TAMBWE PEKE YAKE ANATOSHA YANGA?

TAMBWE PEKE YAKE ANATOSHA YANGA?

1513
0
KUSHIRIKI

Na Oscar Oscar

TAYARI mechi tano za Ligi Kuu Tanzania Bara zimeshachezwa na mwenendo wa bingwa mtetezi, Young Africans, umekuwa wa kusuasua.

Pamoja na kuwa Yanga haijapoteza mchezo hata mmoja, lakini ubutu unaoonekana kwenye idara yao ya ushambuliaji unahitaji kufanyiwa maamuzi magumu. Katika mechi tano zilizopita, Yanga wamefunga magoli manne tu.

Hii si kasi ya Yanga iliyozoeleka katika misimu minne ya hivi karibuni. Kwa kutazama ubora wa timu na idadi ya magoli ya kufunga, Mbao FC, Mbeya City na hata Mwadui zinaonekana bora kuliko Yanga, kwa sababu zimefunga magoli mengi msimu huu.

Hii si Yanga iliyotwaa ubingwa mara tatu mfululizo katika kipindi hiki. Ni Yanga inayohitaji kufanya maamuzi magumu ya kiufundi. Wiki iliyopita taarifa za kurejea kikosini mshambuliaji Amisi Tambwe, zimepokelewa kwa shangwe kubwa na mashabiki na wapenzi wa timu hiyo ya Jangwani, lakini Tambwe peke yake anatosha kuiokoa Yanga? Ni suala la kusubiri na kuona.

Ni kweli Amisi Tambwe ni mshambuliaji mzuri na rekodi zake zinaongea, lakini Yanga inaonekana kuwa na tatizo zaidi ya kumkosa mfungaji mahiri. Ni kweli Tambwe atakuja kupunguza tatizo la

ufungaji walilonalo Yanga, lakini inaonekana kukosa pia watu wenye kasi wa kukimbiza kule mbele. Donald Ngoma ni moja kati ya washambuliaji wapambanaji sana akiwa fiti lakini msimu huu mwili umegoma.

Si Ngoma yule mbabe wa kuzifumania nyavu. Ni Ngoma ambaye anaonekana hayuko sawa. Obrey Chirwa angalau msimu uliopita alianza kuingia kwenye mioyo ya mashabiki wa timu hiyo, baada ya kumaliza msimu akiwa na magoli 12 lakini msimu huu naye anaruka ruka tu ndani na nje ya uwanja.

Lazima benchi la ufundi la Yanga lifanye maamuzi magumu katika kipindi hiki wanachosua sua. Hakuna ubishi kwamba Yanga kwa sasa inategemea zaidi ubora wa Ibrahimu Ajib pale mbele kwenye idara ya ushambuliaji, lakini Ajib peke yake hawezi.

Ajib anahitaji kuzungukwa na wachezaji wenye kasi pale mbele na ukitazama kikosi cha Yanga kwa sasa, utakutana na jina la Emmanuel Martin upande mmoja na upande wa pili kuna Geofrey Mwashiuya. Hawa vijana wanaweza kuiongezea kasi Yanga kwenye idara ya ushambuliaji, wanahitaji imani ya kocha George Lwandamina tu.

Tumewahi kuona Barcelona wakimtumia Cesc Fabregas kama mshambuliaji wa kati na timu yao ikawa na mafanikio. Tumewahi kuona Chelsea wakimtumia Eden Hazard kama mshambuliaji wa kati na wakafanikiwa, achilia mbali Roberto Firmino anavyotumika pale Liverpool. Kwa kipindi kama hiki ambacho wachezaji wa idara ya ushambuliaji halisi hawako sawa Yanga, Ibrahim Ajib anaweza kutumika kama mshambuliaji wa kati na mambo yakaenda.

Ni suala la uthubutu tu ndilo linahitajika hapa. Mpeleke Mwashiuya pembeni kushoto na Emmanuel Martin pembeni kulia kisha muache Ibrahim Ajib kama mshambuliaji wa mwisho. Upo uwezekano mkubwa sana Yanga ikabadilika kwenye idara ya ushambuliaji. Ngoma na Chirwa ni wachezaji wazuri lakini kwa kipindi hiki wanaweza hata kutokea nje ingawa ni maamuzi magumu mno kwa kocha kuyachukua.

Yanga imekosa mfungaji lakini imekosa pia vijana wakimbizaji ndiyo maana kwa kutazama umri na ubora wa Mwashiuya na Martin, nashiwishika kuwa wakipewa nafasi wanaweza kuleta mabadiliko.

Ibrahim Ajib si mshambuliaji wa mwisho kiasilia lakini anajua kufunga. Ni kijana mwenye miguu ya sumaku, akicheza karibu na goli atakuwa msumbufu sana kwa mabeki wa timu pinzani. Lazima kocha akune kichwa kuona ni kwa namna gani timu yake itapita kwenye kipindi hiki kigumu kwao bila kupoteza uelekeo mapema.

Ni kazi ngumu sana kwa George Lwandamina lakini ni lazima aifanye. Hakuna asiyejua ubora wa Donald Ngoma, lakini Ngoma huyu si yule mbabe wa nyavu niliyemzoea. Amisi Tambwe anaweza kurudi lakini Yanga ikakosa wakimbiaji na kusiwe na mabadiliko makubwa wengi wanayotarajia.

Pamoja na kurudi kwake, Martin na Mwashiuya wanahitajika kwa sasa ndani ya kikosi cha kwanza. Mchezo wa soka ni mchezo wa magoli, Yanga wanawajibu wa kuiboresha idara yao ya ushambuliaji mapema.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU