GEORGE WEAH AKARIBIA KUINGIA IKULU LIBERIA

GEORGE WEAH AKARIBIA KUINGIA IKULU LIBERIA

930
0
KUSHIRIKI

MONROVIA, Liberia

NYOTA wa zamani wa klabu za Chelsea na Manchester City, AC Milan na PSG, aliyewahi kuweka rekodi ya kuwa Mwafrika wa kwanza kutwaa tuzo ya Ballon d’Or, George Weah, anakaribia kuwa rais wa Taifa la Liberia.

Weah, mwenye umri wa miaka 51 kwa sasa, tayari ana cheo cha useneta katika nchi yake hiyo ya Liberia na yupo kwenye kinyang’anyiro kikali cha kuwania urais nchini humo na anapewa nafasi kubwa ya kuingia Ikulu kati ya wagombea 20 wanaowania kuchukua kitu cha mwanamama, Ellen Johnson Sirleaf.

Weah aliichezea Chelsea mechi 15 na kufunga mabao matano, akiichezea kwa mkopo kutoka Milan mapema mwaka 2000. Alijiunga na City mwaka huo huo lakini alicheza mechi tisa tu baada ya kuzozana na kocha, Joe Royle.

Straika huyo aliwahi kutwaa mataji lukuki akiwa na Milan, PSG na Monaco, pia akilitumikia taifa lake la Liberia katika mechi 60.

Sam Mannah, mjumbe wa timu ya kampeni ya Weah, alisema: “Weah yupo katika hali nzuri sana na ana hamu ya uongozi. Kila mtu anamwambia kwamba mabadiliko ni lazima.

“Mwaka 2005 aligombea, ila walisema hana uzoefu, lakini kwa sababu ana cheo cha useneta, wamemkubali.

“Maisha yake ya zamani ya soka yamemsaidia sana. Waliberia wanakumbuka mengi mazuri kutoka kwake. Zamani alilisaidia taifa, akaziwezesha hospitali, alitoa misaada ya chakula na kuwasaidia watu kwenda Marekani na hata kuwalipa wachezaji wa timu ya taifa.

“Watu wanafahamu yote aliyowahi kuyafanya, wanamwona mwenye uwezo wa kubadilisha maisha yao.”

Aidha, mmoja wa wahariri wa gazeti la Liberia, Othello Garblah, aliandika: “Weah ni maarufu sana. Aliahidi kupiga vita rushwa na kuendeleza elimu sambamba na kubuni fursa za kazi.

“Wagombea wote wana mipango hiyo hiyo, hivyo wapiga kura watachagua kulingana na haiba. Umaarufu wa Weah umetokana na maisha yake ya soka.”

Kwa mujibu wa mtandao wa The Sun, uchaguzi huo unafanyika kwa mizunguko kadhaa na matokeo ya mwisho yanatarajiwa kutoka wikiendi hii.

 

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU