KUWA MAKINI, KWANINI MPENZI WAKO ANAKUWA HIVI?

KUWA MAKINI, KWANINI MPENZI WAKO ANAKUWA HIVI?

863
0
KUSHIRIKI

NA RAMADHANI MASENGA

UKO katika mahusiano kwa muda gani sasa? Toka uwe na mwenzako, nini kimepungua na nini kimeongezeka? Yapi mazuri yameongezeka? Mangapi mabaya yameongezeka.

Kwa yote mazuri yalioongezeka ni faida kwako na kwa mahusiano yenu. Hongereni. Ila kwa yale mabaya yaliyoongezeka inabidi utafakari kwa kina zaidi.

Kipi kinafanya mabaya yaongezeke? Kwanini kila siku katika maisha yenu kunatokea changamoto badala ya kupungua? Tatizo ni wewe ama ni yeye?

Tafakari kwa kina chanzo cha migogoro katika mahusiano yenu. Nani msababishi mkuu wa hiyo migogoro. Ni wewe ama ni yeye? Baada ya migogoro kutokea nani huwa na shauku ya kutaka kuimaliza? Ni wewe ama ni yeye?

Kama kila siku migogoro inaletwa na yeye, tena katika hali inayoonekana  ni ya kimakusudi kabisa kisha ni wewe pekee ndiyo huwa unaonesha nia na shauku ya kutaka kutatua hiyo migogoro huku yeye akionekana kutokuwa na habari.

Umewahi kujiuliza hii hali inatokana na nini?

Mapenzi ni suala la kubadilishana raha na amani katika maisha. Wewe umfanye mwenzako awe na amani, raha na msisimko zaidi maishani mwake.

Na yeye kupitia maneno na matendo yake akufanye usahau machungu ya dunia, unafiki wa walimwengu na kero za maisha.

Ni mara ngapi mpenzi wako anakusikiliza kwa makini juu ya manung’uniko na kero zako? Ni mara ngapi mpenzi wako anaguswa na matatizo na shida zako?

Nikisema shida mabinti wengi hukimbilia kuwaza shida za kipesa. Sitaki leo niwe katika mrengo huo. Nataka kuzungumzia shida za kihisia, mawazo na nyinginezo.

Shida za kipesa ni nzuri kusaidiana ila hazifai kufanywa kama kuwa kipimo pekee cha thamani ya mtu kwa mtu.

Ukimweleza mwenzako wasiwasi wako juu ya ukaribu wake na fulani huwa anajibu nini?

Ndiyo, unaweza kuwa wasiwasi wako tu juu yao na hakuna kitu kibaya kinachoendelea. Ila swali la msingi hapa ni kwamba anakujibu vipi? Thamani yako katika hisia zake iko vipi?

Kwa mtu mwenye kuthamini na kujali, japo wasiwasi wako ni wa bure ila atakujibu katika namna ya kukufanya ujue ni kwa namna gani wewe ni muhimu katika maisha yake.

Hata mara moja hawezi kusema kuwa nitolee wivu wako wa kijinga ama shauri yako. Kwanini mtu mwenye kukujali akujibu hivi? Kwani kuna ugumu gani kusema, hapana ukaribu wangu na fulani hauna chochote kisichotakiwa? Kuna ugumu gani kumthibitishia mpenzi wako uhalisia wa mambo ili nafsi yake ipoe?

Mapenzi ni kubembelezana. Bila kuonesha hisia za upole, unyenyekevu na busara kwa mwenzako mapenzi yako yana walakini.

Umuhimu wa mpenzi wako kwako unafaa kuonekana kupitia kauli na matendo yako. Sasa kama mtu haoneshi kujali namna unavyoumia ama kuhangaika na hisia zako za wivu juu yake na fulani, ni kwa namna gani useme anakupenda kwa kiwango stahili?

Mapenzi ni barabara yenye shida na changamoto nyingi. Ila wapenzi makini na wenye kujali huweza kupita katika barabara hii salama kwa sababu ya kujali, kuthamini na kwa unyenyekevu wao.

Katika barabara ya mapenzi kuna kukosea na kukosewa. Ila haya huwa hayana nguvu ya kutengua uhusiano wao kama wahusika wanajitambua na wanajinyenyekeza kwa kila mmoja.

Sikia kila kosa ni kubwa katika uhusiano. Ila pia unyenyekevu wa dhati na kujali hufanya makosa husika katika uhusiano yakose nguvu ya kuharibu uhusiano. Mwenzako yukoje kwako akikukosea?

Ni kweli kukosewa kunauma sana ila mwenzako anafanya nini kujaribu kupunguza maumivu ya kosa alilokufanyia. Ana kunyenyekea na kukuomba msamaha ili yaishe? Ama yeye huwa anakuacha na maumivu yako yakunyooshe vizuri?

Ni ujinga sana kuachana na mtu kisa kakukosea. Nani utakuwa naye na asikukosee? Ila pia inabidi utafakari mara mbili kuwa na mtu ambaye anakukosea na bado haoneshi kujali.

Bila unyenyekevu hakuna mapenzi. Na unyenyekevu upo katika kujali na kuthamini. Sasa vipi akuone unaumia hisia asijali na bado useme anakupenda?

Kila mmoja katika maisha anahitaji amani na furaha. Ila katika kupata amani na furaha kuna gharama yake. Ni lazima ukubali maumivu, kero na maudhi.

Ila kero na maudhi hayafai kusababishwa kila siku na mtu ambaye umemchagua kuwa mapenzi wako.

Mpenzi wako ndiyo mlinzi namba moja wa furaha na amani yako. Hata kama kuna kero ofisini, nyumbani  ama maskani kwenu, mpenzi makini anatakiwa ahakikishe ukiwa naye hizo kero, maudhi na karaha zinapotea ama unazisahau.

Ukiona mtu anakuona umejawa na simanzi baada ya kutoka kazini ama nyumbani kwenu na bado hajali. Basi jua hapo kuna vitu viwili. Huenda hatambui jukumu lake kwako kama mpenzi wako ama hajali hali zako kwa maana humgusi kihisia.

Thamani ya mtu kwa mtu ipo katika kujali na kupigania furaha na amani yake. Hata mara moja huwezi kusema kiwango chako cha mapenzi kwa fulani ni kikubwa hali humjali wala hutamini hali zake.

Kama mpenzi mwenye kujua majukumu na nafasi yako kwa mwenzako, hakikisha uwepo wako kwake unaleta kitu tofauti katika maisha.

Akiwa na wewe ajione yuko katika dunia nyingine, ya mbali iliyotengana na hii dunia iliyojaa kero, visa na karaha zisizoisha.

Mwandishi wa makala hii ni mtaalamu mbobezi wa masuala ya ushauri wa uhusiano, maisha na utulivu wa hisia( Psychoanalyst)

ramadhanimasenga@yahoo.com

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU