SI BURE, KAGERA SUGAR KUNA KITU

SI BURE, KAGERA SUGAR KUNA KITU

578
0
KUSHIRIKI

NA MWANDISHI WETU

UNAWEZA kusema ni bundi amewakalia kooni huko Kagera, kutokana na matokeo mabovu wanayoendelea kupata timu ya Kagera Sugar ‘Wana Nkurukumbi’, katika michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

Tayari mechi nne zimechezwa katika ligi hiyo iliyoanza Agosti 26, mwaka huu, huku kila timu ikitarajia kuvuna ilichopanda kutokana na kile watakachokionyesha.

Kagera Sugar ni timu ambayo ipo katika mabadiliko makubwa, tangu kutua kwa kocha kijana, Mecky Mexime, msimu uliopita ambaye ameonesha uwezo mkubwa.

Kagera iliyokua ikisuasua misimu michache, ilimaliza nafasi ya nne msimu uliopita wa 2016/17, huku kocha wake huyo akiibuka kocha bora wa msimu, lakini pia Juma Kaseja aliibuka kuwa golikipa bora.

Lakini tangu kuanza kwa ligi, Kagera haikuwa vizuri, ilianza msimu kwa kuchapwa bao 1-0 na Mbao FC ya jijini Mwanza, kisha ikalazimishwa sare ya bao 1-1 na Ruvu Shooting, ikatunguliwa na Azam bao 1-0 kabla ya juzi kubamizwa bao 1-0 na Singida United.

Kwa sasa Kagera ina pointi moja, huku ikishika mkia katika msimamo wa Ligi Kuu, unaoongozwa na Mtibwa Sugar yenye pointi 10 baada ya kushinda michezo mitatu na kutoka sare mmoja.

Nimekuwa nikisikiliza maelezo ya Mexime kila anapomaliza mechi na kugundua kuwa anatoa maelezo mepesi sana kama kocha katika kuelezea sababu kwanini timu imepoteza mchezo.

Mara ya kwanza Mexime alipofungwa alikaririwa akisema, hayo ni matokeo na haoni nani wa kumlaumu kutokana na matokeo hayo, watajitahidi waweze kurekebisha makosa katika mchezo uliopita.

Alipofungwa mara ya pili kocha huyo ambaye uwezo wake unajulikana katika kufundisha alikaririwa akisema mchezo una matokeo matatu, hivyo wao kufungwa na Azam si ajabu watahakikisha wanafuta makosa yao na kuweza kufanya vizuri.

Lakini baada ya kufungwa na Stand United, Mexime alikiri Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu ni ngumu, baada ya kufungwa mechi tatu huku akitoka sare mchezo mmoja.

Alieleza kuwa na timu nzuri ni jambo moja na kupata matokeo ni jambo lingine, hivyo anaamini muda si mrefu timu yake itaanza kupata matokeo.

“Kila mmoja alikuwepo uwanjani tumecheza mpira mwingi, lakini matokeo mazuri kwetu imekuwa historia, ‘all in all’ mambo mazuri yanakuja tuendelee kusubiri, nakubaliana na matokeo ya kufungwa, wametufunga kutokana na timu yangu kushindwa kukabiliana nao hasa kipindi cha pili walituzidi,” alisema.

Mexime akarudia tena kauli yake: “Sioni wa kumlaumu na matokeo kama haya ni sehemu ya mpira, kikubwa ni kufanyia marekebisho maeneo ambayo yanaonekana kuwa na shida hasa washambuliaji wangu, ambao kwa namna moja ama nyingine wameonekana kujisahau.”

Najua ni mapema sana kuizungumzia Kagera kwa kuwa ligi ndio kwanza mbichi, lakini Waswahili wanasema dalili ya mvua siku zote ni mawingu na mchelea mwana kulia hulia yeye, je, tunajua sababu ya Kagera kusuasua au Kagera yenyewe imeshakaa kujiuliza hili?

Awali kabla ya kuanza kwa ligi, Yanga ilionyesha nia ya kumtaka Mexime, aende akasaidiane na kocha mkuu wa timu hiyo, Mzambia George Lwandamina, lakini uongozi wa Kagera ulizungumza na kocha wake akabaki.

Matokeo haya yamenifanya nijiulize, Kagera wanatimiza anayotaka Mexime au nao walijiandaa kwa matokeo haya, kwani Kagera ya msimu huu haina tofauti na ya msimu uliopita kwani haina mabadiliko makubwa kusema waanze ligi hivi.

Hayo ni machache niliyoweza kujiuliza kuhusu Kagera ambao kwanza wanaonekana na ukuta mzuri uliokua na watu wazuri kama Mohamed Fakhi, Juma Ramadhan, Adeyuni Ahmed na Mwaita Ngereza, bila kumsahau kipa mzoefu Kaseja.

Kagera inajivunia washambuliaji na viungo wenye uzoefu kama George Kavilla, Edward Christopher, Ame Ally, Ally Nassor ‘Ufudu’, Peter Mwalyanzi, Themi Felix, Venance Ludovic na wengine ambao kwa namna moja ama nyingine wasingekubali kupata matokeo haya.

Ukiangalia wachezaji hawa, wote walikuwapo na Kagera msimu uliopita na mabadiliko waliyofanya ni madogo, lakini kubwa walimuuza Mbaraka Yusuph ambaye aling’ara msimu uliopita na kumchukua Juma Nyoso.

Sitaki kuamini kama kuondoka kwa Yusuph kumeathiri timu maana waliuza mshambuliaji na kumnunua beki.

Mchezo wa mpira ni dakika 90 huenda wamekumbwa na upepo mbaya, ambao naamini baadaye utabadili mwelekeo na kuwaacha kurudi katika uhalisia wao.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU