KWANINI MOURINHO ASIWAPANGE RASHFORD, LUKAKU NA MARTIAL KWA PAMOJA?

KWANINI MOURINHO ASIWAPANGE RASHFORD, LUKAKU NA MARTIAL KWA PAMOJA?

687
0
KUSHIRIKI

MANCHESTER, England

JOSE Mourinho si tu kwamba yuko kwenye nafasi ya kubeba taji la Premier League msimu huu, bali ana nafasi ya kubadilisha kila kitu kwenye historia yake.

Nafasi ya kubeba taji kwa soka la kuvutia na si kupaki basi kama alivyozoeleka na wengi.

Hivi sasa timu mbili za Jiji la Manchester zinaonekana kutawala EPL, iko vita ya chini kwa chini inayoendelea kwenye vichwa vya mashabiki wao. Vita ya makocha.

Pep Guardiola, mtaalamu wa soka la kuvutia dhidi ya Jose Mourinho, mwanadamu anayefurahia kushinda kwa soka lisilovutia.

City ya Guardiola inavutia kuitazama. Inacheza soka safi kwa kusaka matokeo kwa utulivu. United ya Mourinho, japo ina ishara ya kubadilika kidogo, lakini kwa asilimia kubwa wanacheza soka kwa hofu sana.

Lakini kwa hali ilivyo sasa katika kikosi cha Manchester United, Mourinho ana nafasi ya kutengeneza timu yenye safu kali ya ushambuliaji.

Jose anaweza kuwaunganisha mastraika wake watatu kwenye kikosi kimoja. Akawa na Marcus RashfordAnthony Martial na Romelu Lukaku. Unaionaje hii United?

Changamoto pekee inayomkabili Jose kwa sasa ni kusaka mfumo mzuri atakaoweza kuutumia kwa watatu hawa.

Lukaku ni chaguo la kwanza, limeshathibitika hili. Lakini ni mpaka lini Martial na Rashford, wataendelea kuvumilia kupishana uwanjani? Kwanini hawako kwenye kikosi cha kwanza kwa pamoja?

Katika umri wa miaka 19, Rashford yuko kwenye hatua za kuendelea kujifunza baadhi ya mambo, uwezo wake dhidi ya West Ham, Jumapili iliyopita ulithibitisha hili. Lakini Martial, Desemba mwaka huu, atatimiza miaka 22. Ni umri sahihi wa kucheza soka katika kikosi cha kwanza.

Chini ya Mholanzi, Louis van Gaal, wawili hawa walikuwa na nafasi ya kucheza pamoja kwenye kikosi cha kwanza. Japo hawakupata mafanikio makubwa, lakini walionyesha kuna kitu kikubwa ndani yao kama wakiendelea kucheza pamoja.

Lakini huu ni mtihani mkubwa kwa Jose, hasa ukizingatia Januari, mwakani, atakuwa na nyongeza ya Zlatan Ibrahimovic, katika kikosi chake.

Kwenye Premier League, msimu uliopita, Jose aliwapanga mara tano makinda hawa. Dhidi ya Watford, Manchester City, Arsenal, West Brom na Swansea, lakini United hawakufanikiwa kupata ushindi kwenye mechi hizo.

Msimu huu, Rashford ameanza kwenye michezo minne na kuingia akitokea ‘sub’ mara moja, huku Martial akitokea ‘sub’ mara nne na kuanza mchezo mmoja.

Kwa sasa inaonekana ni ngumu sana kubadilisha timu ya ushindi. United wako kwenye kiwango bora mno. Litakuwa jambo la ajabu kubadilisha mfumo haraka hivi.

Anaweza akasubiri, si lazima sasa, lakini kichwani anatakiwa kuelewa kuwa Lukaku, Rashford na Martial, ni ‘utatu mtakatifu’ utakaoifanya United itishe zaidi msimu huu.

Kwa ripoti ya fedha iliyotolewa juzi Alhamisi, United bado ni timu imara kiuchumi, lakini ni muda mrefu umepita sasa tangu mashabiki waishuhudie timu yao ikiwaburudisha uwanjani.

Na kwa uwepo wa Mourinho, msimu huu, kuna dalili za United kuendelea kushinda bila kucheza soka la kuvutia.

Tazama msimu uliopita, United walibeba mataji matatu, lakini hayakuja kwa mtindo unaovutia. Walishinda walipotakiwa kushinda, si vinginevyo.

Msimu huu wako kwenye michuano mingi. Wanahitaji kufanya ‘rotation’ ya kikosi, na pengine ndio wazo la Jose kwa sasa, lakini ni lazima ajaribu kufikiria pia jinsi ya kuwapanga mastraika wake watatu kwa pamoja.

United wanatakiwa kuwa tishio, kutengeneza safu kali ya ushambuliaji itakayoogopwa na mabeki wa timu pinzani.

Ni kazi ya Jose kufikiria hili kwa makini. Ndani ya kikosi chake kwa sasa ana vijana wenye kasi, nguvu na uwezo mkubwa wa kufunga. Kilichobaki ni kuwapa nafasi tu.

Martial, Rashford na Lukaku wanasubiri mfumo sahihi utakaowapa nafasi ya kucheza pamoja na kuiletea United matokeo yatakayoifanya iwe timu yenye kuvutia zaidi msimu huu.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU