DUH! HII ISHU YA ARSENAL BALAA

DUH! HII ISHU YA ARSENAL BALAA

649
0
KUSHIRIKI

>>Arsenal inacheza mechi tatu ndani ya siku sita

>>Mechi yao leo dhidi ya BATE Borisov ni baada ya safari ya maili 2,400

LONDON, England

WIKI iliyopita kocha wa klabu ya Arsenal, Arsene Wenger, alipokuwa akihojiwa na waandishi wa habari alijaribu tu kujifanya kama vile klabu yake haitapata shida sana kwenye michuano ya Ligi ya Europa msimu huu tofauti na Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Wenger alijaribu kufafanua kuwa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya imekuwa ya ‘kawaida’ na alisema ‘imepoteza nguvu ya ushawishi’.

Lakini kama kocha huyo bado atakuwa na hamu ya kuendelea kuiongoza timu yake msimu huu kwenye Ligi ya Europa ambayo walijikuta wakiingia msimu huu baada ya miongo miwili ya kushiriki Ligi ya Mabingwa, basi hamu yenyewe inaweza kuisha kuanzia leo.

Wenger na vijana wake wiki hii wanakutana na jinamizi la ratiba ambapo juzi Jumatatu walianza na West Brom kwenye mchezo wa Premier League kabla ya kusafiri umbali wa maili 2,404 hadi nchini Belarus kwa ajili ya kuvaana na BATE Borisov kwenye mchezo wa Ligi ya Europa usiku wa leo.

Watakaporudi mjini London, ‘The Gunners’ wataingia tena dimbani, Emirates, Jumapili mchana dhidi ya Brighton & Hove Albion. Hivyo ndani ya siku sita watakuwa wamecheza mechi tatu.

Licha ya kwamba muda wa kusafiri kwa ndege hadi Belarus hauzidi saa tatu angani, muda wa kurudi katika ufiti wa kucheza vizuri kati ya mechi na mechi utakuwa umebana sana na bila shaka Wenger hatakuwa na kitu kipya cha kukiongeza kwenye kikosi chake pindi watakapokuwa mazoezini.

Alipokuwa akiendelea kujibu maswali ya waandishi, Wenger alikuwa akitoa sauti fulani hivi ambayo kwa kiasi fulani ilisikika kama ni ya mtu aliyechukia aliposema: “Kwa sababu mechi zote tatu (kuanzia ile ya West Brom) zinatakiwa kuoneshwa kwenye runinga, ndiyo maana imekuwa hivi.

“Ugumu unakujaje? Baada ya kumaliza mchezo wa Ligi ya Europa kule Belarus, tutatakiwa tena kucheza Jumapili mchana.

“Kuanzia Jumatatu (juzi) hadi Alhamisi (leo), tutakuwa na muda mfupi hasa kuanzia Alhamisi hadi Jumapili (keshokutwa). Lakini inakubidi uzoee kila kitu.

“Labda tufanye maamuzi fulani dhidi ya BATE Borisov ambayo yatatupa nafasi ya kuendelea kuwa fiti kati ya hizi mechi mbili.”

Ligi ya Europa kimsingi ni michuano migumu na inayochosha, kama mashabiki wa Arsenal walidhani ni mizuri kama Ligi ya Mabingwa Ulaya basi watambue kuanzia sasa.

Kwa kawaida timu kutoka mataifa yaliyojificha Mashariki mwa Ulaya ndiyo yanayonogesha michuano hiyo, ikiwa na maana kuwa lazima safari zake ziwe ni za mbali na muda mrefu.

Msimu uliopita klabu kama Manchester United ilijikuta kwenye ratiba ya kuchosha ingawa walifanikiwa kulitwaa taji lenyewe, safari za mbali walizosafiri ni kama vile kwenda Ukraine kuvaana na Zorya Luhansk, Uturuki dhidi ya Fenerbahce na Urusi dhidi ya Rostov.

Safari ya kuelekea Belarus ilikuwa ni kwa wale mashabiki wabishi wa Arsenal, kwani tiketi zilizotolewa kwa ajili yao ni 794 tu ambao wataweza kuingia kwenye dimba la Borisov Arena lenye uwezo wa kupokea watazamaji 13,126.

Ndege za moja kwa moja kutoka England kuelekea uwanja wa ndege wa Belarus uliopo Minsk, zinapatikana kwa kiasi kidogo na ghali mno, sehemu za malazi nazo ni ndogo mjini Borisov, hadi ufike huko ni safari nyingine ya saa moja kutoka Minsk.

Kama hiyo haitoshi, uwanja watakaochezea Arsenal leo upo umbali wa takribani kilomita tano nje ya katikati mwa mji, ikiwa na maana kuwa safari za ndege, treni na magari zitahusika tena.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU