MO DEWJI APATA WAPINZANI SIMBA

MO DEWJI APATA WAPINZANI SIMBA

7963
0
KUSHIRIKI

NA ZAITUNI KIBWANA

KAMA kuna wanaodhani itakuwa rahisi kwa Mohammed Dewji ‘MO’ kumiliki asilimia 50 za hisa za Simba, watakuwa wanajidanganya kwani tayari wameanza kujitokeza matajiri kadhaa wanaotaka kuwekeza ndani ya klabu hiyo ya Msimbazi.

Habari ambazo Bingwa imezipata tangu mwanzoni mwa wiki hii, zinasema kuwa kuna matajiri wa Simba wameonyesha nia ya kununua hisa za klabu hiyo, wakiwamo wanaotaka kumpiku MO ambaye ametangaza kumiliki asilimia 50.

Japo matajri hao wamekuwa wakiendesha mchakato wao huo kimyakimya kuepuka kupigwa zengwe na ‘Team MO’, lakini ukweli ni kwamba wapo ambao wamejipanga kutangaza dau kubwa zaidi ya lile la mfanyabiashara huyo ili waweze kumpiku na kuwa na hisa kubwa zaidi ya wanahisa wote.

Tayari jina la mmoja wa vigogo wa Simba, Zacharia Hans Poppe, limetajwa katika orodha hiyo, japo mwenyewe alikana alipozungumza kwa simu na BINGWA jana.

Poppe anayeaminika kuwa mmoja wa matajiri waliopo ndani ya Simba, alisema kwamba taarifa hizo si za kweli na hana mpango wa kununua hisa.

Ukiachana na Poppe, wengine wanaotajwa kuchemelea kununua hisa ndani ya Simba ni Said Salum Bakhressa, Kassim Dewji, Crescentius Magori, Azim Dewji na wengineo.

BINGWA jana iliwatafuta baadhi ya watajwa hao ambapo ilifanikiwa kuzungumza na Magori pekee, huku wengine simu zao aidha zikiwa hazikupatikana au kupokelewa.

Akizungumza juu ya madai hayo, Magori alisema hana mpango wa kununua hisa kwani hana fedha za kumwezesha kufanya hivyo.

“Sina uwezo wa kununua hisa kwani zinahitajika fedha nyingi sana, kwa sasa nina fedha za kula tu… kama Mo ananunua asilimia 50 za hisa kwa Sh bilioni 20, maana yake asilimia moja thamani yake ni Sh milioni 400, nani mwenye uwezo wa kununua japo asilimia moja tu ya hisa Simba?” alihoji Magori.

Alisema Simba ina bahati kubwa kupata mtu kama Mo aliyeonyesha nia ya kununua hisa kwa kiasi hicho cha fedha (50% kwa Sh bil 20), hasa kwa kipindi hiki ambacho hali ya uchumi imekuwa ni ngumu mno.

“Huko mbele bei ya hisa itaongezeka na watakaonunua, watanunua kwa bei kubwa zaidi na kuifanya klabu kufanya vizuri zaidi kwani itakuwa na uwezo wa kusajili wachezaji wakubwa Afrika na hata thamani ya klabu itaongezeka,” alisema.

Awali Mo Dewji alitaka kumiliki hisa asilimia 51, lakini wanachama wa Simba walipinga hilo wakitaka apewe asilimia 50 tu ili kuepuka kumfanya kuwa na nguvu zaidi ndani ya klabu hiyo.

Katika kuonyesha kuwa wapo makini na mabadiliko ya kiundeshaji ndani ya klabu yao, wanachama wa Simba tayari wameanza mchakato wa kuwapeleka mbele zaidi kwa kuteua kamati ya usimamizi wa mfumo wa mabadiliko ya uendeshaji klabu.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU