KENYA WALIVYOIKOSA CHAN 2018

KENYA WALIVYOIKOSA CHAN 2018

538
0
KUSHIRIKI

NAIROBI, Kenya

HATIMAYE Kenya haitakuwa mwenyeji wa fainali za Mataifa Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (Chan) zilizotarajiwa kufanyika mwakani.

Uamuzi huo umetokana na kikao cha siku moja cha Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka barani Afrika (Caf), kilichofanyika mjini Accra, Ghana, kikiongozwa na Rais Ahmad Ahmad.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Caf, wamefikia uamuzi huo baada ya kujiridhisha na uchunguzi wa kina kuelekea michuano hiyo inayoshirikisha mataifa 16, inayotarajiwa kuanza kutimua vumbi Januari 12 na kumalizika Februari 4.

Jopo la wachunguzi wa Caf liliwasili Kenya kuanzia Septemba 11 hadi 17 mwaka huu na kukuta mazingira yasiyoridhisha licha ya kuwa ni miezi michache imebaki kabla ya kuanza rasmi kwa mashindano hayo.

Kwa mujibu wa ripoti ya jopo hilo, ni kiwanja kimoja pekee kati ya vinne kilichokuwa kimekamilika na kufikia viwango vya Caf.

Lakini pia, maofisa wengine wa Caf waliokuwa kwenye kikao mjini Accra waliibua madai ya hali ya siasa nchini humo, wakihofia kuwa huenda hekaheka za uchaguzi mkuu zikatibua michuano.

Waliwasilisha hoja kwamba huenda hali ya usalama nchini Kenya ikawa si rafiki kwa mashabiki, wachezaji, makocha na viongozi wa timu, ikizingatiwa kuwa uchaguzi wa marudio utafanyika mwezi ujao.

Mbali na kuandaa, pia Kenya wanapoteza pia haki ya kushiriki fainali hizo kwa kuwa walifuzu moja kwa moja kama wenyeji.

Mataifa ambayo yalikuwa yakitarajiwa kutua nchini humo kwa mashindano hayo ni Angola, Burkina Faso, Cameroon, Congo Brazzaville, Equatorial Guinea, Guinea, Ivory Coast, Libya, Mauritania, Morocco, Namibia, Nigeria, Sudan, Uganda na Zambia.

Hata hivyo, kushindwa kuandaa fainali za Chan katika dakika za mwisho si suala geni kwa Kenya, kwani hilo limewahi kuwatokea na hii itakuwa mara yao ya pili.

Itakumbukwa kuwa waliwahi kukutwa na majanga hayo mwaka 1996 na nafasi yao kukabidhiwa kwa Afrika Kusini ambao waliishia kuutwaa ubingwa.

Kwa upande mwingine, Kenya kukosa nafasi hiyo ni pigo kubwa kwa Ukanda wa Afrika Mashariki. Kama wangefanikiwa, basi ingekuwa mara ya pili mfululizo kwa Ukanda huo kuandaa fainali hizo baada ya Rwanda kufanya hivyo mwaka jana.

Baada ya Kenya kupoteza fursa hiyo, kumekuwa na madai mbalimbali yanayozihusisha Morocco na Afrika Kusini kuwa wenyeji wa Chan hapo mwakani.

Pia, vyombo mbalimbali vya habari vimezitaja Ethiopia na Ivory Coast kuwa na nia ya kuandaa fainali hizo.

Chama cha Soka nchini Ghana nacho kinaitolea jicho fursa hiyo, hasa baada ya kuandaa fainali za Baraza la Vyama vya Soka Afrika Magharibi (Wafu).

Tetesi hizo ni licha ya taarifa ya Caf iliyoweka wazi kuwa mchakato wa kumsaka mwenyeji mpya wa michuano hiyo utaanza hivi karibuni.

Wakati huo huo, mbali na kuivua Kenya wenyeji wa Chan, wajumbe wa Caf waliokutana Accra walikubaliana kuwa Cameroon itabaki kuwa mwenyeji wa fainali za Mataifa Afrika (Afcon) kwa mwaka 2019.

Walikubaliana kuwa Cameroon itabakiwa na haki hiyo ingawa kamati ya maandalizi inatakiwa kufika mapema nchini humo ili kuchunguza miundombinu.

Lakini pia, uamuzi mwingine katika kikao hicho ulikuwa wa kuitangaza Misri kuwa mwenyeji wa fainali za mwaka 2019 za Afcon kwa vijana wenye umri wa chini ya miaka 23.

Ifahamike kwamba Mafarao wamejipatia nafasi hiyo baada ya Zambia kujitoa kwa madai ya matatizo ya kifedha za kuendeshea michuano hiyo.

Mshindi wa fainali hizo za makinda atakuwa amejihakikishia tiketi ya kwenda kushiriki michuano ya Olimpiki ya mwaka 2020 itakayofanyika Tokyo, Japan.

 

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU