WAKALI HAWA HUENDA WAKAKOSEKANA URUSI MWAKANI

WAKALI HAWA HUENDA WAKAKOSEKANA URUSI MWAKANI

713
0
KUSHIRIKI

AMSTERDAM, Uholanzi

MECHI za kufuzu kushiriki Kombe la Dunia kwa mataifa kutoka Ulaya ndio zinakaribia kumalizika, huku nyota kadhaa wale bora wa Ulaya wakiumiza kichwa kuhusu hatima ya mataifa yao.

Hata hivyo, kuna baadhi ya mataifa makubwa ya Ulaya huenda yakakosa tiketi ya kushiriki michuano hiyo, kitu kitakachopeleka mastaa hawa kukosekana.

 

Arjen Robben

Kabla ya mechi za jana, Uholanzi ilikuwa chini ya Ufaransa na Sweden kwenye kundi lao na kuna hatari taifa hilo la Robben likabaki nyumbani kama walivyokosa kushiriki Euro 2016.

Je, itakuwaje kwa mashabiki wa winga huyo, watajisikiaje kuona staa huyo akikosekana kwenye michuano hiyo mikubwa.

Gareth Bale

Winga huyo hataweza kuisaidia timu yake ya Wales katika harakati za kuisaka tiketi ya Kombe la Dunia kutokana na majeraha na ukweli ni kwamba, hatima yao inaning’inia kwenye uzi kuelekea mechi yao ya kesho dhidi ya Ireland.

Bale anawategemea sana wenzake wapambane ili na yeye akaoneshe makeke Urusi ifikapo mwakani.

Modric, Kovacic na Rakitic

Nyota hao watatu wanaokimbiza LaLiga huenda wakabaki nyumbani kutazama michuano hiyo kwenye TV, kutokana na hali tete inayowakabili Croatia baada ya kushindwa kuwafunga Finland wikiendi iliyopita na sasa matumaini yao ni kuona Iceland ikifungwa na Kosovo ili wafuzu moja kwa moja.

Gianluigi Buffon

Mkongwe huyo ni staa mwingine ambaye huenda tukasikitika kutomwona kule Urusi, kwani timu yake ya Italia itabidi icheze mechi za mchujo ili waweze kufuzu.

Dolberg na Eriksen

Timu nyingine itakayocheza mechi za mchujo ni Denmark, kitu ambacho kinamaanisha mashabiki wa soka Urusi huenda wakakosa burudani ya ufundi wa akina Kasper Dolberg na Christian Eriksen.

Hamsik na Oblak

Kundi F lina mechi kali ambapo Scotland, Slovakia na Slovenia wana vita ya kuwania tiketi ya kucheza mechi za mchujo, sasa hapo ndipo kuna hatari ya kuwakosa hata wakali, Marek Hamsik wa Napoli na Jan Oblak, mlinda mlango mahiri wa Atletico Madrid.

Pjanic na Dzeko

Bosnia & Herzegovina waliwashangaza wengi baada ya kufuzu michuano ya Kombe la Dunia 2010, lakini kipindi hiki vyuma vimekaza na sasa mastaa wa timu hiyo, Miralem Pjanic, Edin Dzeko huenda wakacheza mechi za mchujo iwapo watamaliza nafasi ya pili kwenye kundi H.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU