WACHEKA NA NYAVU WALIOTIKISA TANZANIA   

WACHEKA NA NYAVU WALIOTIKISA TANZANIA   

783
0
KUSHIRIKI

NA HENRY PAUL

UNAPOZUNGUMZIA mafanikio ya soka la Tanzania, lazima utazungumzia kipindi cha mwaka 1979 mwishoni wakati Tanzania inafuzu kwa mara ya kwanza kushiriki michuano ya fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika na fainali hizo kufanyika mjini Lagos, Nigeria mwaka 1980.

Pamoja na kwamba kuanzia miaka hiyo kiwango cha soka letu kimekuwa kinaonekana kama homa ya vipindi, lakini hata hivyo nchi yetu ilibahatika kuwa na wapachikaji mabao mahiri ambao wanakumbukwa, licha ya kiwango kusuasua.

1.PETER TINO

Unapozungumzia wapachikaji mabao mahiri kuwahi kutokea nchini, kamwe huwezi kuacha kulitaja jina la mshambuliaji Peter Tino, kwani alikuwa na kila kitu ambacho mshambuliaji mahiri anatakiwa kuwa nacho ambacho ni mashuti makali, chenga za maudhi, uwezo mkubwa wa kupachika mabao na nguvu pale inapohitajika.

Tino anakumbukwa na wapenzi wa soka nchini kuwa alipokuwa na timu ya taifa, Taifa Stars aliisawazishia timu hiyo dhidi ya timu ya Taifa ya Zambia, katika mchezo wa awali wa kufuzu fainali ya Mataifa Afrika, mechi iliyochezwa katika mji wa Ndola, Zambia mwaka 1979.

Baada ya Tino kusawazisha bao hilo, Taifa Stars ilipata tiketi ya kushiriki fainali hizo zilizofanyika mjini Lagos, Nigeria mwaka 1980. Hivi sasa ni takriban miaka 37 imepita pamoja na kuwa na washambuliaji wengine nyota, lakini Tanzania imejitahidi kushiriki tena fainali hizo bila ya mafanikio.

Tino pamoja na kuichezea timu ya Taifa Stars kwa mafanikio kwa vipindi kadhaa, pia nyota huyo ameichezea klabu ya Yanga, Pan African, African Sports ya Tanga, Kiltex ya Arusha na majimaji ya Songea.

2.ZAMOYONI MOGELA ‘GOLDEN BOY’

Mogela kama ilivyokuwa Peter Tino, naye alikuwa na uwezo mkubwa wa kupachika mabao akiwa na klabu yake ya Simba hali iliyowafanya wapenzi na mshabiki wa timu hiyo kumbatiza jina la ‘Golden Boy’.

Mshambuliaji huyo anakumbukwa na wapenzi wa soka nchini yeye na kiungo mkabaji Mtemi Ramadhani walivunja dhana ya timu za Tanzania kufungwa na timu za Misri, kwa sababu waliifungia Simba mabao mawili dhidi ya Nationali Al-Ahly ya Misri mwaka 1985.

Pia Mogela mwaka 1991 akiwa na klabu ya Simba aliiwezesha kutwaa taji la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati baada ya kuifugia mabao mawili kati ya 3-0 yaliyopatikana siku hiyo katika fainali dhidi ya Club Sports Villa ya Uganda,fainali iliyochezwa katika Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam.

Katika michuano hiyo Mogela aliibuka mfungaji bora baada ya kufunga mabao sita. Nyota huyo pamoja na kuichezea klabu ya Simba kwa mafanikio, pia amezichezea Jogoo, Reli, Tumbaku zote za Morogoro,  Yanga, timu ya Taifa ya vijna na timu ya taifa, Taifa Stars.

3.MAKUMBI JUMA ‘HOMA YA JIJI’

Makumbi alikuwa ni mmoja wa wapachika mabao mahiri wa klabu ya Yanga na timu ya Taifa Stars kuwahi kutokea katika historia ya soka la Tanzania.

Kutokana na uwezo mkubwa aliokuwa nao wa kupachika mabao wapenzi wa klabu ya Simba walimbatiza jina la ‘Homa ya Jiji’ kwa sababu ya kuwapa presha sana wakati timu hizo zilipokuwa zikikutana.

Mshambuliaji huyu alikuwa ni nadra sana kutoka uwanjani bila ya kupachika na hivyo kutokana na hofu kubwa waliokuwa nayo wapenzi wa Simba wakati timu hizo zilipokuwa zinataka kukutana walikuwa wanaomba nyota huyo asichezeshwe au awe mgonjwa kusudi asiweze kucheza, kwani ni lazima tu alete madhara ya kuwafunga.

Makumbi pamoja na kuichezea klabu ya Yanga kwa mafanikio makubwa pia amezichezea klabu kadhaa zikiwemo Pamba, RTC za kigoma, timu za Mikoa ya Kigoma, timu ya mkoa wa Dar es Salaam maarufu Mzizma United na timu ya taifa, Taifa Stars.

4.ABDALLAH ‘KING’ KIBADENI

Kibadeni ambaye alikuwa anacheza namba 10 naye wakati anacheza soka ya ushindani alikuwa ni miongoni mwa wapachika mabao mahiri waliotamba hapa nchini katika miaka ya 1970 hadi 1980.

Mbali na kuzifungia timu zote alizokuwa anazichezea, lakini moja ya rekodi yake ambayo inakumbukwa hadi leo hii ni ile ilipoipachikia mabao matatu timu yake ya Simba katika mchezo dhidi ya Yanga ambapo timu yake hiyo ya Simba iliibuka na ushindi mnono wa mabao 6-0.

Kibadeni alifunga mabao hayo matatu katika dakika ya 10, 43 na 89 ambapo mengine mawili yalifungwa na Jumanne Masmenti (marehemu) katika dakika za 60 , 73 na moja aliyekuwa beki wa Yanga Seleiman Said Sanga alijifunga katika dakika ya 20.

Kibadeni pamoja na kuichezea klabu ya Simba kwa mafanikio, pia amezichezea timu kadhaa zikiwemo Young Boys, Kahe, Hanoi za Dar es Salaam, Majimaji ya Songea timu za Mikoa ya Ruvuma inayojulikana Ruvuma Worries, timu ya mkoa wa Dar es Salaam maarufu Mzizima United na timu ya taifa, Taifa Stars.

5.SAID MWAMBA ‘KIZOTA’

Unapozungumzia wapachikaji mabao mahiri waliowahi kutoka katika soka la Tanzania huwezi kuacha kulitaja jina la Said Mwamba au maarufu ‘Kizota’ ambaye hivi sasa ni marehemu.

‘Kizota’ kutokana na umahiri wa kupachika mabao mwaka 1993 aliibuka mfungaji bora katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati yaliyofanyika Kampala, Uganda ambapo Yanga ilitwaa taji hilo.

Katika michuano hiyo alifunga mabao sita. Katika mchezo wa fainali Yanga ilicheza na Club Sports Villa na kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 ambapo bao la kwanza lilifungwa na yeye ‘Kizota’ katika dakika ya sita na pili lilifungwa na Edibily Lunyamila dakika mbili kabla ya mapumziko.

Pia Machi 27, 1993 Kizota aliifungia mabao mawili timu yake ya Yanga ilipoifunga Simba mabao 2-1 katika mchezo wa kwanza wa Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara (sasa Ligi Kuu). Mabao hayo aliyafunga katika dakika ya 47 na 57.

Nyota huyo hivi sasa hatunaye, kwani alikwisha fariki dunia Februari 11, 2007 baada ya kugongwa na gari eneo la Vetenary akiwa anatoka kuangalia mchezo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho la Soka Afrika raundi ya awali kati ya wenyeji Simba dhidi ya Textile de Pungue ya Msumbiji.

Said Mwamba ‘Kizota’ pamoja na kuichezea Yanga kwa mafanikio, pia ameichezea Posta ya Tabora, Kurugenzi ya Dodoma, timu ya mkoa Dar es Salaam maarufu Mzizima United, Al-Nasor ya Oman na timu ya taifa, Taifa Stars.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU