MABINGWA ULAYA… DAH! HIZI ZIKO HATARINI KUIKOSA 16 BORA

MABINGWA ULAYA… DAH! HIZI ZIKO HATARINI KUIKOSA 16 BORA

1022
0
KUSHIRIKI

LONDON, England

UHONDO wa Ligi ya Mabingwa Ulaya umefikia patamu ambapo sasa kuna hatari ya baadhi ya timu kuikosa hatua inayofuata ya 16 bora.

Kwa mujibu wa sheria za Shirikisho la Soka Ulaya, katika makundi nane timu mbili za juu zitafuzu kuingia hatua hiyo na zile zitakazoshika nafasi ya tatu zitatupwa Ligi ya Europa.

Lakini je, ni timu zipi zilizo kwenye hatari ya kutoingia kwenye hatua ya mtoano msimu huu wa Ligi ya Mabingwa Ulaya?

Atletico Madrid

Wakali hao wa La Liga wako Kundi C ambalo lina Qarabag FK ya Azerbaijan, Chelsea na AS Roma.

Baada ya droo ya makundi iliyofanyika Agosti mwaka huu, ilionekana kuwa ni Atletico Madrid, Roma na Chelsea ndizo zingefuzu.

Hata hivyo, ni Atletico ya kocha Diego Simeone ndiyo iliyo kwenye hatari ya kutokwenda 16 bora, hasa baada ya sare yao dhidi ya Qarabag.

Mbaya zaidi, michezo miwili iliyobaki inayoweza kufufua matumaini ni dhidi ya Roma na Chelsea.

Atletico wana mabao mawili pekee katika michezo yao miwili waliyocheza, wanashika nafasi ya tatu kwenye kundi hilo linaloongozwa na Roma ambao hawajapoteza hata mchezo mmoja, huku Chelsea wakiwa nafasi ya pili.

Napoli

Katika Kundi F, Napoli wako na Feyenoord, Shakhtar Donetsk na Man City walioko kileleni.

Licha ya kiwango kizuri walichonacho Ligi Kuu Italia Serie A, Napoli yenye pointi tatu pekee, imeshindwa kutamba kwenye kundi lao ikiziacha Man City (12) na Shakhtar (9).

Hata hivyo, inaelezwa kuwa Napoli hawaitolei jicho michuano ya Ligi ya Mabingwa kwa kuwa wanaona kuna uhakika wa kubeba taji la Serie A.

Mpango alionao kocha Maurizio Sarri ni kuhakikisha wanaikaba koo Juve na kutwaa taji la Serie A ambalo kwa mara ya mwisho waliinyakua katika msimu wa 1989-90.

Borussia Dortmund

Wababe hao wa Bundesliga wako Kundi H, wakiwa na Tottenham, Real Madrid na Apoel Nicosia.

Ni Spurs pekee ambayo haijapoteza mchezo, hivyo imefuzu moja kwa moja kwenda 16 bora.

Ili Dortmund ifuzu, italazimika kuichapa Madrid inayoshika nafasi ya pili, lakini pia iombe Apoel iifunge timu hiyo ya La Liga.

AS Monaco

Japo msimu uliopita walifika nusu fainali, hali ni mbaya kwa Monaco kwenda 16 bora msimu huu. Kuondokewa na mastaa wao watatu wa kikosi cha kwanza; Kylian Mbappe, Tiemoue Bakayoko na Bernardo Silva, kumeonekana kuwavuruga.

Lakini pia, katika mechi sita za ugenini zilizopita kwenye michuano hii ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, timu hiyo imeshinda mara moja pekee.

Mpachikaji mabao Ramadel Falcao hajawa kwenye ubora wake Ligi ya Mabingwa msimu huu, akiwa amefunga bao moja pekee hadi sasa, licha ya kuwa na 13 kwenye ligi.

Monaco wanaburuza mkia Kundi G, wakiwa hawajashinda hata mchezo mmoja kati ya minne, wakitoa sare mbili.

Ili kufuzu, Monaco wanatakiwa wazifunge RB Leipzig na Besiktas, ambazo zina nafasi kubwa ya kufuzu.

Sporting Lisbon

Tangu mwanzo, Kundi D lilikuwa linatabirika kwa kuwa lina Barcelona na Juventus, ambazo ndizo zilizokuwa zikipewa nafasi ya kwenda 16 bora.

Uzembe wa Lisbon ya Ureno ulikuwa ni kupata ushindi mwembamba wa mabao 3-2 dhidi ya Olympiacos licha ya kwamba walikuwa wanaongoza kwa mabao 3-0 katika kipindi cha kwanza.

Katika mchezo wa pili, waliweza kuibana mbavu Barca lakini wakajikuta wakipoteza matokeo kwa bao la kujifunga la Sebastian Coates.

Ikiwa nafasi ya tatu nyuma ya Juve na Barca, Lisbon sasa watahitaji ushindi katika michezo yao miwili iliyobaki ukiwamo mmoja dhidi ya Barca.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU