LOLA OMOTAYO; MWANAMKE ANAYETAJWA KUIVUNJA P SQUARE

LOLA OMOTAYO; MWANAMKE ANAYETAJWA KUIVUNJA P SQUARE

1008
0
KUSHIRIKI

LAGOS, Nigeria

HABARI za kuvunjika kwa Kundi la P Square linaloundwa na mapacha Peter na Paul, si ngeni tena ingawa ziliwashangaza wadau wengi wa muziki barani Afrika.

Kwa ubora wa tungo zake, kundi hilo liliweza kujizolea umaarufu mkubwa hata kwenye soko la tasnia ya burudani la kimataifa. Mfano mzuri ukiwa ni kufikia hatua ya kufanya kazi na staa wa hip hop nchini Marekani, Rick Rose.

Kuvunjika kwa P Square kuliibuliwa na taarifa ya Peter mwenyewe alipowaambia mashabiki wake kuwa amejitoa na ataanza kufanya kazi zake mwenyewe.

“Watoto 30 hawawezi kuishi pamoja kwa miaka 30. Imefikia hatua ya kutoheshimiana. Si suala la kugombea sifa au cheo, ni heshima tu. Heshima binafsi na kwa familia pia,” alisema Peter.

Aidha, Peter ambaye kwa sasa anataka afahamike kwa jina la Mr Paul, aliongeza kuwa anajutia kuchanganya udugu na biashara, jambo ambalo aliapa kutolirudia.

“Kwa mashabiki, tunawaomba radhi. Huwezi kutaka P Square jukwaani wakati hawaelewani. Nimejaribu kutuliza hali ya mambo lakini imeshindikana … Nimenyoosha mikono kwa ajili ya heshima ya familia ya kila mmoja,” alisema.

Kwa kile ambacho hata Peter alikiri familia yake na ya kaka yake Paul zimekuwa maadui kwa takribani miaka minne sasa.

Mashabiki wanaamini kuwa mke wa Peter, Lola Omotayo ndiye chanzo cha kundi hilo kuvunjika na wamekuwa wakimtupia maneno makali, hata kumwita ‘mchawi’. Kwa mujibu wao, Omotoya ndiye aliyemshawishi Peter kujitoa kwenye kundi hilo.

Wamedai kuwa mwanamama huyo mwenye asili ya Urusi, amekuwa akitamani kuwa msimamizi wa kazi za mume wake huyo kwa muda mrefu.

Wapo mashabiki walioenda mbali zaidi na kudai kuwa hata mama mzazi wa wasanii hao ambaye ameshafariki, hakuwa na maelewano mazuri na Omotayo.

Inaelezwa kuwa mama alihisi msomi huyo wa Shahada ya Sanaa alitaka kuwa meneja wa Kundi la P Square, cheo anachokishikilia Jude Okoye ambaye ni kaka wa Peter na Paul.

Kuna wanaoamini pia kuwa kama mama mzazi huyo angekuwa hai, basi asingekubali kuona mwanawe Peter akifunga ndoa na Omotayo kwani ni mwanamke aliyemuona nuksi kwenye familia yao.

Eti, Peter naye alikuwa akimuunga mkono mkewe huyo, akionesha kutokubali utendaji kazi wa kaka yake Jude, ikizingatiwa kuwa licha ya umaarufu wake, kundi hilo halijawahi kuwa na ofisi za kibiashara.

“Miaka minne iliyopita, nilimwambia Jude ajiuzulu kwa sababu sikutaka kumshushia heshima yake kama kaka, lakini hii ni biashara, lazima tuwe na mfumo,” alisema Peter. “Jina la P Square ni kubwa lakini kundi halina mfumo.

Pia, chanzo kingine kilinyetisha kwamba sababu ya Peter kumtaka Omotayo awe meneja badala ya Jude ni kwamba, ni mkewe huyo ndiye aliyemsaidia kupata dili kibao za matangazo.

Ikumbukwe kuwa kwa kipindi chote hicho, Paul hakuwa akimuunga mkono Peter, jambo ambalo lilisababisha achukiwe na shemeji yake huyo.

Hata hivyo, mpaka sasa mashabiki wa Omotayo nao hawako nyuma kumtetea staa wao huyo, wakisema anachukiwa na familia ya mume kwa sababu ya kabila lake.

Hao ni wale wanaoamini kuwa familia ya akina Peter haikufurahia kuona mtoto wao akioa mwanamke kutoka kabila la Yoruba na ndiyo maana hata Jude hakuihudhuria sherehe ya harusi ya mdogo wake huyo.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU