MAMBO 10 USIYOYAJUA KUHUSU ANCELOTTI

MAMBO 10 USIYOYAJUA KUHUSU ANCELOTTI

428
0
KUSHIRIKI

 

MUNICH, Ujerumani

KOCHA Carlo Ancelotti alitimuliwa kwenye benchi la ufundi la Bayern Munich siku chache zilizopita baada ya  kikosi chake kuchapwa mabao 3-0 na PSG katika mtanange wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Itakumbukwa kuwa PSG pia imewahi kunolewa na Mwitalia huyo, hivyo ni kama wamemfukuzisha kazi kocha wao wa zamani.

Licha ya klabu kadhaa zikiwamo za Ligi Kuu England kuonesha nia ya kumchukua, mkufunzi huyo aliyewahi kuzinoa Real Madrid na Chelsea, ameelezwa kuwa atapumzika soka kwa kipindi kisichopungua miezi 10.

Kuhusu kocha huyo mwenye umri wa miaka 58, haya ni mambo 10 ambayo huenda si kila shabiki wa soka anayajua.

  1. Mpaka anastaafu soka la uwanjani akiwa kiungo, alikuwa ameifungia bao moja pekee timu yake ya Taifa ya Italia ambayo aliichezea mechi 26. Bao hilo alilifunga mwaka 1980 katika mchezo dhidi ya Uholanzi.
  2. Katika klabu ya Roma, Ancelotti aliwahi kunolewa na kocha mkongwe, Sven-Goran Eriksson na ndiye aliyemkabidhi kitambaa cha unahodha katika msimu wa 1985–86. Roma walimaliza ligi msimu huo wakiwa nafasi ya pili, nyuma ya mabingwa Juventus.
  3. Ancelotti ni kocha pekee raia wa Italia ambaye amewahi kushinda tuzo ya Kocha Bora wa Mwaka Ligi Kuu Ufaransa ‘Ligue 1’. Alipewa heshima hiyo katika msimu wa 2012-13 akiwa na PSG.
  4. Kocha huyo ni mtumiaji mzuri wa sigara na mara kwa mara amewahi kunaswa akipuliza. Kuna kipindi uongozi wa Bayern Munich ulimtaka kuachana na tabia hiyo. Mara kadhaa amekuwa akisisitiza kuwa anapigana kuachana na utumizi wa sigara.
  5. Kocha huyo amepoteza mchezo mmoja tu kati ya minne ambayo ameingia fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Mtanange huo ni ule aliokuwa na Milan iliyovaana na Liverpool mwaka 2005. Mpaka timu hizo zinakwenda mapumziko, Milan walikuwa mbele kwa mabao 3-0 lakini baadaye walifungwa kwa mikwaju ya penalti.
  6. Mmoja kati ya wasaidizi wake katika benchi la ufundi la Bayern alikuwa mtoto wake wa kiume, Davide Ancelotti, ambaye alianza kucheza soka kwenye academy ya AC Milan. Wengine ni Paul Clement na Hermann Gerland. Ancelotti alimteua mwanawe huyo mwenye umri wa miaka 28 mwaka jana.
  7. Mwaka 2013, akiwa kocha wa Real Madrid, Ancelotti alimwajiri mchumba wa binti yake, Katia, Mino Fulco, kuwa mtaalamu wa vyakula kwa wachezaji klabuni hapo. Hata hivyo, haikuwa rahisi kwa Ancelotti kumpa ‘shavu’ mkwewe huyo kwani Madrid walisema wana daktari wao.
  8. 8. Ancelotti ni kocha pekee mwenye rekodi ya kushinda mataji matatu ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na kufika fainali nne za michuano hiyo. Pia, Muitalia huyo ameshinda mara mbili fainali za Kombe la Dunia kwa ngazi ya klabu akiwa na AC Milan na Real Madrid.
  9. Akiwa mkuu wa benchi la ufundi, Ancelotti ameshinda vikombe katika ligi zote tano barani Ulaya. Ameweza kunyakua mataji ya Ligi Kuu England, Serie A, Ligue 1, La Liga na Bundesliga.
  10. Ancelotti ni miongoni mwa watu saba pekee duniani kubeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya wakiwa wachezaji na kisha wakiwa makocha. Wengine ni Miguel Munoz, Pep Guardiola, Giovanni Trapattoni, Johan Cruyff, Frank Rijkaard na Zinedine Zidane.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU