HURUMA YA MOURINHO NDIYO ITAKAYOWANUSURU CARRICK, HERRERA MAN UTD

HURUMA YA MOURINHO NDIYO ITAKAYOWANUSURU CARRICK, HERRERA MAN UTD

618
0
KUSHIRIKI

 

LONDON, England

HADI sasa mambo yanaonekana kuwa magumu kwa nyota wawili Man Utd; Michael Carrick na Ander Herrera, baada ya kushindwa kupangwa kwenye kikosi cha kwanza ukiwa ni mwanzoni mwa msimu huu licha ya kocha wao, Jose Mourinho, kuwaliwaza akisema kuwa wana mchango mkubwa katika mipango yake.

Hii ni kutokana na kwamba nahodha wa klabu hiyo,  Carrick, msimu huu hajaambulia mechi hata moja katika kikosi cha Man Utd huku mchezaji bora wa msimu uliopita wa klabu hiyo, Herrera,  akiambulia kucheza mara moja katika kikosi cha kwanza kati ya michezo mitano ambayo timu hiyo imeshazicheza kwenye michuano ya Ligi Kuu England.

Kwa sasa Mourinho anaonekana kuwaamini katika safu ya kiungo, Nemanja Matic na  Marouane Fellaini, kuliko nyota hao wawili na  huku aking’ata na kupuliza akidai kuwa  Carrick  na  Herrera   watapata nafasi ya kucheza jambo ambalo linadhihirisha  wazi kuwa itategemea na huruma yake kuwafikiria  mastaa hao.

“Kwa Carrick na Ander ni jambo la kuvuta subira kwani kuna wakati utawadia,” hiyo ni moja ya kauli ya Mourinho aliyoitoa hivi karibuni kupitia kwenye tovuti ya klabu hiyo.

“Watakuja kuwa wachezaji muhimu kwetu nina uhakika. Hii ni timu, hiki ni kikosi hatuwezi kuwachezesha wachezaji 11 pekee,” aliongeza kocha huyo katika taarifa hiyo.

Wakati mastaa hao wakipakwa mafuta kwa mgongo wa chupa, mwenzao, Matic ambaye amesajiliwa kutoka kwenye klabu ya zamani ya Mourinho,  Chelsea kabla ya dirisha la usajili halijafungwa, kwa haraka ameshaanza kuchomoza  na hivi karibuni alitangazwa kuwa shujaa wa mechi katika ushindi wa mabao 4-0  walioupata dhidi ya timu za West Ham United na Everton na huku  Fellaini akionekana kufanya vyema katika michezo aliyoanzishwa kikosi cha kwanza na hata akitokea benchi.

Hata hivyo, pamoja na hali hiyo, Mourinho  bado anang’ang’ania kwa utaratibu wake ni lazima wachezaji watacheza kwa mzunguko jambo ambalo bado linatia shaka kuhusu hatima ya wawili hao.

“Sergio Romero alicheza mechi ya fainali ya Ligi ya  Europa ambayo ndiyo ilikuwa kubwa kwetu  msimu uliopita na mpaka sasa hajacheza. Herrera ni mchezaji bora wa klabu, pia msimu uliopita hajakanyaga kikosi cha kwanza. Nadhani mnafahamu haya ndiyo maisha katika klabu kubwa,” anasema Mourinho.

“Tulimpa Michael Carrick, mkataba mpya kwa sababu ni mchezaji tegemeo. Hili ni jambo tu ambalo lipo ndani ya timu ambapo Matic na Fellaini  wapo kwenye ubora wao na si kwamba siwaoni,” anasema Mreno huyo.

Pia kauli hii inaweza kutafsiriwa kama ni ya kuwaliza mastaa hao kama ilivyowahi kutokea kwa nyota wengine ambako Mreno huyo amepitia, lakini matokeo yake wakajikuta wakiambulia kusugua benchi na hatimaye wakaamua kuondoka.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU