SINGIDA UNITED KUSAKA POINTI TISA KWA JASHO

SINGIDA UNITED KUSAKA POINTI TISA KWA JASHO

1006
0
KUSHIRIKI

NA SALMA MPELI

SINGIDA United inayoshika nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, imeweka mikakati ya kupata pointi tisa kwa michezo mitatu itakayochezwa nje ya uwanja wao wa nyumbani.

Uongozi wa timu hiyo inayofundishwa na Hans van der Pluijm, umedhamiria kuzipata pointi hizo kwa kuvuja jasho wakati watakapokuwa wakicheza ugenini.

Singida United watatoka nyumbani kwa kucheza na Ruvu Shooting, katika mchezo utakaochezwa Jumamosi Uwanja wa Mabatini mkoani Pwani, baadaye watakwenda kucheza na Ndanda, Mtwara kabla ya kuwavaa Mtibwa Sugar, Manungu Morogoro.

Mkurugenzi wa Singida United, Festo Sanga, alisema timu inaendelea na maandalizi yao kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma, kujiandaa na michezo hiyo.

Alisema mipango ya kocha wao ni kuhakikisha wanajikusanyia pointi tisa katika mechi zote tatu kabla ya kuwavaa Yanga Novemba 4, mwaka huu, katika uwanja wao mpya wa Namfua, Singida.

“Timu ipo kwenye hali nzuri, tunahitaji kupata pointi tatu muhimu kwenye mechi ijayo, lakini pia kocha amepanga kuhakikisha timu inapata pointi tisa, katika mechi zake tatu nje ya Uwanja wa Jamhuri ambapo ni dhidi ya Ruvu, Ndanda na Mtibwa Sugar,” alisema Sanga.

Aliongeza kuwa baada ya hapo watarudi kwenye makao yao makuu Singida kujiandaa na mechi yao dhidi ya Yanga, mchezo huo utakuwa wa kwanza kwenye uwanja huo mpya tangu ufanyiwe ukarabati na kushindwa kutumika tangu kuanza kwa Ligi Kuu msimu huu.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU