TOFAUTI YA TUZO WALIZOTUNUKIWA KIBA, DIAMOND KWENYE LEBO ZAO

TOFAUTI YA TUZO WALIZOTUNUKIWA KIBA, DIAMOND KWENYE LEBO ZAO

1712
0
KUSHIRIKI

NA CHRISTOPHER MSEKENA

MTAANI bado kuna sintofahamu juu ya tuzo ambazo wasanii wa Bongo Fleva, Ali Kiba na Diamond Platnumz, wametunukiwa na lebo zao ambazo zimekuwa na utaratibu wa kuwatunuku wasanii wake pale ambapo nyimbo zao zinapofanya vizuri au kuweka rekodi fulani.

Lebo kubwa kama Warner Music Group (WMG), Sony Music Entertainment (SME) na Universal Music Group (UMG) zimekuwa na utaratibu huo wa kuwapa tuzo wasanii wanaowasimamia ili kuwapa motisha na kuongeza ushindani wa kutoa kazi nzuri zitakazoendelea kutikisa duniani.

Kama ulikuwa hufahamu, Ali Kiba, ni msanii ambaye kazi zake zinasimamiwa na lebo ya Sony Music Entertainment (SME) na Diamond Platnumz kazi zake zinasambazwa na lebo ya Universal Music Group (UMG) ambazo zote zina makao yake makuu New York, Marekani na matawi yake ya Johannesburg, Afrika Kusini.

Februari mwaka huu lebo ya Sony ilimtunuku Ali Kiba tuzo ikimpongeza kuwa msanii aliyefikisha watazamaji milioni 5 kwa muda mfupi kwenye mtandao wa YouTube kupitia wimbo wake wa Aje alioutoa mwaka jana. King Kiba alikuwa msanii wa kwanza Afrika Mashariki kupewa tuzo hiyo na Sony kati ya wasanii wote waliowahi kusimamiwa na Sony.

Tuzo hiyo ina mwonekano wa picha kubwa ikiwa ndani ya fremu na maneno ya pongezi yakionyesha lengo hasa la tuzo hiyo kwa msanii husika na hakika inatia moyo kuona kazi ambayo umefanya imefanikiwa na kuonekana mpaka uongozi umeamua kukutunuku tuzo.

Pia wiki iliyopita, Diamond Platnumz, alipewa tuzo na lebo yake ya Universal Music Group kufuatia wimbo wake wa Marry You aliomshirikisha Ne-Yo kufikisha mauzo ya nakala kwa kiwango cha Platnum mara sita mfululizo kwa mjumuisho wa mauzo kutoka kwenye maduka yanayouza nyimbo kama vile iTunes, Spotify, Deezer na mingineyo.

Hapa watu wengi wamechanganya kwa kuhusisha na YouTube. Unapaswa kufahamu kuwa tuzo hiyo aliyopewa Diamond haihusiani kabisa na YouTube ni mauzo yaliyopatikana kwenye maduka ya mtandao yanayouza nyimbo pekee kwani YouTube hawauzi nyimbo zaidi ya kuangalia bure video za muziki.

Tuzo hiyo imegawanywa katika madaraja tofauti kulingana na kiwango ambacho msanii atafikia. Kiwango cha chini kabisa ni Silver kikifuatiwa na Gold kisha Platnum na mwisho kabisa ni Diamond hivyo basi Diamond Platnumz amepata daraja la tatu (Platnum).

Diamond amekuwa ni msanii wa kwanza Afrika aliyesainiwa na lebo ya Universal Music Group (UMG) kutunukiwa tuzo hiyo kwa kuuza nakala laki 6 mara 6 mfululizo kwa kuwa Platnum moja kwa mfumo wa Marekani ni nakala laki 6.

Mjadala mkubwa umeibuka pale ambapo Diamond alitamba kuwa yeye ndiye msanii wa kwanza Afrika kupata tuzo hiyo kisha mashabiki wakamkumbusha yeye si wa kwanza kwani hata Ali Kiba naye aliwahi kupata tuzo kama hiyo kabla yake.

Ukweli ni kwamba, tuzo aliyotunukiwa Ali Kiba na ile aliyotunukiwa Diamond ni tofauti kabisa na hazipaswi kulinganishwa kwa namna yoyote ile kwani wasanii hawa wapo lebo mbili tofauti zinazotunuku wasanii wake kwa mitindo tofauti. Ali Kiba ni mbabe kwa upande wake wa Sony na Diamond pia ni mbabe kwa upande wake wa Universal.

Hali kadhalika, Ali Kiba, alitunukiwa tuzo na lebo yake ya Sony Music Entertainment kutokana na wimbo wa Aje kufikisha watazamaji milioni 5 kwa muda mfupi huku Diamond ametunukiwa tuzo hiyo kwa na lebo yake kwa kuuza wimbo wa Marry You mara sita mfululizo katika kiwango cha Platnum.

 

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU