KWA TAKWIMU HIZI, GUARDIOLA, MOURINHO HAWAMWACHI MTU EPL

KWA TAKWIMU HIZI, GUARDIOLA, MOURINHO HAWAMWACHI MTU EPL

693
0
KUSHIRIKI

MANCHESTER, England

MAKOCHA hao ndio wanaozungumziwa sana kwa sasa kwenye mbio za kuwania taji la Ligi Kuu England, kwani timu zao zinakabana koo kileleni zikilingana pointi. Pep Guardiola na Man City yake wanaongoza ligi kwa bao moja tu la kufunga.

Timu hizo za jijini Manchester zimeiacha Tottenham inayoshika nafasi ya tatu kwa pointi tano.

Jose Mourinho wa Man United bado hajakutana na timu kubwa huku Man City wakiwa wamecheza na Chelsea pekee na kuitungua bao 1-0.

“Nilisema mwanzoni kabisa mwa msimu kwamba ubingwa utatua jijini Manchester na tayari hilo limeanza kuonekana,” alisema beki wa zamani wa Man United, ambaye kwa sasa ni mchambuzi wa soka wa kituo cha televisheni cha Sky Sports, Gary Neville.

Lakini je, licha ya kupewa nafasi kubwa kwenye safari ya kuivua Chelsea ubingwa wa msimu uliopita, takwimu za vikosi vya Guardiola na Mourinho zikoje zikiwa zimeshachezwa mechi saba tangu kuanza kwa msimu huu?

Walinda mlango

Baada ya mechi saba, makipa wa timu zote mbili wameruhusu mabao mawili kila mmoja. Mchezo pekee ambao David de Gea wa Mourinho alifungwa mara mbili ni ule wa sare ya mabao 2-2 dhidi ya Stoke.

Kipa mpya wa Man City, Ederson, ameuanza vizuri msimu wake wa kwanza England, ambapo ameokoa asilimia 85 ya hatari zilizofika langoni mwake.

Mabeki

Katika eneo la beki wa kati, Mourinho amewaamini Eric Bailly na Phil Jones huku Guardiola akiwapa kazi hiyo John Stones na Nicolas Otamendi.

Eneo la beki wa pembeni, Guardiola alitumia pauni milioni 126 wakati wa majira ya kiangazi aliwanunua Kyle Walker, Benjamin Mendy na Danilo.

Ni kama kamari yake hiyo imelipa kwani mabeki wa pembeni wameshatoa asisti nne na kutengeneza nafasi 13 zilizozaa mabao.

Viungo

Safu ya kiungo ya Man United imeonekana kuwa bora zaidi kuliko ya Man United. Ikiwa chini ya Nemanja Matic na Marouane Fellaini, wamekuwa na wastani mzuri wa kuhusika katika mabao na kutibua mashambulizi.

Fellaini peke yake ana mabao matatu katika mechi sita na amekuwa akiaminiwa kwa kiasi kikubwa tangu Paul Pogba alipoumia.

Viungo wa Man City; David Silva na Kevin De Bruyne, wamechangia kupatikana kwa mabao mawili pekee hadi sasa.

Washambuliaji

Timu zote zina wastani wa kufunga mabao matatu katika kila mchezo. Chini ya Sergio Aguero, Man City ina wastani mkubwa zaidi wa kutengeneza na kutumia nafasi za mabao.

Raheem Sterling amefunga mabao matano, Gabriel Jesus, ametupia manne na Mjerumani Leroy Sane, ana matatu.

Hata hivyo, straika wa Man United, Romelu Lukaku, ndiye anayeongoza orodha ya wapachikaji mabao Ligi Kuu England, akiwa amezifumania nyavu mara saba katika mashuti yake 15 yaliyolenga lango.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU