CHIRWA; YANGA WANATAKA MABAO SI NDONDI

CHIRWA; YANGA WANATAKA MABAO SI NDONDI

1992
0
KUSHIRIKI

JUZI jioni katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, mshambuliaji wa Yanga, Obrey Chirwa, alifanya kituko cha mwaka baada ya kumshambulia kwa makonde mwandishi na mpigapicha, John Dande.

Dande ambaye ni mfanyakazi wa New Habari (2006) Limited, wazalishaji wa magazeti ya Bingwa, Dimba, Mtanzania, na RAI, alifika uwanjani hapo ili kutimiza majukumu yake kabla ya kukutwa na kasheshe hiyo.

Mbali ya kumrushia makonde katika sehemu mbalimbali za mwili, Chirwa pia alitishia kumchoma Dande na mkasi aliokuwa ameshika.

Kwa mujibu wa Dande, wakati wachezaji wa Yanga wakijiandaa kuingia uwanjani kwa ajili ya mazoezi, alikuwa akipiga picha, lakini ghafla akavamiwa na Mzambia huyo na kuanza kumshambulia.

Habari za Chirwa kumshambulia Dande, zimepokewa kwa hisia tofauti na wapenzi wa soka nchini, akiwamo Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh, ambaye alisema kitendo hicho ni utovu wa nidhamu akidai kuwa hata kocha mkuu wa timu hiyo, George Lwandamina, amekerwa nacho akiahidi kumchukulia hatua Mzambia mwenzake huyo.

BINGWA tunalaani kwa nguvu zote kitendo kilichofanywa na Chirwa ambacho si cha kiungwana hata kidogo, ukizingatia kwa kiwango cha uchezaji na mwonekano wake, hakupaswa kumshambulia mwanahabari huyo hata kama alikuwa amemkosea.

Chirwa ambaye amejikuta akiwa kipenzi cha wapenzi wa soka hapa nchini, hasa wale wa Yanga, hatuamini kama hafahamu nini majukumu na umuhimu wa vyombo vya habari.

Hatuamini kama Chirwa hafahamu jinsi magazeti ya New Habari, hasa BINGWA na DIMBA yalivyompamba mara baada ya kutua Yanga, lakini pia yanavyowajuza Watanzania, wakiwamo wale wanaoishi vijijini jinsi klabu yake hiyo ilivyolamba dume kwa kumsajili.

Lakini pia, hatuamini kama Chirwa hafahamu jinsi magazeti ya New Habari wanavyowapa matumaini watu wa Yanga kuwa ukame wa mabao Jangwani utakoma mara tu mshambuliaji huyo atakapokaa sawa baada ya kuandamwa na majeraha, lakini pia kuwa nje ya kikosi kwa muda mrefu akitumikia adhabu.

BINGWA hatuamini kama Chirwa hafahamui nini watu wa Yanga wanakitaka kutoka kwake kwa sasa wanapomwona Emmanuel Okwi wa Simba akiongoza kwenye msimamo wa mabao akiwa na mabao sita ambayo ni zaidi ya yale yote yaliyofungwa na timu yake ndani ya mechi nne za Ligi Kuu Tanzania Bara.

Sasa Chirwa huyo huyo ambaye BINGWA na DIMBA wamekuwa wakimfagilia mara kwa mara, leo hii anampiga mwandishi wa magazeti hayo! Nini kimemkumba Mzambia huyo?

Ni akili yake au ameanza kutumia vitu vinavyoathiri uwezo wake wa kufikiri? Hebu tuwaachie Yanga watupe majibu ya maswali yetu maana klabu hiyo siku zote imekuwa mstari wa mbele katika kukemea vitendo vya kihuni kama hicho na utovu wa nidhama kwa ujumla, kuanzia kwa wachezaji hadi mashabiki wao.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU