MWOKOZI: MATUMAINI YALIANZA KUFIFIA, ILA AKAIBUKA RONALDO NA KUWAOKOA

MWOKOZI: MATUMAINI YALIANZA KUFIFIA, ILA AKAIBUKA RONALDO NA KUWAOKOA

2031
0
KUSHIRIKI

ANDORRA LA VELLA, Andorra

LILIKUWA ni bao la nahodha na mshambuliaji mwenye rekodi lukuki, Cristiano Ronaldo, ambaye alitokea benchi lililozidisha matumaini kwa taifa la Ureno kuelekea michuano ya Kombe la Dunia mwakani, ambapo aliihakikishia timu yake hiyo ushindi muhimu wa mabao 2-0 ugenini dhidi ya Andorra.

Ureno iliondoka ugenini na alama zote tatu muhimu juzi Jumamosi, ambapo bao hilo la Ronaldo dakika ya 63 ya mchezo liliamsha morali ya wenzake na kuufanya usiku wa Jumamosi kuwa wa furaha kwa staa huyo wa Real Madrid.

Kwa muda mwingi wa mtanange huo, Ureno iliumiza kichwa mno kuipangua ngome ya Andorra, lakini kitendo cha kocha kumuinua supastaa huyo kutoka benchi na kwenda kufunga bao la kwanza kabla ya straika Andre Silva kupachika la pili, kitaufanya mchezo wa mwisho baina ya Ureno na vinara wa kundi B, Uswisi, utakaochezwa mjini Lisbon kesho, uwe mkali na wa kusisimua.

Mechi hiyo itaamua sasa nani ataongoza kundi hilo na kukata tiketi ya moja kwa moja kuelekea Urusi na yupi atacheza mechi ya mchujo.

Uswisi ambao waliitandika Hungary mabao 5-2 juzi, wanaongoza kundi hilo wakiwa na alama 27 walizozikusanya kutoka kwenye michezo tisa. Iwapo watapata sare dhidi ya Ureno ambao wana alama 24, watamaliza ratiba wakiwa kileleni.

Kabla ya mchezo huo, Ronaldo alikuwa akitajwa kama mmoja wa mastaa wakubwa barani Ulaya wenye hatari ya kukosekana kwenye michuano hiyo ya Kombe la Dunia kufuatia mwenendo wa kusuasua wa mataifa hayo.

Kwa kipindi kirefu mataifa mengine makubwa ya Amerika Kusini ndiyo yamekuwa habari ya mjini, wengi wakiwa na hofu ya kuwaona mastaa wakubwa wa soka katika mataifa hayo wakikosa nafasi ya kwenda Urusi mwakani.

Lionel Messi na Alexis Sanchez ndio mastaa wa huko ambao mataifa yao yako hatarini kukosa nafasi ya kushiriki Kombe la Dunia, lakini pia hata Ulaya kuna mastaa wakubwa tu ambao nao huenda tukawakosa.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU