MARCELO ATACHEZA WINGA ZAIDI MSIMU HUU?

MARCELO ATACHEZA WINGA ZAIDI MSIMU HUU?

363
0
KUSHIRIKI

KWENYE mechi ya tatu ya Ligi Kuu msimu huu dhidi ya Levante, kocha Zinedine Zidane, aliwapanga mabeki wawili wa kushoto, Marcelo na Theo Hernandez. Ndani ya uwanja, Marcelo alionekana kama winga zaidi huku Theo kama beki wa kushoto.

Kiufundi Zidane aliijua kasi ya Levante, ambayo imepanda ligi  msimu huu kwa hiyo alitaka kudhibiti mashambulizi yao kwa kuimarisha beki ya kushoto.

Carlo Ancelotti amewahi kuwapanga Marcelo na Fabio Coentrao, ambao wote ni mabeki wa kushoto. Uzuri ni kwamba, Coentrao akipangwa winga wa kushoto huwa hashangai.

Ndani ya mechi hiyo kulikuwa na mabadiliko kati ya wawili hao. Kama Theo alipanda kushambulia basi Marcelo alirudi eneo la beki wa kushoto kulinda lango. Kama Marcelo alipanda kushambulia basi Theo alikuwa anarudi eneo la beki wa kushoto kulinda.

Marcelo aliposhambulia aliingia ndani ya mipira mingi zaidi na kukutana na viungo waliokuwa wakitafuta njia ya kuivunja ngome ya Levante.

Ingawa kulikuwa na makosa madogo madogo kwani kubadilishana namna ndani ya uwanja iliwafanya wakosee mara kadhaa. Lakini hilo tunaweza kusema ni suala la muda mfupi, kwa kuwa Theo ameingia kikosini msimu huu. Bado hajaelewana na wachezaji wengine.

Kuwapanga mabeki hao ina maana kocha ameamua kulinda lango lake, wakati huo huo anatamani kuona kashikashi katika lango la adui.

Ndiyo kusema Zidane ameamua kujaribu mbinu hiyo kutokana na Marcelo kutabiri kila anapocheza maana anaweza kuwa eneo la kiungo, mshambuliaji wa kati au winga, ingawaje yeye ni beki wa kushoto. Kila kocha angetamani hali hiyo, lakini inahitaji uangalifu mkubwa sana.

Kwa mtazamo wangu uamuzi wa kuwapanga Theo na Marcelo katika mechi moja ni kutuambia kuwa kuna mbinu za ziada zinakuja msimu huu. Mbinu hizo zinapitia kwa Marcelo.

Kwamba endapo tutazidiwa kabisa na kupaswa kujilinda tutawahitaji Marcelo na Theo. Iwapo timu itahitaji kuongeza kashikashi na kupata ushindi mnono watapangwa Marcelo na Theo. Mbinu hii inaleta mjadala zaidi kwani itampunguzia mechi za kucheza Lucas Vazquez au Borja Mayoral.

Kwanini Marcelo anawatamanisha makocha!

Aliondoka kwao Brazil akiwa winga wa kushoto. Alisajiliwa kutoka klabu ya Fluminense. Lakini alikuwa na uwezo wa kucheza beki wa kushoto. Benchi la ufundi la Madrid lilimwona kama mchezaji anayeweza kubadilishwa nafasi kutokana na kipaji kikubwa alichonacho.

Marcelo alikuja kurithi mikoba ya Mbrazil mwenzake, Roberto Carlos, aliyesajiliwa na Madrid akitokea Inter Milan. Marcelo anaichezea timu ya taifa ya Brazil kama beki wa kushoto. Ameshiriki mashindano mengi duniani akiwa beki wa kushoto. Sifa nyingine aliyonayo ni udambwidambwi. Huo ni upande mmoja wa Marcelo.

Upande wa pili wa Marcelo ni huu wa mabadiliko ya ndani kwa ndani. Anaweza kucheza kwenye eneo la kiungo mkabaji (nambari 6). Anaweza kucheza kwenye eneo la kiungo mchezeshaji (nambari 8). Anaweza kucheza kwenye eneo la mshambuliaji wa pili (namba 10). Anaweza kucheza kwenye eneo la winga wa kushoto au kulia.

Na zaidi hataki kuwekwa kwenye ‘dropping ball’, pale timu inaposhambulia na kuacha beki mmoja nyuma ili kuokoa hatari zozote za kushtukiza.

Mambo yote mazuri ni kwamba, kipindi ambacho Ronaldo akicheza upande wa kushoto kulikuwa na kombinenga nzuri sana kati yake na Marcelo. Ronaldo alikuwa akirahisishiwa kazi nyingi na Marcelo katika upande huo. Linki yao ni mwiba kwa timu pinzani.

Kama timu inashambulia kupitia kushoto basi mapishi yote yanakuwa yamepikwa na Marcelo. Kuna wakati anakuwa eneo la beki wa kati na kiungo mkabaji kusaidia kulinda lango. Kuna wakati anaweza kuchukua mpira eneo la kiungo mkabaji kisha akakokota katikati ya dimba na kuwalamba chenga msitu wa wachezaji wa timu pinzani.

Kwa mfano, katika mechi ya marudiano ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu uliopita dhidi ya Bayern Munich, Marcelo alifanya kitu kama hiki. Alichukua mpira nusu ya eneo la Madrid. Akakokota kuelekea lango la Bayern akikatisha katikati ya msitu wa viungo na mabeki wao.

Wote walishindwa kumzuia. Si Matt Hummeles, wala Thiago Alcantara au Alonso. Halafu akatengeneza pande safi kwa Ronaldo aliyepachika bao la nne.

Mechi nyingine ni ile ya dhidi ya Valencia msimu uliopita pale Santiago Bernabeu. Alikutana na krosi ndefu iliyopigwa na Alvaro Morata kutoka upande wa kulia. Akatuliza mpira na kuanza kukokota kulisogelea lango la Valencia.

Akili za mabeki wa Valencia walidhani angetengeneza pasi ya mwisho kwa mfungaji. Haikuwa hivyo, Marcelo akiwa nje ya 18, akikimbia kwa kasi kuingia kwenye boksi kisha akaachia mkwaju mkali uliokwenda moja kwa moja wavuni.

Lilikuwa tukio la haraka mno. Ni tukio ambalo angeweza kutoa pasi kwa mchezaji mwingine katika eneo hilo, badala yake akapiga shuti kali kwa mguu wa kulia.

Matukio ya Marcelo kuliacha eneo lake na kuwa maeneo mengine yametokea mara nyingi. Kuna wakati inasemwa kuwa Marcelo ni fundi wa kushambulia kuliko kukaba. Lakini wenyewe tunajua ubora wa mchezaji huyu ni pale anapokuwa anaongoza mashambulizi au kuifanya timu icheze kwa utuvuli wa hali ya juu.

Swali linaturudia palepale Marcelo anafaa kucheza winga? Kwanza ana sifa ya mzuka wa mpira. Pili anajua kuliandama lango la adui. Tatu, amekuwa akiwarudisha nyuma mawinga na mabeki wa timu pinzani ili kupunguza shinikizo dhidi yake. Jambo la nne hababaiki na presha ya mchezo.

Msimu uliopita alipika mabao 9 katika mechi 28 alizocheza. Hayo si haba kwa beki wa kushoto ambaye kazi yake ni kulinda lango. Kwa hiyo utaona huenda angekuwa anacheza winga wa kulia au kushoto angetengeneza mabao mengi mno.

Zamu yako msomaji!

Wiki ijayo nitachapisha maoni yenu, andika ujumbe mfupi kujibu maswali wawili tu; una mtazamo gani kinda wetu, Borja Mayoral, unadhani ataziba pengo la Alvaro Morata? Je, ana chochote mguuni cha kukutisha?

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU