MAKOCHA WALIOKUWA MABEKI ZAMANI WANAVYOTAWALA VPL

MAKOCHA WALIOKUWA MABEKI ZAMANI WANAVYOTAWALA VPL

1377
0
KUSHIRIKI

NA WINFRIDA MTOI

MARA nyingi mashabiki hufikiria kwamba makocha wanaofanikiwa kwenye soka ni wale ambao kwenye zama zao za uchezaji walicheza nafasi ya kiungo, au ushambuliaji kama ilivyo kwa kocha wa Manchester City, Pep Guardiola na Zinedine Zidane wa Real Madrid, ambao wote walikuwa viungo.

Bila kujua kwamba kuna makocha wengine ambao zamani walikuwa mabeki na wengine hata soka lenyewe hawakulicheza kama ilivyokuwa kwa Jose Mourinho wa Manchester United.

Hili nalo limejitokeza Ligi Kuu Tanzania Bara, ambapo makocha wengi wanaozinoa timu za ligi hiyo zama zao za uchezaji walikuwa mabeki, huku idadi inayofuata ya makocha hao wakiwa ni viungo na washambuliaji wachache.

BINGWA limeorodhesha makocha kadhaa na nafasi zao walizokuwa wakicheza zamani na nafasi wanazoshika kwa sasa katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Joseph Omog (beki)

Kocha wa Simba, Joseph Omog wa Cameroon zamani alikuwa akicheza nafasi ya beki kwenye klabu kama Dragon Yaounde, ambapo aliinoa Azam FC msimu wa 2013/2014 na 2014/2015 kabla ya kutua kwa Wekundu wa Msimbazi msimu uliopita.

Kocha huyo ambaye aliisaidia AC Leopards kubeba Kombe la Shirikisho Afrika mwaka 2013, amekisaidia kikosi cha Simba kukusanya pointi 16, baada ya kushinda mechi nne na kutoka sare nne na sasa wanashika nafasi ya nne, lakini wataweza kurejea kileleni kama wakishinda au wakipata sare dhidi ya Mbeya City, mechi ambayo ilitarajiwa kuchezwa jana jioni kwenye Uwanja wa Sokoine.

George Lwandamina (beki)

Kocha huyo raia wa Zambia, anainoa timu ya Yanga aliyojiunga nayo katikati ya msimu uliopita akitokea Zesco akichukua nafasi ya Hans van der Pluijm. Licha ya kuwa hajacheza soka kwa muda mrefu kutokana na majeraha yaliyokuwa yanamsumbua, alikuwa ni miongoni mwa mabeki waliowahi kuwamo kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Zambia.

Hans van der Pluijm (kipa)

Baada ya kuisaidia Yanga kutwaa mataji matatu ya Ligi Kuu Tanzania Bara akiwa timu ya Yanga, kocha wa Uholanzi, Hans van der Pluijm sasa amejiunga na Singida United msimu huu na sasa kikosi chake kinashika nafasi ya sita baada ya mechi tisa ikishinda tatu, wakitoka sare mechi tano ikiwamo dhidi ya klabu yake ya zamani waliocheza mwishoni mwa wiki iliyopita.

Pluijm ambaye aliamua kustaafu kucheza soka miaka ya 1980, alikuwa akicheza nafasi ya mlinda mlango kwenye klabu ya FC Den Bosch nchini Uholanzi.

Aristica Cioaba (kiungo mkabaji)

Kocha huyo wa Romania, Aristica Cioaba, msimu uliopita alionekana kushindwa kuifanya Azam FC kuwa bora lakini amejipanga na msimu huu anaonekana yuko kivingine kutokana na kikosi chake kung’ang’ania nafasi za juu katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kwa sasa Azam wanaongoza ligi hiyo wakiwa na pointi 19, baada ya kushinda mechi tano wakitoka sare nne, lakini wanaweza kushushwa na Simba ambao walitarajiwa kucheza dhidi ya Mbeya City, lakini Arista ambaye zamani alikuwa kiungo mkabaji ameonekana anaweza kufanya maajabu msimu huu kwa kuifanya klabu hiyo ya Chamazi kuwa kati ya timu zinazowania ubingwa msimu huu.

Malale Hamsini (beki)

Beki huyo wa zamani wa Mlandege na JKU za Visiwani Zanzibar, Malale Hamsini, kwa sasa anainoa Ndanda FC ambayo inashika nafasi ya tisa ikiwa na pointi 10, baada ya kushinda mechi mbili na kutoka sare nne. Pia aliwahi kuzifundisha KMKM, JKT Ruvu na Ruvu Shooting, ambao ameachana nayo msimu uliopita.

Etienne Ndayiragije (kiungo, mshambuliaji)

Etienne Ndayiragije amejitambulisha Tanzania kwa soka lake linalochezwa na vijana wake wa Mbao FC, ambao walipanda msimu uliopita na kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho Tanzania mwaka jana dhidi ya Simba na kufungwa 2-1 kwa tabu, pia alifanikiwa kuibakiza timu hiyo Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kuwa kwenye hatari ya kushuka daraja.

Kocha huyo, Ndayiragije, ambaye enzi zake akicheza soka alicheza nafasi ya kiungo na mshambuliaji, imeisaidia Mbao FC kukusanya pointi nane na kushika nafasi ya 10, akishinda mechi moja akitoka sare tano katika mechi tisa alizocheza msimu huu.

Mecky Mexime (beki)

Msimu huu umekuwa mbaya kwa beki wa zamani wa Mtibwa Sugar na timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Mecky Mexime, ambaye msimu uliopita alimaliza Ligi Kuu akiwa nafasi ya tatu na kikosi chake cha Kagera Sugar.

Lakini ushindi wao wa mabao 2-1 dhidi ya Ndanda FC wiki mbili zilizopita na sare ya mwishoni mwa wiki iliyopita dhidi ya Tanzania Prisons, imeisaidia timu yake ya Kagera kutoka nafasi za timu zitakazoshuka daraja ambapo kwa sasa wana pointi saba wakishika nafasi ya 13 baada ya kushinda mechi hiyo moja na sare nne.

Habibu Kondo (beki)

Majimaji ambayo inashika nafasi ya 11 ikiwa imeshinda mechi moja na kutoka sare tano, wakipoteza mechi tatu na kukusanya pointi nane wananolewa na kocha Habibu Kondo, ambaye enzi zake alikuwa akimudu kucheza beki wa beki wa kulia, kushoto, kati, kiungo mkabaji na timu yake ya mwisho kuichezea ilikuwa Mtibwa Sugar mwaka 2004.

Amri Said (beki)

Beki wa zamani wa Simba, Amri Said, sasa anakionoa kikosi cha Lipuli ambacho kinashika nafasi ya saba baada ya kushinda mechi tatu, kufungwa mbili, kutoka sare tatu na kukusanya pointi 12, jana walitarajiwa kucheza dhidi ya Mwadui mechi ambayo itawafanya wapande hadi nafasi ya sita kama watakuwa wameshinda.

Mrage Kabange (winga)

Hakuna nafasi nyingine aliyomudu kucheza zaidi ya ushambuliaji na timu aliyokaa muda mrefu ni Simba kwa miaka 10 mfululizo hadi alipostaafu miaka ya 1990. Hivi sasa ni kocha wa Njombe Mji akirithi mikoba ya Hassan Banyai aliyejiuzulu na sasa timu hiyo inashika nafasi ya 14 ikishinda mechi moja pekee na kutoka sare nne na kufungwa nne kati ya tisa walizocheza.

Zubery Katwila (kiungo mshambuliaji)

Zubery Katwila ndiye kocha wa Mtibwa Sugar wanaoshika nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ikiwa na pointi 16 ila wanategemea matokeo ya mechi ya Simba dhidi ya Mbeya City iliyotarajiwa kuchezwa jana ambapo Wekundu wa Msimbazi wakishinda au kutoka sare, basi Mtibwa watashuka hadi nafasi ya nne.

Katwila aliyestaafu soka msimu wa 2012/13 akiwa na Mtibwa, alikuwa anamudu kucheza nafasi ya beki, kiungo na hata ushambuliaji.

Jumanne Ntambi (kiungo)

Jumanne Ntambi alirejeshwa na Mwadui FC msimu huu wa Ligi Kuu Tanzania Bara akitokea Panone FC inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza. Ntambi ambaye zamani alicheza nafasi ya kiungo sasa anaiongoza timu hiyo inayoshika nafasi ya 12 ikiwa imeshinda mechi moja na kutoka sare nne, wakifungwa mechi tatu na kukusanya pointi saba.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU