YANGA MWENDOKASI KIMARA: SIMBA WALIKUWA WANAKULA UGALI KWA MLENDA WAKACHEKELEA

YANGA MWENDOKASI KIMARA: SIMBA WALIKUWA WANAKULA UGALI KWA MLENDA WAKACHEKELEA

1713
0
KUSHIRIKI

MASHABIKI wa timu za Yanga na Simba siku zote hawaishiwi kutupiana vijembe, kiasi kwamba hata kama mmojawapo amezidiwa si rahisi kumpa sifa mwenzake na kukubali kujishusha.

Katika mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara zinazoendelea, ni wazi kuwa Simba wameanza vizuri kuliko watani zao Yanga, lakini Wanayanga bado wanajikubali kuwa wao ni bora kuliko Wekundu wa Msimbazi hao.

Yanga imecheza mechi tatu, ikashinda bao 1-0 na kutoka sare ya bao 1-1 katika michezo miwili dhidi ya Lipuli na Majimaji, ambapo leo watashuka dimbani kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, kukipiga na Ndanda FC.

Simba wao wamecheza mechi nne, mbili wakatoka na ushindi mnono, ambapo mchezo wa awali waliichapa Ruvu Shooting mabao 7-0, wakaifunga Mwadui 3-0, wakatoka sare na Azam FC bila kufungana na Mbao FC 2-2.

Kutokana na matokeo hayo, katika msimamo wa ligi, Simba wapo nafasi ya pili wakiwa na pointi nane huku Yanga wakiwa nafasi ya saba na pointi tano.

Licha ya hayo, mashabiki wa tawi la Yanga Mwendokasi lililopo Kimara, jijini Dar es Salaam, wamewatupia dongo watani zao na kusema matokeo wanayopata ni kama walikuwa wanakula ugali na mlenda halafu wanachekelea.

Maneno hayo yanatoka kwa Katibu Mkuu wa tawi hilo, Abdallah Gonza, akimaanisha kuwa Simba walikuwa hawajakutana na timu ngumu kama Azam FC na Mbao FC zilizowabana na kuambulia sare.

“Ujue hata mgonjwa ukimpa ugali na mlenda anameza tu bila shida, ndio mechi za Simba walizoshinda kwani wamekutana na timu nyepesi, mbona Azam na Mbao hawajafunga.

“Yanga hatuna presha na matokeo tunayopata kwa sababu hatujafungwa, kama kawaida yetu tunakuja taratibu na watapisha wenyewe kwenye nafasi yetu bado naamini tunatetea ubingwa,” anatamba Gonza.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU