WEWE NI NANI KATIKA MAISHA YA MWENZAKO

WEWE NI NANI KATIKA MAISHA YA MWENZAKO

390
0
KUSHIRIKI

NI bahati sana kuwa na mtu uliye naye. Mtu anayekupenda, kukujali na kukuthamini kwa kiwango kinachosisimua. Hakika ni bahati sana, wengine wanatamani kupata mtu wa aina yako mwenye kuwajali, kuwasikiliza na kuwafanya kuwa na amani na furaha ila wapi.

Wengi wapo katika mahusiano yanayowapa majuto na kuwatoa machozi. Kila siku sura zao zimetawaliwa na majonzi pamoja na simanzi ya kutisha. Kwanini usijione wa bahati kuwa na huyo uliye naye? Una sababu ya kujidai, kuringa na kujivunia.

Kuwa na mtu mwenye kukujali kiuhalisia na kukuthamini si jambo dogo. Ambaye kila anapoona ‘missed call’ yako hawezi kulala mpaka akupigie. Ambaye kila siku anaona thamani na fahari sana kuongea na wewe. Wewe ni mtu mwenye bahati sana. Hasa ukizingatia unaishi katika ulimwengu wa utandawazi ambao wachache wamegeuza mapenzi kuwa kama mradi. Wapo radhi kukuambia wanakupenda huku wanalia kwa kuwa wanajua baadaye ni lazima utawahonga pesa.

Katika hali hii haiepukiki kusema wewe ni mtu mwenye bahati katika mahusiano yako. Hongera sana. Ila kweli unahisi unastahili hii hongera? Kuna baadhi hawastahili.

Hawa ni wale wanaoona fahari kuwa na wapenzi wenye kazi fulani na mionekano fulani huku suala la mapenzi likiwa linasua sua. Yaani kwa urembo wa mpenzi wake anaona fahari sana na kujivunia kuwa naye huku matendo ya mhusika yakiwa yamezungukwa na usiri na kizungumkuti cha kutisha. Huyu hafai kuhisi bahati ya kuwa na aliye naye. Huyu hafai kuona kama mhusika ni zawadi kubwa kuimiliki.

Mapenzi hayaamuliwi na mvuto wala kazi ya mtu. Ni uvivu kudhani kuwa eti kuwa na msichana mrembo ni bahati katika maisha yako. Ni ujuha kuamini kuwa kwa kuwa ana kazi nzuri basi ni zawadi kubwa sana kummiliki hata kama haoneshi kukupenda.

Suala la msingi katika amani ya mapenzi si sura wala kazi, ni upendo. Hata kama ni mzuri kiasi gani ikiwa haoneshi upendo na kukujali kwa namna iliyo bora. Hakufai. Hakufai kwa maisha yako wala kwa furaha yako. Furaha ya mahusiano haipatikani katika kazi ya mtu ama kiuno chake. Furaha kamili huja katika jumla ya matendo yake juu yako.

Namna anavyokujali na kukusikiliza. Namna anavyopenda kukuona ukiwa na furaha na amani. Acha kubabaika kwa sababu ya pesa na urembo wake.

Na watu wenye kusumbuliwa na hali hii ya kuamini kuwa na warembo au watanashati ni bahati wanasumbuliwa na tatizo la kutojiamini. Kwa fikra zao dhaifu zilizoelemewa na hali ya unyonge wanaamini hivi bila kujali maana halisi ya kuwa katika mahusiano yao. Na katika hali kama hii ndiyo maana wengi tunaona wanasumbuliwa na kunyanyasika katika mahusiano yao. Ila kuachana wanaogopa.

Mbali na mambo mengine ila wanaamini  uzuri au kazi za wahusika ni vitu muhimu zaidi kwao. Kuna raha gani kuwa na mrembo anayekupa mateso na manyanyaso ya nafsi? Kuna faida gani kuwa na bosi anayekupa masimango na kukuletea vimada? Kuwa katika hali hii ni kujitukanisha. Kujidhalilisha na kutojitambua hasa.

Jali upendo na umuhimu wake katika furaha na amani ya maisha yako. Ikiwa hana vitu hivi maana yake kuwa hana hisia na wewe. Hivyo kumganda ni sawa na kulazimisha mapenzi. Jiulize, kwanini sasa ulazimishe mapenzi? Ni nani uliyewahi kumuona akilazimisha mapenzi na bado akawa na furaha? Kulazimisha mapenzi ni janga. Ni mtihani, ni kamba itakayonyonga furaha yako.

Unanyanyaswa makusudi ila hutaki kumuepuka unadhani anakufikiriaje? Anakufikiria unambabaikia kwa sababu ya sura au kazi yake. Na katika hali kama hiyo hatoacha kukunyanyasa kwa sababu anajua unachojali ni namna anavyoonekana au kazi yake, hivyo wa kuwa anavyo basi huwezi kufanya lolote kwake. Wengi wanateswa kwa sababu hii. Wengi amani ya mahusiano yao haipo sawa kwa sababu ya kutojiamini na kuruhusu kudharaulika. Kama nawe ni mmoja wapo shtuka kisha kaa kando.

Ni mara ngapi umemwambia kuhusu tabia yake mbovu? Ni kwa muda gani umemwambia aache maovu anayofanya ila bado anaendelea nayo? Kuwa na unayempenda ni suala zuri ila kuwa na mnayependana ni suala zuri zaidi. Narudia. Furaha ya kweli ya mahusiano haiko kwa mtu unayempenda ila iko kwa mtu unayependana naye.

Bila kujali anavyoonekana au aina ya kazi anayofanya, muepuke anayekuliza kwa makusudi. Ambaye haoni thamani wala maana ya chozi lako. Ikiwa anaona kuna kitu unababaikia katika maisha yake atafanya kila anachojisikia kwa kuwa anajua wewe ni mbabaikaji tu. Na siku zote mbabaikaji ni mtu mjinga asiyejiamini.

Thamini utu wako. Amini akili na uwezo wako, ikiwa kama haoneshi kukupenda achana naye. Kulia kwa mtu asiyejali ni kupoteza muda tu. Ni sawa na kuimba nyimbo nzuri kwa mtu asiyesikia. Haina maana kabisa.

Mwandishi wa makala hii ni mtaalamu mbobezi wa masuala ya ushauri wa uhusiano, maisha na utulivu wa hisia

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU