RONALDO MASHINE ASIKWAMBIE MTU

RONALDO MASHINE ASIKWAMBIE MTU

619
0
KUSHIRIKI

MADRID, Hispania

NYOTA Cristiano Ronaldo, jana alirejea uwanjani akitoka kuitumikia adhabu ya kuzikosa mechi tano za La Liga baada ya tukio lake la kumsukuma mwamuzi, Ricardo de Burgos Bengoetxea.

Staa huyo alitolewa nje kwa kadi nyekundu katika mchezo wa Spanish Super Cup kati ya Real Madrid na Barcelona uliochezwa Agosti 13, mwaka huu.

Hata hivyo, kwa kipindi chote Ronaldo alichokaa nje, kikosi cha kocha Zinedine Zidane kimeonekana kuyumba kwa kiasi kikubwa, hasa katika idara ya upachikaji mabao.

Kabla ya matokeo ya jana dhidi ya Real Betis, baada ya kuifunga Deportivo La Coruna mabao 3-0 katika mchezo wa ufunguzi, Madrid walijikuta wakiambulia sare dhidi ya Valencia na Levante, ingawa walipata matokeo dhidi ya Real Sociedad.

Katika michezo hiyo miwili ya sare, Madrid walitengeneza nafasi nyingi za mabao, ambazo kama Ronaldo angekuwepo uwanjani, basi zingekuwa faida kubwa kwa timu hiyo.

Kwa mujibu wa mtandao wa takwimu wa Opta, Karim Benzema, peke yake alishindwa kuzitumia nafasi sita za wazi katika mchezo waliovaana na Valencia.

Dhidi ya Levante, nyota Gareth Bale, alikosa nafasi tatu za kuifungia Madrid, jambo ambalo si rahisi kutokea kwa Ronaldo. Bale amekuwa kwenye wakati mgumu kwa kipindi chote ambacho Ronaldo amekuwa nje, ambapo amejikuta akizomewa na mashabiki wa Madrid kutokana na kiwango chake kibovu.

Mabao mawili aliyoyafunga Ronaldo katika ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya APOEL katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya ni ushahidi kuwa Madrid wamekuwa kwenye wakati mgumu pindi staa huyo anapokuwa nje ya uwanja.

“Real wana aina nyingi za uchezaji. Wanaweza kucheza ‘counter attack’ au wakamiliki mpira, lakini wanahitaji mpachikaji mabao pale mbele,” alisema mchambuzi mmoja wa Sky Sport.

“Bado (Madrid) iko imara bila yeye.  Bado watakuwa kwenye kinyang’anyiro cha kuwania ubingwa hata akikosekana. Lakini wanapokuwa naye wanakuwa na uhakika wa zaidi ya mabao 40 (katika michuano mbalimbali).”

Ronaldo, akiwa na timu yake ya Taifa ya Ureno, katika mechi za kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia za mwakani zitakazofanyika nchini Urusi, alikuwa kwenye kiwango bora na kukiwezesha kikosi chake kuibuka na ushindi wa mabao 5-1 dhidi ya Visiwa Faroe.

Wakati Madrid wakihaha kwenye idara ya mabao, nahodha huyo aliifungia Ureno ‘hat trick’.

Akizungumzia kurejea kwa Ronaldo juzi, Zidane alieleza kufurahishwa kwake na kitendo hicho.

“Hatutazungumzia kuhusu adhabu, tumefurahi kuona amerudi na nafikiri itakuwa ni mwisho kutokuwa naye uwanjani,” alisema Zidane.

“Namwona Cristiano akiwa na furaha, kwa sababu anapenda kucheza na kuwa na wenzake kikosini.”

Wakati mashabiki wa Madrid wakisherehekea ujio wa Ronaldo dimbani, habari nyingine njema kwao ni ile ya kocha Zidane kuongeza mkataba mpya wa kuendelea kufanya kazi Santiago Bernabeu.

Taarifa zimesema Mfaransa huyo mwenye umri wa miaka 45, ameongeza miaka miwili na mabingwa hao wa Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu uliopita.

Zidane alianza kuliongoza benchi la ufundi la Madrid mwanzoni mwa mwaka jana, akichukua nafasi ya Mhispania, Rafa Benitez.

Inasemekana mshahara mpya wa Zidane utafikia dola milioni 9.5, mbali na bonasi na dili zake binafsi za matangazo.

Kabla ya mchezo wa jana, Zidane alikuwa amekiongoza kikosi hicho katika mechi 95, akiwa ameshinda michezo 71, sare 17 na kupoteza saba pekee, huku kikiwa kimefunga mabao 264 na kuruhusu nyavu zao kutikiswa mara 97.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU