HAO NAPOLI NI NOMA SERIE A

HAO NAPOLI NI NOMA SERIE A

331
0
KUSHIRIKI

NAPLES, Italia

KOCHA Maurizio Sarri, anaonekana kufanya kazi nzuri sana ndani ya kikosi chake cha Napoli kwa sasa, akiwa amewaimarisha mno vijana wake hasa kwenye mashambulizi.

Hivi sasa ndiyo timu inayoongoza kwa kushambulia nchini Italia na ni moja ya klabu zinazoongoza kwa kuwa na mashambulizi makali duniani.

Ni kwa jinsi gani wanavyofanya mashambulizi yao? Twende sawa upate madini.

Mfumo wao wanaoutumia ni 4-3-3 ambapo kikosi chao bora cha kwanza msimu huu kinawajumuisha mlinda mlango, Pepe Reina, mabeki ni Elseid Hysaj na Faouzi Ghoulam, ambao wanatembea kwenye mashavu ya kulia na kushoto, halafu Raul Albiol na Khalidou Koulibaly, wanamaliza kati.

Viungo watatu wanakuwa ni Jorginho, Allan na Marek Hamsik, mbele pale sasa wanamaliza Lorenzo Insigne, Dries Mertens na winga wa zamani wa Real Madrid, Jose Callejon.

Jinsi wanavyocheza ni kwa kufanya ‘pressing’ ya nguvu na hilo linawafanya wawe na uwezo wa kupokonya mipira mara nyingi na kushambulia sana.

Napoli wamekuwa wakicheza soka la kasi na pasi zao ni za mbele kwa mbele ili kufika langoni mwa mpinzani mapema na kufunga mabao ya kutosha.

Jorginho, ambaye kimsingi huanza kama kiungo mkabaji, hushuka chini zaidi kuwasaidia mabeki katika suala la kuunda mashambulizi kwa tempo ya kawaida.

Kwa kuwa wachezaji wa timu pinzani wana shinda na mpira, Jorginho na wenzake (walinzi) hujikuta kama wanazidiwa, hivyo Hamsik na Allan nao huungana nao kusaidia kulinda umiliki wa mpira na kuwavuta zaidi maadui kutoka kwenye eneo lao.

Hamsik na Allan hucheza kama viungo wachezeshaji ambao hujipanga karibu na wale wa ulinzi na washambuliaji, kujaribu kuhakikisha timu inakuwa na uhakika wa kuumiliki mchezo, kutengeneza nafasi na kufunga mabao.

Ili kuzivunjavunja safu za ulinzi za timu pinzani na kwa sababu Napoli hucheza pasi za fasta fasta, wanawategemea sana akina Mertens, Insigne, Callejon na Hamsik katika kukimbia kwenye njia ili kuwapa nafasi wenzao wawapenyezee pasi za kutanguliza.

Mtu muhimu katika suala la kukimbia kwenye hizo njia ni Mertens ambaye hucheza kama mshambuliaji wao wa kati, mara nyingine hukimbia kupitia kati au pembeni.

Kwa kawaida, kama Mertens akikimbia kupitia nje ya eneo lake mahsusi basi lazima ataenda kushoto kwani kiasili yeye ni winga wa upande huo halafu Insigne ambaye naye ni winga wa upande huo, anakuwa anaingia sana ndani na kuacha uwazi.

Kila Mertens na Insigne, wanapobadilishana hizo nafasi wakati wa mchezo, mabeki hujikuta njia panda wamkabe yupi, wamuache nani na hapo ndipo mabao yanapofungwa.

Kinachomfanya Insigne aingie sana ndani kutokea kushoto ni kwa sababu mguu wake wa kulia ndio wenye nguvu, halafu kule kulia anakocheza Callejon, yeye mara nyingi hutulia zaidi pembeni kwa ajili ya kumimina krosi kutokana na mguu wake wenye nguvu kuwa ni wa kulia.

Krosi hizo, zimekuwa zikitumika sana na Insigne, Mertens pamoja na Hamsik. Lakini, katika mfumo huo wa mashambulizi, Insigne na Callejon, wameonesha uwezo mkubwa msimu huu wa kukimbia kwenye njia na kufunga mabao makali baada ya kupenyezewa pasi murua.

Hamsik yeye hukimbia kwenye njia za upande wa kushoto, kutokana na nafasi yake kuwa ni ‘kiungo wa kati kushoto’. Mara nyingi mabeki hushindwa kumgundua haraka kwani huanzia mbali.

Pia, Napoli wamekuwa wakifunga sana mabao kutokana na ubunifu wa Mertens kurudi nyuma ili mabeki wamfuate na hivyo kuwatengenezea wenzake njia za kukimbia kwa ajili ya kwenda kufunga kutokana na kucheza sana kama namba 9 feki.

Hatimaye inakuja kugundulika kuwa Napoli inafunga sana msimu huu kutokana na washambuliaji wao watatu wenye kasi wenye uwezo wa kuzunguka mno eneo la mwisho.

Upande wa kushoto wa Napoli unatajwa kuwa ndio hatari zaidi, kuna Insigne kama winga wa kushoto, halafu Hamsik naye anatokea upande huo huo, beki wa kushoto, Faouzi Ghoulam, huwasaidia tu. Upande wa kulia unamilikiwa sana na Callejon.

 

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU