SABABU HIZI ZISIKUFANYE UANZISHE MAHUSIANO

SABABU HIZI ZISIKUFANYE UANZISHE MAHUSIANO

873
0
KUSHIRIKI

Na RAMADHANI MASENGA

KILA kitu ili kiweze kudumu ni lazima kiwe na msingi imara katika uanzishwaji wake. Ni hivyo hata katika suala la mapenzi.

Ikiwa kweli unataka kudumu nakufurahia mahusiano yako kuna baadhi ya mambo si rahisi kuyaepuka. Miongoni mwake, ni lengo la kuanzisha mahusiano yako.

Dhamira au lengo lako la kuanzisha mahusiano ndilo litatoa jibu halisi na picha ya hayo mahusiano yako jinsi yatakavyokuwa. Katika hili ni lazima kuwa makini zaidi ili kujiepusha kuingia katika mahusiano ambayo baadaye yatakuletea karaha na maudhi. Mahusiano yatakayokufanya ujutie uamuzi wako au kufikia hatua ya kuanza kuhisi watu wa jinsia flani hawana maana. Tuangalie hizo sababu kwa makini.

KWA KUWA HUNA MTU

Hii ni moja ya sababu ambazo zinatumiwa na wengi katika suala la kuanzisha mahusiano. Ni kweli mtu hatakiwi kuanzisha mahusiano mengine akiwa tayari yuko ndani ya mahusiano.

Ila kutokuwa na mtu haitakiwi kuwa ndiyo sababu ya msingi ya kuanzisha mahusiano yako, kwa sababu si kila asiye na mpenzi kwa sasa ni lazima awe naye. Mtu anapaswa kuingia katika mahusiano kwa kuvutwa na upendo kwa mhusika. Si kwa sababu yuko nje ya mahusiano.

Mara nyingi watu wanaoanzisha mahusiano kwa sababu hii baadaye hujikuta wakijilaumu kwa maamuzi waliyofikia. Hii inatokana na ukweli kwamba, mhusika baada ya kudumu katika mahusiano kwa muda mrefu hujihisi kuanza kuchoka. Kwanini?

Yule aliye naye hakumpenda bali alikuwa naye katika kipindi ambacho alihitaji ‘kampani tu’. Pia watu wa aina hii ambao hukurupuka kuanzisha mahusiano kwa kigezo cha kutokuwa na mpenzi, hujikuta  njia panda (in dilema) baada ya kuwaona wale ambao kweli nafsi zao zinawahitaji katika maisha na si katika kipindi kifupi. Chunguza nafsi yako kwa makini, ndiyo uamue kuwa na mtu na si kwa sababu huna mtu.

UZURI

Ni kosa ambalo hutumiwa na watu wengi na mwishowe hujikuta wakijuta. Ni vyema ikatambulika kuwa asili ya kila binadamu nikuwa na tamaa. Lakini pa ni vema ikajulikana kuwa kila mmoja ana uwezo wa kudhibiti hali yake ya tamaa.

Jicho la binadamu huwa likiangalia kitu chochote kizuri au chenye kuleta mshawasha wa aina yoyote ile akili hupenda kuamini kuwa ni kitu kinachofaa, hata kama siyo. Hiyo husababishwa na hali ya tamaa ambayo ni asili ya binadamu. Hata katika suala la mapenzi huwa hivyo.

Macho yakimwona mvulana mtanashati au msichana aliyevaa vizuri na kupendeza haraka wazo huja kuwa yule ndiye mtu sahihi wa kuishi naye. Na mara moja unajikuta ukianza kufanya mipango ya namna ya kumpata. Tamaa inafanya kazi yake.

Na mara zote mapenzi ya namna hii hayawezi kukuletea furaha na amani. Tamaa huwa haina maisha marefu. Baada ya kuishi naye kwa muda flani au kufanya naye ngono utahisi kuanza kumchoka au kumwona hana jipya. Kwanini? Kwa sababu chanzo cha yote ni tamaa na si upendo. Upendo huwa hauozi.

Upendo siku zote huwa na uwezo wa kuhimili vipindi vyote katika maisha. Hata siku moja watu wanaopendana kwa dhati hawawezi kuchokana au kudharauliana. Lakini kwa mtu uliyemtamani inawezekana. Unaweza leo ukamwambia yeye ni mzuri kama malaika, lakini baada ya kukutana naye kimwili ukamwambia hana kitu. Hiyo ndiyo tamaa bwana!

MALI

Ukimpapatikia kwa sababu ya mali zake jua unaenda kuishi katika tanuru. Hakuna raha hapo. Ni kweli katika siku za mwanzoni utafurahia maisha na kuamini kuwa umepata bahati kuu katika maisha yako kuwa na yeye.

Hiyo ni kutokana na asili ya mwanadamu ya kuwa na hamu na kitu au vitu vipya vyenye taswira ya kumfurahisha au kumrahisishia jambo. Lakini baada ya kumzoea yeye na mali zake hapo ndiyo balaa litaanza. Utahisi kukosa kitu muhimu.

Asikwambie mtu kuishi na mtu ambaye moyo wako hujamridhia kwa dhati ni zaidi ya balaa. Nafsi hukataa kuwa na furaha. Kila unachofanya utahisi bado kuna kitu unapaswa kuwa nacho. Utamwona kama askari jela.

Uwepo wake ni mara nyingi utakuwa haukufurahishi. Utahisi kama anakubana vile. Si ajabu akipata safari kujihisi na wewe umepata ahueni badala ya kuona kuwa ‘utammis’.

Mali za mtu haipaswi kuwa sababu hata kidogo ya kukufanya uanzishe mahusiano yako ya kimapenzi. Thamini utu wako na jiamini.

KABILA

Jambo hili kwa mjini si sana, tatizo liko vijijini. Kila siku watu wanalazimishwa ama kushauriwa kuoa au kuolewa na watu wenye ufanano nao wa makabila. Lakini hebu chunguza kabila lake katika mahusiano yenu linasaidia nini? Ukipata jibu, utajua ni kwanini nakwambia si sababu ya kukufanya uoe au uolewe.

Ushauri ni kwa malipo.

ramdhanimasenga@yahoo.com

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU