‘CANNAVARO’ AKOMAA NA MANJI

‘CANNAVARO’ AKOMAA NA MANJI

2162
0
KUSHIRIKI

NA HUSSEIN OMAR

NAHODHA wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, amesema anatamani kuona Mwenyekiti wao wa zamani, Yussuf Manji, anarejea kuiongoza timu hiyo yenye maskani yake mitaa ya Twiga na Jangwani, jijini Dar es Salaam ili kuokoa jahazi linaloelekea kuzama.

Manji alitangaza kujiuzulu kuiongoza Yanga na nafasi yake kukaimiwa na Makamu Mwenyekiti wake, Clement Sanga, kutokana na kile kilichodaiwa kuchoshwa na mambo yanavyokwenda ndani ya klabu hiyo.

Akizungumza na BINGWA baada ya mazoezi ya jana, jijini, Cannavaro alisema sapoti ya Manji bado inahitajika baada ya klabu hiyo kuyumba kiuchumi na kusababisha wachezaji kumkumbuka kiongozi wao huyo wa zamani.

“Nipo tayari kumshawishi mwenyekiti arejee, kimsingi bado tunahitaji sapoti yake kwa kuwa alifanya maamuzi ya kung’atuka Yanga mapema,” alisema Cannavaro.

Alisema yeye kama nahodha wa timu hiyo, atahakikisha anapambana kivyake kumshawishi mfanyabiashara huyo kurejea tena kundini kuendelea kuiongoza Yanga.

“Wenzetu sasa hivi wanapanda ndege, wana tajiri wao mkubwa, sisi tunapanda basi, hii ni shida sana kwa kweli, tunajisikia vibaya, tunapenda arejee tena kundini,” aliongeza Cannavaro.

Cannavaro alisisitiza kuwa ingawa hawezi kuzungumzia kwa undani masuala ya uongozi, lakini kwa utashi wake amepanga kukutana faragha na kiongozi wao huyo wa zamani kuzungumza naye.

“Najua ile siku tuliyokwenda mahakamani, Mwenyekiti aliniita tukakuzungumza mengi, lakini kubwa ni kumtaka arejeshe nguvu zake klabuni na akaniahidi kuwa matatizo yake yatakapoisha tutazungumza tena,” alisema Cannavaro.

Katika hatua nyingine, Cannavaro amewataka wachezaji wenzake kuweka pembeni matatizo yao ya kutolipwa mishahara na kuelekeza nguvu zao katika michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara inayofuata.

“Nimeongea na vijana, tumekubaliana kwanza tufanye kazi, kisha maslahi yetu tutadai tu, kimsingi hakuna mgomo kila kitu kipo sawa, tunawaahidi mashabiki wetu kuwapa raha zaidi katika michezo inayofuata,” alisema Cannavaro.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU