SERIKALI KUWATAFUTIA MDHAMINI BFT

SERIKALI KUWATAFUTIA MDHAMINI BFT

244
0
KUSHIRIKI

NA WINFRIDA MTOI

SERIKALI imeahidi kuwatafutia mdhamini wa kudumu wa timu ya Taifa ya ngumi ili kukabiliana na changamoto za ukata zinazowafanya washindwe kufanya maandalizi ya kutosha ya michuano mbalimbali.

Kauli hiyo ilitolewa juzi na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, alipokutana na uongozi wa Shirikisho la Ngumi Tanzania (BFT).

Akizungumza na BINGWA jana, Katibu Mkuu wa BFT, Makore Mashaga, alisema walifanya kikao na waziri huyo kwa lengo la kujadili mambo mbalimbali yakiwamo maandalizi ya michezo ya Jumuiya ya Madola itakayofanyika Machi mwakani Gold Coast, Australia.

Mashaga alisema katika kikao hicho walimweleza changamoto  wanazokumbana nazo ikiwamo ukosefu wa eneo maalumu la kufanyia mazoezi na  Waziri Mwakyembe kuahidi kuwatafutia mdhamini wa kudumu kwa kushirikiana na shirikisho hilo.

“Hiki ni kikao cha pili tunakutana na waziri mwenye dhamana ya michezo, tumemweleza changamoto zote ambazo ni kikwazo cha maendeleo ya ngumi na ameahidi kushughulikia moja baada ya nyingine,” alisema Mashaga.

Alisema  jambo jingine walilomsisitiza ni kurudisha mchezo huo shuleni kama ilivyokuwa zamani  ili  kuandaa wachezaji kuanzia ngazi ya chini kuliko kutegemea klabu pekee.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU