwa kupiga mitungi na kuruka ‘debe’ kwenye club za disco usiku kucha wakiamini shoo ingefanyika, upepo ulibadilika.

Combattants waliamua kutuma video zao kwenye mitandao ya Facebook na Youtube wakisisitiza kuzuia shoo isifanyike kwa namna yoyote ile, wakiwasihi raia wote nchini humo na wale waliotoka nchi za jirani kutulia majumbani mwao.

Pamoja na kutoa angalizo lao hilo, waliamua kuwatisha wamiliki wa Ukumbi wa Olympia kuwa watafanya vitendo vya kigaidi na kisha kuuchoma moto ukumbi huo.

Uongozi wa ukumbi huo ulikuwa ukipokea simu za vitisho pamoja na barua pepe (emails) kila baada ya muda mfupi.

Uongozi wa Olympia ukaamua kutoa taarifa polisi juu ya vitisho hivyo ukizingatia kuwa ukumbi huo upo karibu kabisa na Bunge na maduka maarufu ya Galeries Lafayette ambayo ni kivutio kikubwa cha watalii pia si mbali na Ikulu ya nchi hiyo.

Siku ya shoo ilipofika, Combattants walifika eneo la kituo cha Metro Madelaine jirani kabisa na ukumbi wa Olympia wakishauriana kuweka mikakati kupambana na polisi, kuleta vurugu ili shoo isifanyike.

Wakati wakiwa katika harakati hizo, walikuwa wakiimba nyimbo mbalimbali huku wakisema “Ingeta, Ingeta” wakimaananisha kuwa hawaogopi mtu wala kitu chochote, wengine walikuwa wakiimba nyimbo kumtukana Rais Joseph Kabila, wakimtaka arudi kwao Rwanda.

Watanabe na vijana wake hawakulaza damu baada ya kuingia ukumbini mapema kutesti ‘mitambo’ ya vyombo vyao.

Nje ya ukumbi Askari wa Kuzuia Fujo ‘CRS’ kama ilivyo hapa Bongo (FFU), walishafika eneo hilo wakiwataka mashabiki kukaa umbali wa mita 500 kutoka kwenye ukumbi.

Ilpotimu milango ya saa moja usiku, mashabiki wachache walianza kumiminika nje ya ukumbi huo, askari wakawashauri waingie moja kwa moja ukumbini.

Waandaaji wa shoo hiyo baada ya kuona mashabiki ni wachache, waliamua kushusha bei ya kiingilio na wengine kuruhusiwa kuingia bure. Wakati shoo inakaribia kuanza, Combattants nje ya ukumbi wakaanza kufanya vurugu kubwa, wakichoma matairi ya magari.

Mashabiki wakaamua kupiga simu polisi pamoja na Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi hiyo, wakati haya yakitendeka askari wa kuzuia fujo walikuwa wakiwazuia Combattants kwa kuwarudisha mbali na eneo la ukumbi.

Ndani ya ukumbi tayari baadhi ya Combattants walishaingia wakijifanya kama ni mashabiki wa kawaida, hawa ndio walikuwa wakiwapa taarifa wenzao walio nje ya ukumbi kila kinachoendelea ukumbini humo.

Watanabe alipopanda tu jukwaani, huko nje vurugu zikaongezeka zaidi safari hii Combattants wakichoma moto gari la polisi.

Hali ilipokuwa tete polisi waliamua kusitisha shoo hiyo mara moja wakiingia ndani ya ukumbi na kuwatoa mashabiki, Watanabe pamoja na vijana wake.

Baada ya shoo hiyo kusitishwa, shangwe kubwa zikiambatana na nyimbo mbalimbali za kumshutumu Rais Kabila ziliendelea kurindima toka kwa Combattants, wakisherehekea ushindi kuzuia shoo hiyo isifanyike.

Kwa sasa hivi Watanabe na vijana wake wako nchini Marekani kuendelea na harakati zao za kutaka kupiga shoo huko, je, Combattants watazuia tena?

Wapenzi wasomaji wa kona hii, hayo ndiyo maswahibu yaliyomkuta Watanabe kiasi cha kusema kuwa hataisahau maishani mwake Julai 15, 2017. Tukutane wiki ijayo hapa hapa.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU