NILISHAKUFA

NILISHAKUFA

388
0
KUSHIRIKI

Ilipoishia

Baadaye tulitoka pale nyumbani na kwenda katika hoteli moja iliyokuwa mbele kidogo na mtaa wao. Tulikaa na kuongea mengi yanayohusu ukurasa wa mapenzi yetu. Hakika nilijiona ni mwenye thamani sana kuwa mwanaume wa Paulina, watu wengi walinitazama kwa wivu na wengine kwa mitazamo wanaoijua wao.

Tukiwa tunaendelea kupata vinywaji, nilimtazama Paulina na kumwambia.

 “Paulina tafadhali naomba tuanze kupanga maandalizi ya ndoa yetu sitaki kuchelewa kukuoa.”

Paulina alitazama kwa muda mrefu, akainamisha kichwa chini na kunijibu.

 SASA ENDELEA

Fredy mimi sina kipingamizi ni wewe tu kama unajiona uko tayari kwa kuoa sawa,” aliongea Paulina kauli iliyonishtua, sikuamini.

“Paulina ni kweli uyasemayo?” nilimuuliza kwa furaha.

“Ndio Fredy mimi ni mwanamnke, ninapaswa niwe nimeolewa. Bahati nzuri nakuona ni kijana mzuri mwenye kila sifa ya kuitwa mume wangu. Hivyo kama unajiona umejiandaa kuwa na mke ni vema ukanioa.”

Hakika ni kweli nilichanganyikiwa kwa furaha, sikuamini kama Paulina atakubali haraka kiasi kile. Nilijiona ni mwenye bahati. Niliushika mkono wake  na kuubusu mara nyingi.

“Asante Paulina asante mpenzi wangu,” niliongea kama mtu nisiyeelewa.

Siku hiyo tulizungumza mengi. Nilimfahamu Paulina vile nilivyoweza. Kiukweli alikuwa ni msichana mwenye tabia nzuri mcheshi na mwenye aibu sana. Tulipanga mengi sana endapo tutakuwa ndani ya ndoa.

“Asante Paulina najiona ni mwenye bahati sana kupendwa na wewe,” mara zote nilikuwa nikimwambia hivyo Paulina.

Baada ya maongezi hayo na kufurahi pale hotelini, nilimsindikiza hadi nyumbani kwao, watu waliendelea kunitazama mimi, wengine wasiamini kama nilikuwa pembeni ya mrembo Paulina. Siku hiyo ilikuwa ni siku nzuri sana hasa pale Paulina aliponibusu kwenye midomo yangu.

Alinisogelea taratibu na kunipiga busu  moyo wangu ulitikisika, mwili wangu wote ulisisimka.

“Kesho Fredy,” aliniaga kwa sauti ya maajabu.

Nilihema na kumeza mate nikimtazama kwa matamanio makubwa.

“Usiku mwema lala salama,” nilimjibu huku nikimtazama sana.

Baada ya kuagana, nilirudi nyumbani nikiwa na furaha zaidi ya ile ya juzi. Nilijiona ni mwenye bahati kubwa. Sikuamini kama nakwenda kuwa mume wa mrembo Paulina.  Hamu yangu kubwa pia ilikuwa ni kumtaarifu mama yangu mzazi aliyopo jimbo la Vensa kuwa nimempata mwenzangu wa maisha.

Usiku huo nilimwandikia mama yangu mzazi barua, nikimtaarifu kuwa nilikuwa nimempata msichana wa kumuoa. Pia nilimwomba yeye na dada yangu pamoja na mdogo wangu Zuni wajiandae kwa ajili ya kuja Wimbodone, kuhudhuria harusi yangu niliyopanga kuifanya baada ya miezi miwili.

Baada ya wiki mbili, nilipokea majibu kutoka kwa mama yangu. Barua ilinifikia kutoka Vensa. Kwanza Mama yangu alifurahishwa na hatua hiyo lakini aliniuliza maswali kadhaa kupitia barua hiyo. Swali lake la kwanza aliniuliza je, nimepata kumchunguza vya kutosha msichana ninayetaka kumuoa? Swali lake la pili lilikuwa ni je, nimejiandaa vya kutosha kuishi na mke? Swali lake la tatu aliniuliza rafiki zako wamekushauri nini kuhusu msichana unayetaka kumuoa?

Swali lake la mwisho lilikuwa ni je, msichana unayemuoa ni mcha Mungu na  ameridhika na kipato chako.

Maswali hayo yote sikuwa na majibu yake, kwa kuwa  sikuwa nimemchunguza Paulina vya kutosha. Hivyo nilimjibu mama yangu kwa kumridhisha tu nikimwambia kuwa nilikuwa nimempata msichana mwenye tabia nzuri.

Rafiki yangu Halid hakuamini kama kweli Paulina alikuwa amekubali nimuoe. Siku moja tukiwa tumepumzika klabu ya Freesize aliniambia.

“Fredy besti yangu, unajua naona kama masihara, Paulina amekubali umuoe?”

“Haa haha haaa! Nilikwambia Halid mimi ndiyo Fredy lazima nitamuoa Paulina na sasa nakwenda kutimiza ahadi ya maneno yangu,” nilimjibu kwa kicheko na kujisifu.

“Basi atakuwa amekupenda kweli. Lakini mbona kakubali mapema hivi? Nina mashaka,” aliongea Halid kwa mshangao wa mashaka.

“Mimi mwenyewe nashangaa, kasema kwa sasa ameamua kuolewa na anaona mimi ndio mwanaume sahihi kwake.”

“Unajua Fredy wewe una bahati. Mwanzoni mimi nilikuwa naogopa uwe na Paulina nikijua kuwa anaweza akakufilisi na kukuachia matatizo makubwa. Kwa sasa sina kipingamizi nakutakia maisha mema na mrembo wako Paulina,” aliongea Halid kwa furaha.

“Haa haha Haa! Asante besti naona sasa umenikubali,” nilimjibu kwa kicheko.

“Sema umepigiania sana penzi la Paulina licha ya vikwazo nilivyokuwa nakupa.”

“Usijali besti.”

Baada ya mwezi mmoja, niliwatumia nyumbani barua na nauli ya kuja mjini Wimbodone. Mimi nilihamia kwenye nyumba yangu mpya niliyojenga, nyumba iliyokuwa na vyumba viwili vya kulala na vingine viwili vya sebule. Ile nyumba niliyokuwa nimepanga niliwaandalia familia yangu, mama yangu, dada yangu na mdogo wangu Zuni.

Dada yangu na mdogo wangu walifurahi sana kuingia kwenye mji huo mkubwa. Mji uliokuwa makao makuu ya nchi ya Kaisavuna. Nilifurahi sana kuonana na familia yangu ambayo kwa mara ya mwisho tulikuwa tumeonana miaka mitatu iliyopita.

Niliwapenda ndugu zangu na kuwathamini sana nikiamini kuwa walikuwa ndio mboni ya jicho langu la maisha. Mdogo wangu nilimtafutia shule ya kimataifa ya kizungu. Ambayo ada yake ilikuwa ni shilingi 5,000 kwa mwaka.

Siku ya Jumapili nilimtambulisha Paulina kwa mama yangu. Paulina alipoingia tu ndani, mama yangu alibaki kushangaa, maana hakuamini kama mrembo Paulina ndiye msichana ninayetaka kumuoa. Uzuri na mwonekano wa Paulina ndivyo vilivyomshtua mama yangu. Alijiuliza maswali mengi kichwani kwake juu ya Paulina. Mama yangu alionyesha hali ya mashaka.

“Shkamoo mama,” alisalimia Paulina kwa kupiga magoti baada ya kuingia ndani.

“Marhaba mwanangu karibu sana. Mimi ndio mama yake na Fredy,” aliongea mama yangu akitabasamu.

“Asante mama na mimi ndio mke mtarajiwa wa mwanao,” aliongea Paulina kwa adabu zote.

“Nashukuru mwanangu. Naomba mpendane sana.

Nilimuacha mama yangu na Paulina, wakizungumza mengi mama yangu akimhoji Paulina maswali mengi kuhusu wazazi wake pia.

Mimi nilitoka pale nyumbani na kwenda nyumbani kwa Halid ambako kulikuwa  na kikao cha harusi yangu.

Niliporudi nyumbani, nilimkuta Paulina akila chakula pamoja na familia yangu. Nilifurahi sana kuuona muunganiko ule. Baada ya chakula cha jioni, Paulina aliaga kwa ajili ya kurudi nyumbani. Nilimsindikiza hadi nyumbani kwao. Aliniaga kwa busu lingine kali lililoniongezea kichaa kingine cha mapenzi. Kiwango cha mapenzi kilizidi kile cha jana. Nilimpenda sana msichana huyu, kiasi cha kujiona mgonjwa. Nikiamini ugonjwa huo sitoweza kupona.

Niliporudi nyumbani mama yangu alinikalisha chini.

“Fredy mwanangu huyu msichana mlikutana naye wapi?” aliniuliza mama yangu akiwa na mashaka.

Nilishtuka kidogo maana sikutegemea swali lake lije katika  hali ya mashaka.

“Nilikutana naye kazini kwetu, kwani vipi mama,” nilimjibu nikimuongopea.

“Mmmmh mwanangu pamoja na hayo, umemchunguza vya kutosha?”

“Nimemchunguza sana mama hadi nafikia hatua ya kumuoa ujue nimefanya sana kazi hiyo.”

“Fredy mwanangu mbona mimi nina mashaka juu yake?”

“Mashaka ya nini  tena mama?”

“Yule msichana haendani na wewe kabisa, siamini kama amekubali kuwa na wewe kwa lengo zuri.”

“Kivipi mama?”

“Macho yangu na moyo wangu vimepata mashaka juu yake. Licha ya kuonekana ni msichana mwenye tabia nzuri.”

“Ina maana mama mimi sistahili kupendwa na msichana mzuri?”

“Sina maana hiyo mwanangu, wewe pia ni kijana mzuri unaweza kupata mwanamke mzuri ila si kwa huyu. Sijui nikueleze vipi ili unielewe?”

“Mama usijali Paulina ananipenda na mimi ninampenda. Kuhusu yeye alivyo wala usitilie shaka,” niliongea mimi nikijaribu kuutetea upendo wangu.

“Ngoja nikwambie mwanangu, kwa kuwa tayari mko kwenye maandalizi ya mwisho ya ndoa yenu, nashindwa la kufanya ila kama ningewahi kabla hamjafikia hatua hii ningekushauri umuache huyu msichana,” aliongea mama yangu kwa ujasiri mkubwa.

“Heee kwanini mama?”

“Sioni kama atakuwa mke mwema kwako.”

“Mama usizungumze hayo. Hiyo ni mipango ya Mungu, ninaamini Paulina atakuwa mke mwema kwangu. Ninaomba baraka zako ili niweze kufunga naye ndoa.”

“Siwezi kupinga ndoa yako mwanagu,  ninakupa baraka zote na ninapenda uoe. Lakini pale ninapokuwa na mashaka sina budi kukueleza kile kilichopo ndani ya nafsi yangu, kwa kuwa mimi ni mlinzi wako na ninayekuongoza pia.”

Nini kitaendelea? Usikose kesho.  

 

 

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU