NI WAKATI WA KUTUPIA MACHO UDHAMINI FDL

NI WAKATI WA KUTUPIA MACHO UDHAMINI FDL

352
0
KUSHIRIKI

NA ZAITUNI KIBWANA

LIGI Daraja la Kwanza Tanzania Bara (FDL) ilianza Septemba 16, mwaka huu, ikishirikisha timu 24 ambazo zinapambana kuwania nafasi ya tatu za juu ili kupanda kucheza Ligi Kuu Bara  msimu wa 2018/19.

Timu zinazoshiriki ligi hiyo ni African Lyon, Ashanti United, Friends Rangers, Mshikamano FC, JKT Ruvu, Kiluvya United, Mgambo JKT na Mvuvumwa ambao zimepangwa Kundi A.

Kundi B linaundwa na timu za Coastal Union, JKT Mlale, KMC, Mbeya Kwanza, Mufindi United, Polisi Dar, Polisi Morogoro na Mawezi Market, huku Kundi C likiwa na timu za Alliance School, Pamba, Toto Africans, Rihno Rangers, Polisi Mara, Polisi Dodoma, Transit Camp na JKT Orjoro.

Ligi hii ina mashabiki wengi kwa kuwa ndio inayozalisha wachezaji wengi chipukizi ambao baadaye hung’ara katika ligi kuu na michuano mengine.

Mwaka huu michuano ya FDL ilianza bila kuwa na hamasa ya wadhamini tofauti na msimu uliomalizika, kwani chini ya Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi, ligi hiyo ilikuwa na wadhamini wawili ambao baadaye walijitoa kwa madai ya tuhuma za upangaji matokeo.

FDL ilikuwa na udhamini kutoka Kampuni ya Star Times na Sahara Media, lakini ulisitishwa kutokana na kuwepo kwa tuhuma za upangaji matokeo msimu uliopita.

Kwa uhalisia timu zinazoshiriki Ligi Daraja la Kwanza hazina uwezo wa kifedha  hivyo zinakumbana na changamoto nyingi ambazo zinachangia michuano hiyo kukosa mvuto.

Tunafahamu kuwa ligi kuu ina wadhamini wake ambao ni Kampuni ya Mawasiliano yaVodacom, Azam Media na pia mashindano ya vijana chini ya miaka 20 yanadhaminiwa na Uhai.

Pia mashindano ya vijana wenye umri chini ya miaka 17, wadhamini wake ni  Airtel na yale ya vijana wa umri chini ya miaka 15 ya Copa Coca Cola yanadhaminiwa na Kampuni ya  Coca Cola.

Kutokana na hali hiyo, ni jambo la kujiuliza inawezekana vipi TFF ikashindwa kutafuta wadhamini kwa ajili ya FDL, kwani mashindano haya ni muhimu kwa kuwa ndio yanatoa timu tatu zinazotakiwa kucheza ligi kuu yenye ushindani kila mwaka.

TFF wanatakiwa kutambua kuwa FDL ni ligi ya pili kwa ukubwa nchini baada ya Ligi Kuu, hivyo ni lazima itafutiwe  udhamini unaoeleweka.

Shirikisho halitakiwi kukwepa  jukumu la kutafuta udhamini wa ligi hiyo kama kweli linataka kuhakikisha mashindano yanakuwa na msisimko na kukuza soka la Tanzania.

Hakika ukosefu wa udhamini FDL ni kikwazo kikubwa cha maendeleo ya mpira wetu kutokana na kukosekana kwa ubora na ushindani wa kweli ndani ya ligi hiyo.

TFF inatakiwa kulisimamia hili kwa sababu jukumu la kukuza hapa nchini lipo chini yake, lakini pia wadau wanapaswa kushauri kampuni mbalimbali kujitokeza kuidhamini FDL, kwani hiyo ni fursa nzuri kwao  kujitangaza kupitia mashindano hayo.

Tunaamini kwamba TFF, Bodi ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara (TPL) na wadhamini ndio watakaoweza kuifanya ligi ya FDL  kuwa na msisimko, kwani timu shiriki zinakuwa zimejiandaa vyema.

Kama TFF walishaanza mchakato wa kutafuta wadhamini basi waendelee ili timu ziweze kukabiliana  na changamoto zilizopo na kuipa ubora ligi hiyo na kuimarika zaidi.

Changamoto zinazojitokeza FDL zinaongeza ugumu na tabu kwa baadhi ya timu shiriki ambazo zipo katika hali mbaya kiuchumi, kwani zinashindwa kulipa wachezaji mishahara, kukosa pesa ya chakula, malazi na usafiri pindi zinapokuwa zikijiandaa na michezo yao.

Tumeshuhudia timu nyingi zikishindwa kujiendesha zenyewe, jambo ambalo linawafanya wachezaji kukata tamaa na hata kutocheza vizuri.

Tatizo la hali mbaya ya uchumi limekuwa janga kubwa kwa baadhi ya timu zinazoshiriki ligi hiyo, hivyo huu ni wakati mwafaka wa TFF kukaa chini na kupanga mikakati ya kupata wadhamini.

TFF inapaswa kujiangalia upya ili kuona ni hatua gani watachukua ili kuwashawishi wadhamini kuingia ili kupata fursa ya kujitangaza.

Kama changamoto zilizopo sasa zitapatiwa ufumbuzi na kuondoa vikwazo vya maendeleo ya soka, ni wazi kwamba tutaweza kusonga mbele na kuingia kwenye soka la ushindani.

 

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU