SIMBA MIKAKATI MIZITO

SIMBA MIKAKATI MIZITO

3321
0
KUSHIRIKI

*Niyonzima safii, Bocco ashindwe mwenyewe

NA SAADA SALIM

UONGOZI wa klabu ya Simba umesema kuwa umeweka mikakati kabambe kuhakikisha timu yao inafanya vizuri katika michezo yao ya Ligi Kuu Tanzania Bara, ukiwamo wa wikiendi hii dhidi ya Mtibwa Sugar ili waweze kufikia malengo yao ya kutwaa taji la michuano hiyo msimu huu.

Simba wanaongoza ligi hiyo kwa idadi kubwa ya mabao baada ya kulingana kwa pointi na Mtibwa Sugar pamoja na Azam, zote zikiwa zimefikisha alama kumi na moja, lakini zikitofautiana kwa mabao ya kufunga na kufungwa.

Wakati Simba wakiwa wamecheka na nyavu za wapinzani wao mara 14, wao wamefungwa mabao matatu tu, huku Mtibwa Sugar wakiwa na mabao matano ya kufunga na kufungwa mawili.

Wakati benchi la ufundi likiendelea na programu yake kuhakikisha wanaendelea kukaa kileleni, uongozi nao umeamua kutimiza majukumu yao vilivyo ili mambo yaweze kwenda kama yalivyopangwa.

Akizungumza na BINGWA jana, Katibu Mkuu wa Simba, Arnold Kashembe, alisema tayari viongozi wamekutana na kujadili mambo mbalimbali, zaidi ikiwa ni jinsi ya kutimiza mahitaji ya wachezaji wao na benchi la ufundi, hali itakayowawezesha kuvuna kile wanachokitarajia.

“Tuna imani tukitimiza mahitaji ya wachezaji wetu kwa muda mwafaka pia tukiwaweka katika kambi nzuri na utulivu, bila shaka vijana watatufanyia kazi nzuri na kufikia lengo letu,” alisema.

Kashembe alisema walikutana na benchi la ufundi kujadiliana, ambapo kila mmoja alitoa mikakati yake, wakianzia na mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar utakaochezwa Jumapili kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

“Mtibwa ni timu nzuri na tayari benchi la ufundi linaongozwa na Joseph Omog, wameshatueleza mahitaji yao na tumewatimizia, baada ya hapo tutaangalia mchezo unaokuja na mahasimu wetu Yanga,” alisema.

Katibu huyo alisema suala la kambi ya Yanga wataweka wapi, itajulikana baada ya mchezo wao na Mtibwa.

Alisema baada ya kucheza na Mtibwa, watajiandaa vilivyo kuwakabili Yanga ili kuhakikisha mchezo huo hawapotezi na kuendelea kutoa vipigo katika mechi nyingine zinazofuata, huku akiahidi klabu yao kutofanya makosa ya misimu iliyopita.

Kwa misimu kadhaa iliyopita, Simba imekuwa ikianza vizuri ligi, lakini baadaye ilijikuta ikipotea njia na kutoa mwanya kwa Yanga kufanya vitu vyao na mwisho wa siku, watani wao hao wa jadi kubeba ‘mwali’ kiulaini.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU