NI NGOMA AU LWANDAMINA TATIZO YANGA?

NI NGOMA AU LWANDAMINA TATIZO YANGA?

2769
0
KUSHIRIKI

NA MICHAEL MAURUS

YANGA juzi jioni kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, ilipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Ndanda FC ya Mtwara, katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, huo ukiwa ni ushindi wao wa pili ndani ya mechi nne msimu huu.

Matokeo hayo yameiwezesha Yanga kufikisha pointi nane na hivyo kukabana koo na watani wao wa jadi, Simba ambao nao wana idadi kama hiyo ya pointi, lakini Wekundu wa Msimbazi hao wakiwa na mabao 12 dhidi ya matano ya wakongwe wenzao hao.

Kabla ya mchezo huo wa juzi, wapenzi wa Yanga na baadhi ya wachambuzi wa soka nchini, walikuwa na matumaini makubwa kwamba mabingwa hao wa Tanzania Bara wangeshinda kwa idadi kubwa ya mabao.

Miongoni mwa sababu za imani yao hiyo, ni kutokana na ukweli kwamba ilitua Uwanja wa Uhuru, ikitokea kwenye viwanja vya mikoani (Njombe na Ruvuma) ambavyo ilivilalamikia kuwa havikuwa na ubora, hivyo kuwakwamisha wachezaji wao kucheza katika viwango vyao vya kawaida na mwisho wa siku kushindwa kutoa dozi ya mabao kama walivyokuwa wakitarajia.

Katika mechi zao mbili za mikoani, Yanga ilipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Njombe Mji mjini Njombe, kabla ya kuambulia sare ya bao 1-1 ilipovaana na Majimaji mjini Songea.

Na ikiwa inacheza kwenye uwanja unaoaminika kuwa ni bora wa Uhuru, watu wa Yanga waliamini wangeichabanga Ndanda idadi kubwa ya mabao, lakini mwisho wa siku waliambulia moja tu, shukrani ziende kwake Ibrahim Ajib aliyefunga bao hilo pekee la timu yake hiyo mpya aliyojiunga nayo msimu huu akitokea Simba.

Lakini pia, sababu nyingine iliyokuwa ikiwapa jeuri watu wa Yanga kutoka uwanjani na ushindi mnono juzi, ni matokeo ya mechi ya Alhamisi ya wiki iliyopita ya watani wao wa jadi, Simba ambao waliambulia sare ya mabao 2-2 dhidi ya Mbao FC kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Matokeo hayo yaliaminika yangewapandisha mzuka wachezaji wa Yanga kucheza kufa au kupona ili kupata ushindi mnono zaidi dhidi ya Ndanda na hivyo kujibu mapigo ya Simba waliotoa kipigo cha ‘mbwa mwizi’ cha mabao 7-0 dhidi ya Ruvu Shooting na cha 3-0 walipovaana na Mwadui kwenye Uwanja wa Uhuru.

Lakini baada ya mchezo huo wa juzi, mjadala uliobaki kwa mashabiki ulikuwa ni juu ya ubutu wa safu ya ushambuliaji ya Yanga, wakidai kuwa timu hiyo ilistahili kufunga mabao mengi kwani wapinzani wao hao hawana timu ya kutisha.

Pia, wapo waliodai kuwa ushindi huo wa bao moja ulitosha kabisa kwani Yanga inapochuana na Ndanda huwa inapata wakati mgumu, wakitolea mfano jinsi ambavyo wamekuwa wakipata ushindi kwa mbinde mara kadhaa kufungwa au kuambulia sare dhidi ya Wanakuchele hao.

Pamoja na utetezi huo ambao hauna msingi hata kidogo kutokana na ukweli kwamba kikosi cha Ndanda kimebomolewa mno baada ya kuondokewa na wachezaji wake mahiri, Kiggi Makasi, Paul Ngalema na Atupele Green waliotimkia Singida United.

Kwa hali hiyo, hoja ya kwamba Yanga inapocheza na Ndanda huwa inakuwa na wakati mgumu, inaonekana haina mashiko, hasa kutokana na jinsi timu hiyo ilivyofanya mashambulizi mengi na makali langoni mwa wapinzani wao hao, ikiwamo mashuti mawili kugonga mwamba wa juu.

Kinachoonekana ni kwamba kuna tatizo ndani ya kikosi cha Yanga na iwapo halitafanyiwa kazi, mashabiki wa timu hiyo wanaweza kujikuta wakizidi kupungua viwanjani na kujikuta wakijazana kwenye baa kuwashuhudia akina Romelu Lukaku, Sergio Aguero, Neymar, Cristiano Ronaldo, Alexis Sanchez, Alvaro Morata na wengineo wakifanya mambo huko Ulaya.

 

Lwandamina ndio tatizo Yanga?

Kuna wanaoamini tangu Hans van der Pluijm alivyoondolewa Yanga na mikoba yake kuchukuliwa na kocha wa zamani wa Zesco ya Zambia, George Lwandamina, makali ya safu ya ushambuliaji ya timu hiyo yamepungua.

Watu wa Yanga wanadai Lwandamina uwezo wake wa kutengeneza kikosi cha ushindi mnono ni mdogo ukilinganisha na Pluijm ambaye enzi zake, ushindi wa mabao zaidi ya 5-0 hakikuwa kitu cha kushangaza kwa mabingwa hao wa Bara.

Na hata baada ya mchezo wa juzi, wapo waliokuwa wakishauri Pluijm kurejeshwa Jangwani, wakidai kwamba hata huko aliko, Singida United, hana furaha kwani suala la mshahara limekuwa tatizo.

Pia, wapo wanaomlaumu kocha huyo kwa kuwapa mazoezi makali wachezaji wake hata siku chache kabla ya mechi, akidaiwa anawachosha wachezaji wake na kuwafanya kuwa wazito.

Hoja hii kidogo imekuwa na ukakasi kutokana na ukweli kwamba kwa uzoefu alionao, akiwa ameibeba Zesco na kufika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, sidhani kama hafahamu madhara ya mazoezi makali kwa wachezaji wake siku chache kabla ya mechi.

Lakini tunapomlaumu Lwandamina, hebu tutupie macho na aina ya wachezaji alionao na utamaduni wa soka la Yanga.

Inafahamika kuwa soka la Yanga ni la kasi, mipira mirefu na mabao yake mengi, hutokana na mipira ya kona au shambulizi la kushtukiza.

Kwa miaka na miaka, Yanga imekuwa ikibebwa na mawinga wenye kasi. Wakumbuke akina Edibily Lunyamila, Abubakar Salum ‘Sure Boy’, Sanifu Lazaro ‘Tingisha’, Said Maulid ‘SMG’, Joseph Lazaro, Thomas Kipese ‘Uncle Tom’, Akida Makunda, Mrisho Ngassa na Simon Msuva aliyeondoka Jangwani hivi karibuni na kutua timu ya Difaa al Jadida inayoshiriki Ligi Kuu nchini Morocco.

Lakini hebu tukitupie macho kikosi cha Yanga cha sasa, kuna winga aina ya akina Lunyamila, Tingisha, Makunda au hata Msuva?

Jibu ni rahisi, hakuna. Kama ni Mwashiuya, bado hajaiva akiwa ameathiriwa mno na wimbi la majeruhi. Iwapo kijana huyo kutoka Mbeya asingekumbwa na majeraha, kwa muda ambao amekuwa Yanga, kwa sasa angekuwa msaada mkubwa kwa timu hiyo, kwani anaonekana kuwa na uwezo wa kufuata nyayo za akina Msuva, hasa kutokana na mbio, lakini zaidi ni krosi zake murua zinazotua kwa mlengwa katika muda na nafasi sahihi.

Mwashiuya anaonekana kuwa na faida zaidi ya nguvu ambapo anapoamua kuchanja mbuga, ni nadra sana kutolewa kwenye njia.

Kwa sasa wachezaji wanaopangwa pembeni Yanga wengi wao ni viungo ambao majukumu yao ni kuua winga na kuongeza idadi ya viungo, huku wakitoa nafasi kwa mabeki wa pembeni kupiga krosi, kitu ambacho Gadiel Michael (kushoto) na Juma Abdul (kulia) wameshindwa kukifanya kwani timu inahitaji kuwa na mabeki wa pembeni wenye mapafu ya mbwa kama Erasto Nyoni au Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ wa Simba.

Vipi kuhusu mashambulizi ya kati? Hili ni tatizo kwa Yanga, tangu kupotea kwa washambuliaji wa aina ya Makumbi Juma, Peter Tino, Abeid Mziba, marehemu Said Mwamba ‘Kizota’, Mohammed Hussein ‘Mmachinga’ au hata Mbrazil Jenilson Santos ‘Jaja’, kwa sasa hakuna mshambuliaji mwenye uwezo wa kupokea pasi ya kati na kuwatoka mabeki na hatimaye kucheka na nyavu.

Angalau Obrey Chirwa anaweza kufanya hivyo au hata Ajib, lakini kukosekana kwa majeruhi, Amissi Tambwe ambaye naye huwa si haba katika hilo, nako kumekuwa tatizo japo mwisho wa siku, utamaduni wa soka la Yanga (kutumia ziadi mawinga) unaonekana ‘kuwalevya’ washambuliaji hao kiasi cha muda mwingi kushambulia wakitokea pembeni.

Nini kifanyike? Lwandamina ni vema akatuliza kichwa chake na kutafuta suluhisho la matatizo yaliyopo kwenye kikosi chake. Ni vema akapambana na hali yake na hali ilivyo ndani ya Yanga.

Kwa sasa hakuna muda wa kuilaumu Kamati ya Usajili ukizingatia sote tunafahamu jinsi Yanga ilivyohaha katika suala zima la usajili, ikiwa imeshindwa kuwanasa wachezaji wengi iliyokuwa imewapigia hesabu kutokana na suala zima la ukata.

 

Vipi kuhusu Ngoma? Anawaibia Yanga?

Baada ya mchezo wa juzi, kuna mashabiki walikuwa wakimtupia lawama Donald Ngoma wakidai kuwa mshambuliaji wao huyo wa kati, hajaamua kucheza.

Mashabiki hao wanaamini Ngoma ana uwezo wa kuwabeba lakini anaonekana kucheza chini ya kiwango, wakati aliwaringia mno wakati wa usajili akitaka alipwe fedha zake zote ndipo ‘amwage wino’.

Walifika mbali zaidi wakimtaka Lwandamina kumweka benchi Ngoma kutoa nafasi kwa Ajib kucheza pamoja na Chirwa katikati.

Binafsi nadhani suala la Ajib kucheza pamoja na Chirwa ambaye anaonekana kurejea kwa kasi, lina mashiko bila kujali kama Ngoma anacheza chini ya kiwango au la.

Kwa kuwapanga Ajib na Chirwa, maana yake pembeni kushoto anakuwapo Mwashiuya au Emmanuel Martin na kulia Rafael Daudi ambaye kazi yake itakuwa ni kuongeza idadi ya viungo kutoa nafasi kwa Abdul kupanda.

Abdul hatakuwa na sababu za kushindwa kusaidia mashambulizi kwa wakati huu Yanga ikiwa na kiungo mkabaji asilia, Pappy Kabamba Tshishimbi ambaye ameonekana kuwa na uwezo wa hali ya juu kusaidia safu ya ulinzi na kupandisha mashambulizi pia.

Kwa upande wa Ngoma, ninapata shaka kidogo na kiwango chake cha sasa, sijui ni woga wa kupata majeraha! Ngoma wa sasa si yule tuliyekuwa tukimfahamu. Ngoma yule hakuwa akipoteza mpira kirahisi. Kila ‘golikiki’ iliyopigwa kutoka langoni kwake, yeye ndiye aliyekuwa wa kwanza kuucheza mpira kabla ya beki wa timu pinzani. Uwe ni wa juu au wa chini.

Lakini kwa sasa imekuwa tofauti. Ngoma amekuwa laini mno kama ilivyojionyesha juzi kwani alimiliki mipira wa golikiki miwili tu kati ya 14, mara nyingi alijikuta akizidiwa ujanja na mabeki wa Ndanda.

Hata alipopata nafasi ya kuelekea golini, Ngoma alijikuta akiipoteza katika mazingira ya kushangaza na mwisho wa siku kuwaacha mashabiki wa Yanga wakiishia ‘kukaanga chipsi’.

Ukiachana na safu ya ushambuliaji, beki haina tatizo sana japo Gadiel anatakiwa kuongeza umakini katika kukaba, lakini pia pasi zake maana juzi kuna wakati alijikuta akipoteza mipira kirahisi. Lakini pia benchi la ufundi la Yanga ni vema wakakaa na Tshishimbi ili kumuonya na suala zima la uchezaji rafu zisizo na msingi ambazo zinaweza kuigharimu timu kama ilivyojitokeza, ambapo tayari ataukosa mchezo muhimu ujao wa timu yake dhidi ya Mtibwa Sugar baada ya kupata kadi tatu za njano.

Pia, Tshishimbi juzi alipoteza mipira zaidi ya sita ambapo pasi zake nyingi zilinaswa na wachezaji wa Ndanda. Tatizo hili lazima mchezaji huyo alifanyie kazi.

Zaidi ya hapo, kikosi cha Yanga ni kizuri na bado kina nafasi kubwa ya kutetea ubingwa wao wa Ligi Kuu Tanzania Bara, lakini tu iwapo wachezaji watapewa sapoti inayostahili, yaani kulipwa mishahara na posho mbalimbali kulingana na makubaliano baina yao na uongozi, ukizingatia soka ndio maisha yao.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU