HII NDIYO MAANA YA KUJIPANGA KABLA HUJAINGIA KATIKA NDOA

HII NDIYO MAANA YA KUJIPANGA KABLA HUJAINGIA KATIKA NDOA

1246
0
KUSHIRIKI

Na RAMADHANI MASENGA

UNATAKA kuingia katika ndoa? Umejipanga? Mara ngapi umesikia vijana wakiulizwa swali hilo wakiwa katika harakati za kuingia katika maisha ya ndoa?

Umejipanga limekuwa swali ambalo vijana wengi wamekuwa wakiulizwa wakati wa kuingia katika ndoa. Ila bahati mbaya sana majibu yao huwa hayatokani na uelewa halisi wa hili swali.

Wengi hukimbilia kukubali kuwa wamejipanga. Kujipanga kwao humaanisha kuwa na kazi nzuri, akiba ya kutosha benki ama kuwa na maandalizi kabambe ya sherehe.

Kujipanga katika ndoa si suala la kuwa na pesa nyingi tu na kuishi maisha ya anasa. Kim Kardashian na Kris Humphries, walikuwa na mali za kutosha na umaarufu mwingi ila ndoa yao haikufika hata miezi mitano.

Rose Ndauka na Malick Bandawe, hawakuwa na shida ya pesa ya kula ama usafiri ila bado suala lao la kutaka kuingia katika maisha ya ndoa liligeuka kitendawili. Unataka kuingia katika ndoa, je, umejipanga?

Ndoa inahitaji zaidi maandalizi ya kisaikolojia kuliko fedha. Yes, pesa na mali ni muhimu katika malezi ya maisha ya ndoa. Ila si kitu pekee ambacho unatakiwa kuwekeza akili zako zote.

Jiandae kiakili zaidi. Ndoa inahitaji uvumilivu, busara na umakini wa hali juu. Bila kujipanga vizuri katika akili, utaingia katika ndoa leo na kutoka kesho. Umejipanga kuingia katika maisha ya ndoa?

Unaenda kuishi na mtu mwenye akili na mtazamo binafsi. Kuwa na mtu wa aina hii maana yake mnaweza kukoseana, kukwazana ila ukiwa umejiandaa vizuri kichwani huwezi kukimbilia kutoa ama kuomba talaka.

Watu walioingia katika ndoa kwa pupa, kama fasheni ama kwa msukumo wa vitu vingine visivyo na maana katika mapenzi, kwao kuachana ni kitendo cha dakika moja.

Kujipanga kabla ya kuingia katika maisha ya ndoa ni muhimu kwa ajili ya ustawi na furaha yako na mwenzako.

Mwanamume aliyejipanga kabla ya kuingia katika ndoa huwa mwalimu, mvumilivu na mwenye busara katika kutatua changamoto za mahusiano yake.

Mwanamume huyu, hata ikatokea kakosana na mwanamke wake hawezi kukimbilia kumtishia kuachana. Kwake wazo la kuachana huwa mbali kwa sababu kabla hajaingia katika ndoa alijipanga kwa kujiuliza maswali magumu, akatafakari kwa kina uamuzi wake na ndipo akajipiga kifua na kusema naingia katika ndoa na nitapambana na changamoto zake.

Mwanamume aliyejipanga katika ndoa hata kumpiga mke wake akimkosea haiwi kitu rahisi. Kwanini ampige ovyo mtu mwenye kumpenda, kumjali na aliyemkubali kwa kila kitu kabla ya kuingia naye katika ndoa?

Halikadhalika mwanamke aliyejipanga na kujua nini maana ya ndoa huwa mvumilivu kwa mwenzake na mwenye busara. Hawezi kudai talaka kwa maneno ya kuambiwa kuwa mume wake ana mchepuko nje.

Hata ikitokea akaona kuna matatizo katika mahusiano yake na mume wake hutafuta njia mahususi za kutibu mahusiano yao. Kwani mara ngapi wanawake wamewafumania waume zao na kuamua kuwasamehe na maisha kuendelea?

Mwanamke makini hata akikosewa huangalia sababu ya yeye kukosewa na nafasi ya mume wake kutubu na kujirudi. Unataka kungia katika ndoa? Umejipanga?

Sawa umekusanya mali, sawa umepanga kufanya harusi ya kifahari sana. Ila kumbuka hata mwanamuziki Nuh Mziwanda na mke wake waliingia katika ndoa wakiwa na bashasha sana.

Kila mmoja alionekana kumpenda na kumhitaji mwenzake. Nawar, mke wa zamani wa Nuh Mziwanda, mara kadhaa aliwahi kukiri katika vyombo vya habari kwamba anampenda na kumhitaji Nuh Mziwanda.

Zaidi ya mara moja aliwahi kusema hawezi wala hafikirii kumuacha Nuh Mziwanda. Miezi kadhaa baada ya kuingia katika ndoa maneno yake yakapoteza maana na msisimko.

Aliyesema hawezi kumuacha mwenzake, aliyesema anampenda sana mwenzake, akasahau yote. Akamuacha akiwa analia na asijue cha kufanya. Unataka kuingia katika ndoa? Umejipanga?

Ndoa nyingi za vijana zinavunjika sio kwamba hawapendani. Watu wanaachana kwa sababu wakati wanaingia katika ndoa, wao walifikiria mazuri tu, wao walikuwa na zile kumbukumbu za matendo ya starehe na raha tu, kwa fikra hizo sasa walipokutana na magumu katika maisha ya ndoa, wakashangaa, wakapagawa, wakaamua kukimbia.

Ili ndoa yako iwe imara, idumu acha kuikimbilia. Jiulize mara nyingi kadiri inavyowezekana kama umejipanga. Waliojipanga katika ndoa hudumu.

Hawa wakikosea, hata wakikwazana wao ndoa yao inayumba tu na baadaye kukaa katika mstari na raha huendelea kama kawaida.

Aliyewahi kuwa Rais wa Marekani, Bill Clinton, wakati akiwa bado madarakani aliwahi kukumbwa na kashfa ya kujihusisha kingono na mfanyakazi wake wa Ikulu, Monica Lewinsk.

Kashfa ile iliripotiwa na vyombo vingi vya ndani na nje ya Marekani. Kwa namna kashfa ile ilivyokuwa, kila mmoja alijua tamati ya ndoa ya Bill na Hillary ilikuwa imefika.

Maajabu yakatokea. Hillary kila alipokuwa akihojiwa na vyombo vya habari kuhusu habari za mume wake kuwa na mahusiano na Monica.

Alikanusha, akawa anamtetea, akasema ana imani na mume wake na aachwe kwamba hataki maswali ya aina hiyo.

Ingekuwa mwanamke mwingine angemvua nguo hadharani Bill Clinton. Angemponda na kusema anataka kuachana. Ila kichwa cha Hillary kiko vizuri.

Alijipanga kabla ya kuingia kwenye ndoa na kujua ndani yake kuna shida, raha na unahitajika kuwa mvumilivu sana. Unataka kuingia katika ndoa? Umejipanga?

Mwandishi wa makala hii ni mtaalamu mbobezi wa masuala ya ushauri wa uhusiano, maisha na utulivu wa hisia (Psychoanalyst)

ramadhanimasenga@yahoo.com

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU