YANGA WAPATA BONGE LA ZALI

YANGA WAPATA BONGE LA ZALI

4434
0
KUSHIRIKI

*Kamusoko amgomea Tshishimbi kweupee Njombe

NA ONESMO KAPINGA, ALIYEKUWA NJOMBE

KAMA kuna anayedhani kuwa Yanga itakuwa na wakati mgumu kutetea ubingwa wao wa Ligi Kuu Tanzania Bara kutokana na kile kinachoaminika ukata unaowakabili, basi atakuwa anajidanganya.

Kwanini anajidanganya? Ni hivi, matajiri wa timu hiyo waliopo mikoa mbalimbali, wamekuja kivingine kuisaidia inaposafiri kwa ajili ya mechi za mikoani ili kuhakikisha inazoa pointi zote tatu hali itakayowaweka kwenye mazingira mazuri ya kubeba taji la Ligi Kuu Bara kwa msimu wa nne mfululizo.

Kampeni hiyo ya matajiri wa Yanga imeanzia mjini Njombe wakati timu yao ilipokuwa huko kuivaa Njombe Mji, ambapo ilipata mapokezi ya hali ya juu, ikiwamo kufikia kwenye hoteli ya kifahari ya Day To Day iliyopo eneo la Kibena.

Hoteli hiyo inayomilikiwa na mfanyabiashara, Leo Mgaya, ilitoa ofa kadhaa kwa timu hiyo kama sehemu ya kuwahamasisha na kuwapandisha mzuka wachezaji wa Wanajangwani hao, kuhakikisha wanawavaa wenyeji wao wakiwa na ari ya ushindi.

Mbali ya ofa iliyotolewa na hoteli hiyo kwa msafara mzima wa Yanga, pia jana wanachama na mashabiki wa klabu hiyo walipewa ofa ya kupata chakula cha jioni na wachezaji kama sehemu ya kuwahamasisha vijana wao kupambana kwa nguvu na uwezo wao wote kupata ushindi katika mechi zao zinazofuata kama ilivyokuwa mjini hapo walipowachapa wenyeji wao bao 1-0.

Mapokezi na ofa waliyoipata Yanga Njombe, vinatarajiwa kuendelea kwenye mechi zao nyingine za mikoani, ikiwamo inayofuata wikiendi hii dhidi ya Majimaji ya Songea, mkoani Ruvuma.

Tayari kuna taarifa kutoka Songea kuwa matajiri wa huko wanapigana vikumbo ili kuipokea Yanga itakapotua huko leo jioni, kama sehemu ya kuhakikisha wachezaji wao wanahifadhiwa sehemu tulivu na yenye usalama itakayowawezesha kuisambaratisha Majimaji.

Ikiwa Njombe, Yanga ilifanya maandalizi mazuri kuelekea mchezo wao na wenyeji wao, yaliyowawezesha kupata ushindi, wakifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Chai.

Hata baada ya mchezo wao huo wa Jumapili, Kocha Mkuu wa Yanga, George Lwandamina, alivutiwa na mandhari ya hoteli hiyo na kupendekeza kuendelea kubaki  katika hoteli hiyo kujiwinda na  Majimaji wanaotarajiwa kucheza Jumamosi kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea.

Lwandamina aliridhishwa na mandhari ya hoteli hiyo waliyokuwa wamefikia wachezaji na benchi la ufundi la timu hiyo na kuweza kufanya maandalizi yao wakiwa sehemu tulivu.

Matajiri wa Yanga wanaamini kuwa kwa kuisaidia timu yao kushinda mechi za mikoani, ni njia pekee itakayowarahisishia kampeni yao ya kutetea ubingwa wa Bara.

Mara nyingi mechi za mikoani zimekuwa zikiisumbua Yanga, huku ikiwa rahisi kwao kuvuna pointi zote tatu wanapocheza kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Hata hivyo, msimu huu wameshindwa kupata pointi zote katika mchezo wao wa kwanza wa ligi waliocheza Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam dhidi ya Lipuli ya Iringa, lakini wakafanya kweli Jumapili iliyopita dhidi ya Njombe Mji.

Akizungumzia kuhusiana na hoteli hiyo ya Day To Day, Mgaya amezitaka timu nyingine zitakazokwenda kucheza soka mkoani humo, kufikia hapo.

Alisema anaamini kwamba, wachezaji wakiweka kambi katika hoteli hiyo, wataweza kujiandaa vizuri, kwani ni sehemu tulivu.

Katika hatua nyingine, Mzimbabwe Thaban Kamusoko, amegoma kufunikwa na kiungo mwenzake wa Yanga, Pappy Kabamba Tshishimbi mjini Njombe kama ilivyokuwa ikitarajiwa na mashabiki wengi wa soka wa huko.

Kabla ya Yanga kuivaa Njombe Mji Jumapili iliyopita, mashabiki wengi walimtaja Tshishimbi kama mchezaji atakayetamba zaidi katika mchezo huo kutokana na kile walichokuwa wakiamini uwezo mkubwa alionao.

Tshishimbi aliyesajiliwa na Yanga katika dirisha kubwa la usajili la Ligi Kuu Tanzania Bara akitokea Mbabane Swallows ya Swaziland, alipata umaarufu mkubwa baada ya kuisumbua Simba katika mechi ya Ngao ya Jamii iliyochezwa Agosti 23 mwaka huu, kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Sababu hiyo ndiyo iliyowafanya mashabiki wa Njombe Mji kumhofia zaidi Tshishimbi kuliko wachezaji wengine, wakiwamo Ibrahim Ajib, Kamusoko na Donald Ngoma ambao walikuwa wamefunikwa na kiungo huyo tangu msimu huu ulipoanza.

Lakini baada ya mchezo dhidi ya timu yao, mashabiki wa Mjombe Mji walimwona Tshishimbi ni mchezaji wa kawaida baada ya kubanwa na kushindwa kuonyesha kiwango cha juu kama alivyofanya dhidi ya Simba.

Katika mechi hiyo, Kamusoko ndiye aliyeonekana kukubalika kutokana na uwezo alioonyesha na kuisaidia timu yake kushinda bao 1-0.

Bao hilo lilipatikana kabla ya Kamusoko kutolewa na pengo lake kuonekana wazi, kwani Njombe Mji walifanya mashambulizi mengi, ingawa hayakubadili matokeo ya mechi hiyo.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU