KILA LA HERI TANZANITE

KILA LA HERI TANZANITE

227
0
KUSHIRIKI

TIMU ya Taifa ya soka ya wanawake iliyo chini ya miaka 20 ‘Tanzanite’, inatarajia kushuka uwanjani leo kucheza na Nigeria katika mchezo wa kuwania kufuzu Kombe la Dunia, utakaochezwa nchini humo.

Mchezo huo tunauona ni muhimu kwa Tanzanite kushinda ili kujiweka katika mazingira bora kusonga mbele wanaporudiana hapa nchini.

Kutokana na sababu hiyo, ni matarajio yetu kwamba kocha wa Tanzanite, Sebastian Nkoma, atakuwa amekiandaa kikosi cha ushindi baada ya kufanya mazoezi kwa muda mrefu.

BINGWA tunaamini kwamba, Nigeria si timu kubwa inayoweza kuitisha Tanzanite na kushindwa kuibuka na ushindi wakiwa katika uwanja wa ugenini.

Tunasema si mara ya kwanza kwa Tanzanite kucheza na Nigeria,  tunakumbuka waliwahi kucheza, hivyo watakuwa wanajua udhaifu wao.

Hata hivyo, BINGWA tunaamini kwamba benchi la ufundi chini ya kocha Nkoma litakuwa limewajenga  kisaikolojia wachezaji wake ili waweze kuibuka na ushindi.

Tunaamini kwamba, ushindi kwa Tanzanite dhidi ya Nigeria utaweza kuiweka katika nafasi nzuri ya kufuzu fainali hizo.

Ushindi kwa Tanzanite una umuhimu mkubwa kwetu Watanzania, ikizingatia Tanzania imeshuka nafasi tano katika viwango vilivyotolewa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa).

Katika orodha ya sasa Tanzania inashika nafasi ya 125 kutoka 120 iliyokuwa inashika kwenye orodha ya mwezi uliopita.

Hivyo basi, Tanzanite wanatakiwa kushinda mchezo wa leo ili kuamsha matumaini mapya kwa soka la Tanzania, baada ya timu ya Taifa Stars kushindwa kufanya vizuri katika michuano ya kimataifa, inayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) na Fifa.

Kwa mantiki hiyo, tunawasihi wachezaji wa Tanzanite kucheza kwa kujituma ndani ya dakika zote 90 ili kuweza kupata matokeo mazuri.

Ikumbukwe kwamba, Nigeria watakuwa katika ardhi ya nyumbani wakipata sapoti kutoka kwa mashabiki wa nchi yao, hivyo Tanzanite wanatakiwa kukabiliana na changamoto zote zitakazojitokeza dhidi yao.

Tunasema Tanzanite tupeni raha Watanzania kwa kuhakikisha ndani ya dakika 90 kunapatikana ushindi na baadaye katika mchezo wa marudiano utakaochezwa nyumbani.

BINGWA tunaitakia kila la kheri Tanzanite tukiamini wachezaji hawatawaangusha na tupo nyuma yao.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU