FIKRA HIZI ZITAKUFANYA UDUMU KATIKA UHUSIANO WAKO

FIKRA HIZI ZITAKUFANYA UDUMU KATIKA UHUSIANO WAKO

390
0
KUSHIRIKI

Na RAMADHANI MASENGA

KABLA ya kitu chochote kufanyika ni lazima kwanza kitokee katika fikra. Mfano ukitaka kuoa ni lazima kwanza wazo la kuoa lijae kichwani mwako na baada ya hapo ndipo hatua nyingine zitafuata.

Hiyo iko kwa kila kitu. Fikra ndiyo mzizi wa mengi kutokea na kutotokea. Unataka kudumu katika uhusiano wako? Una fikra zipi juu ya mwenzako? Una fikra zipi katika uhusiano wako?

Ili mahusiano yoyote yaweze kudumu ni lazima kila mmoja awe na muono wa mbali na mahusiano husika.

Ni ngumu mno kwa ndoa ama mahusiano kudumu kama kila mmoja aliye katika uhusiano ana amini mahusiano hayo ni kitu cha muda mfupi.

Unaamini nini katika mahusiano yako?  Unaamini mwenzako ni mwafaka ama uko naye kwa kuwa inabidi tu uwe na mtu?

Hakuna mkamilifu katika maisha. Aliye bora katika kitu A anaweza kuwa dhaifu katika kitu B, maisha ndiyo yalivyo.

Kama hauna amani na mwenzako kwa sababu ana udhaifu mahali fulani jua unataka kujiingiza katika mahangaiko ya bure maisha yako.

Hakuna aliye bora kwa kila kitu katika uhusiano na maisha. Unachotakiwa ni kuwa na mtu mwenye kuwa na vingi vya kukufanya ujivunie kuliko vya kukufanya uumie na kukereka.

Ili mahusiano yako yaweze kufika mbali inabidi uwe na fikra safi juu ya mwenzako na juu ya mahusiano yako. Inabidi uwaze kuwa mwenzako ndio mwisho wa safari yako ya kutafuta mtu sahihi wa maisha yako.

Fikra za namna hii zitakuepusha kukimbilia kuwaza kuachana pindi mnapokoseana na badala yake mtakuwa makini katika kutafuta suluhu ya matatizo yenu.

Kutakuwa na amani na raha zaidi katika mahusiano yenu kama utamfikiria mwenzako kama kikomo cha safari yako ya kusaka mwenza.

Kwa maana katika fikra hizi ndipo utajifunza kuvumilia na kuzikubali baadhi ya tabia zake huku pia ukitafuta njia bora na mwafaka ya kumbadilisha kwa zile tabia zinazokupa chukizo katika maisha yako.

Mbali na mambo mengine ila mahusiano bora yanajengwa kwa namna unavyomwona mwenzako na kumtafsiri.

Kama ukimwona mwenzako wakuzugia, hata kama ana vitu bora ila huwezi kuviangalia kwa namna halisi kwa maana akili yako bado itakuwa busy ikisaka mtu mwingine.

Itakupelekea hata mwenzako huyu akifanya kosa la kibinadamu wewe utakimbilia kuamini hakufai kwa sababu katika akili yako humwoni kuwa mtu sahihi katika maisha yako.

Watu wanaokoseana sana na kusameheana ni wale wanaoamini wenzao ni bora na wanafaa sana katika maisha yao.

Fikra hizi huwa ndicho chanzo cha utulivu wao hata katika kipindi cha matatizo makubwa. Unawaza nini juu ya mahusiano yako? Unamuwaza vipi mpenzi wako?

Fikra huwa chanzo cha kubomoa na kujenga katika uhusiano. Kataa kuwa na fikra za kubomoa uhusiano wako. Kuwa na fikra mwafaka kwa mwenzako na kwa uhusiano wako ili upamoja wenu uweze kufika mbali zaidi.

Unaletewa maneno ya ovyo juu ya mwenzako? Unamwonaje mwenzako? Usikae ukaamini maneno ya watu ovyo. Kama kuna kitu wanasema kuhusu mwenzako na unahisi yana ukweli, fanya uchunguzi wako mapema.

Usiache maneno ya ovyo kujaa katika kichwa chako bila kuyafanyia kazi. Ikiwa utaacha fitina za watu kujaa kwako, ikiwa utaacha maneno ya ovyo kukutawala, utajikuta unaanza kumwangalia mwenzako katika mtazamo hasi kitu kitakachokupelekea hata umwone hana maana na hafai katika maisha yako.

Nakukumbusha, mahusiano yako ni suala linalokuhusu wewe na maisha yako. Amani na raha ya mahusiano yako hapati mtu mwingine ila wewe. Na pia kama ukiwa na huzuni katika uhusiano wako, maumivu utapata wewe na si watu wengine.

Kuwa makini kuazima sikio lako kwa watu wanaokwambia kuhusu mwandani wako. Ndiyo, ni vizuri kusikia watu wanasema nini.

Ila unajua kwanini wanakwambia? Acha kukubali kila unachoambiwa. Fanya uchunguzi mwenyewe. Suala linalokuhusu wewe inabidi uliamue wewe baada ya kupata ushauri wa wataalamu ama watu makini.

Thamani ya mahusiano yako iko kwako na kwa mwenzako. Mwenzako atakavyokuona katika akili na hisia zake ndivyo atakavyokutendea.

Akikuona wa maana na wa thamani basi atakutendea wema na mambo mazuri. Ila pia kama katika akili yake anakuona mtu wa ajabu, upo upo tu.

Ukiwepo sawa na usipokuwapo sawa. Basi atakutendea kiovyo ovyo hivyo hivyo. Fikra zako zinaweza kukuachanisha na mpenzi wako kama usipokuwa makini.

Ili mambo yasifikie huko jitathmini kwanini unamuwazia mambo ya ovyo mwenzako? Kwanini unahisi hakufai? Je, ni kwa sababu ya maneno unayosikia juu yake? Je, ni kwa sababu ya matendo yake usiyoyaelewa?

Kwa kila ambacho hukielewi, kaa naye na jadili naye kwa kina. Kuna wengi wameachana na wapenzi wao kwa kusukumwa na fikra zao zilizokuwa zikiamini wenzao walikuwa watu wabaya kumbe sio.

Tatizo la fikra mbaya kadiri unavyoziacha bila kuzitafutia usahihi mapema ndivyo zinavyozidi kukusanyika na kuwa nyingi zaidi.

Fikra za ovyo mfano wake ni kama moto katika nyasi kavu. Moto katika nyasi kavu inabidi ushughulikiwe mapema maana bila kufanya hivyo utaenea eneo kubwa hata kuwa vigumu mno kuuzima tena.

Kuwa makini na fikra pamoja na hisia mbaya juu ya mwenzako. Mahusiano yako yatakuwa na amani na furaha ikiwa utamwona mwenzako katika mtazamo chanya.

Ikiwa mwenzako unamwona katika mtazamo hasi hata matendo yake mazuri kwako utayaona usanii mtupu. Kuwa makini.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU