CHONDE CHONDE YANGA, SIMBA  ZISICHEZEE UHURU OKTOBA 28

CHONDE CHONDE YANGA, SIMBA  ZISICHEZEE UHURU OKTOBA 28

779
0
KUSHIRIKI

MECHI ya watani wa jadi, Yanga na Simba, imepangwa kuchezwa Oktoba 28, mwaka huu, lakini hadi sasa haijajulikana itachezwa kwenye uwanja upi, kutokana ule wa Taifa, jijini Dar es Salaam,  kufungwa kwa ajili ya ukarabati unaoendelea.

Kutokana na hali inavyoendelea, kuna uwezekano mdogo wa Uwanja wa Taifa, unaobabe mashabiki 60,000 wanaoketi kwenye viti kutumika, baada ya serikali kusema kwamba, ukarabati wake utachukua miezi mitatu.

Kwa sababu hiyo, ukarabati wa uwanja huo utakuwa haujakamilika itakapofikia Oktoba 28 kwa kuwa nyasi zilizopandwa zitakuwa hazijakomaa kwa Yanga na Simba kuweza kuutumia.

Tayari Serikali kupitia Mkurugenzi wa Idara ya Michezo, Alex Mkenyenge, amesema itakuwa ni vigumu kuruhusu uwanja huo kutumika kwa tukio lolote kwa sasa mpaka utakapokamilika ukarabati wake.

Kwa kauli ya Serikali, Yanga, watakaokuwa wenyeji wa mechi hiyo wajifikirishe na kuchagua uwanja mwingine utakaotumika kwa mchezo huo.

Sisi BINGWA tunaona kwamba Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam, wenye una uwezo wa kuchukua mashabiki  wasiozidi 25,000, hautaweza kukidhi mahitaji ya mashabiki wengi.

Yanga na Simba zina mashabiki kila kona ya Tanzania na watakuwa wanataka kwenda uwanjani siku hiyo kuzishangilia timu zao ili kupata ushindi, lakini bila usalama wa kutosha kunaweza kutokea majanga.

Lakini kutokana na Uwanja wa Taifa kufungwa hadi Desemba mwaka huu, TFF na Yanga wakubaliane pamoja mechi hiyo ichezwe kwenye uwanja mwingine watakaouona una usalama.

BINGWA tunatoa tahadhari mapema kwa TFF na vyombo vya ulinzi na usalama kuwa makini iwapo mechi hiyo itaamuliwa kupigwa kwenye Uwanja wa Uhuru, tunauoana mdogo.

Hofu yetu ni kwamba Uwanja wa Uhuru unaweza kufurika mashabiki wengi na vyombo vya dola kushindwa kudhibiti hali ya usalama.

Ni vizuri TFF na Yanga wakafikia uamuzi wa kuipeleka mechi kwenye uwanja tunaoamini utakuwa salama kwa mashabiki watakaokwenda kushuhudia pambano hilo.

Tunasema chonde chonde mechi ya Yanga na Simba isipigwe kwenye Uwanja wa Uhuru ili kuepuka madhara.

 

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU