HUU NI MSIMU MGUMU KWA YANGA

HUU NI MSIMU MGUMU KWA YANGA

2402
0
KUSHIRIKI

 MZEE WA KUPASUA, kapssmo@gmail.com 0716985381

NA ONESMO KAPINGA

Yanga hawakuanza msimu vizuri baada ya kufungwa kwa changamoto ya mikwaju ya penalti 5-4- na Simba, katika mchezo wa Ngao ya Jamii uliochezwa Agosti 23, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

 Timu hiyo ilishindwa kupata ushindi katika dakika 90 za kawaida na kuwafanya Simba kuibuka na ushindi kwa mikwaju ya penalti.

 Ni tofauti ya misimu iliyopita, Yanga walikuwa wanaanzia kubeba Ngao ya Jamii na ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara na makombe mengine.

 Lakini msimu huu wa Ligi Kuu Bara, Yanga walianza kwa kupata sare ya kufungana bao 1-1 na Lipuli katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Yanga walishinda bao 1-0 dhidi ya Njombe Mji katika mchezo uliofuata uliochezwa kwenye Uwanja wa Sabasaba mjini Njombe, lakini walitoka sare ya kufungana bao 1-1 na Majimaji ya Songea kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea.

Baada ya matokeo hayo, Yanga walipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Ndanda katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Uhuru, kabla ya kutoka sare ya kutofungana na Mtibwa Sugar.

 Rekodi ya Yanga inaonesha katika michezo mitatu waliyocheza kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Uhuru, wameambulia pointi tano, badala ya tisa kama wangeshinda michezo yote.

 Kwa hesabu za haraka haraka, unaweza kuangalia matokeo na kusema kwamba, msimu huu wa Ligi Kuu Bara umekuwa ni mgumu kwa Yanga.

 Ukiangalia idadi ya mabao wanayofunga, utagundua Yanga hawako vizuri, kwani msimu uliopita walikuwa wanafunga zaidi ya mabao mawili katika mchezo mmoja, lakini msimu huo wao ni mwendo wa bao 1-0 wanashinda au sare.

 Kutokana na mwenendo wao katika ligi hiyo, Yanga wanatakiwa kufanya kazi ya ziada kuweza kutetea ubingwa wao, kwani  wakitaendelea kupata matokeo hayo, itakuwa ngumu kwao kutimiza malengo yao.

 Pamoja na kuonekana ligi bado mbichi, lakini kwa bingwa mtetezi kukosa pointi nne katika uwanja wao wa nyumbani ni ishara  mbaya kwao.

 Yanga wanakuwa katika wakati mgumu wa kupata matokeo mazuri huku wakiwa na kocha, George Lwandamina ambaye ana uwezo mkubwa wa kufundisha soka.

 Lwandamina alitua Yanga katika msimu uliopita, baada ya uongozi wa klabu hiyo kuridhishwa na uwezo wake, akiwa anaifundisha ZESCO ya Zambia iliyofika nusu fainali kwenye michuano ya Afrika ya Ligi ya Mabingwa.

 Hiyo ilikuwa ni sababu kubwa kwa Yanga kumwajiri Lwandamina walioamini angeweza kuifikisha timu yao mbali kwenye michuano ya kimataifa, baada ya kocha aliyemtangulia Hans van der Pluijm kuishia robo fainali ya Kombe la Shirikisho barani Afrika.

 Lwandamina anaonekana ni kocha wa kawaida baada ya kutua Yanga, hali inayowafanya mashabiki wa timu hiyo, waanze kumkumbuka Pluijm aliyeondoka klabuni hapo akiwa ameacha rekodi nzuri.

 Rekodi ya Pluijm inaonekana bado imesimama Yanga kutokana na matokeo ya timu hiyo katika msimu huu alioanza nao Lwandamina. 

 Kutokana na matokeo hayo, Mzee wa Kupasua anabaki kujiuliza maswali mengi kuliko majibu na wakati mwingine kwenda hadi Zambia kutaka kujua uwezo wa Lwandamina.

 Ni kweli uwezo wa kufundisha wa Lwandamina ni huo tunaoushuhudia Yanga ikishindwa kupata ushindi katika michezo miwili ya nyumbani? Au kuna kitu nyuma ya matokeo hayo?

 Lwandamina yule tunayemjua wa ZESCO ni huyo tunayemshuhudia, Yanga ikiendelea kupata sare mbili katika michezo yake ya nyumbani?

  Tutakutana Jumatatu ijayo

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU